Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 8 November 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 51....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.” Watu zaidi ya arubaini ndio waliokula njama kufanya hivyo.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, “Sisi tumekula kiapo kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo. Sasa basi, nyinyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumwua hata kabla hajafika karibu.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Lakini mtoto wa ndugu yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo. Hapo Paulo akamwita mmoja wa maaskari, akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia.”
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Maneno ya faraja kwa Siyoni
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nisikilizeni enyi mnaotaka kukombolewa,
nyinyi mnaonitafuta mimi Mwenyezi-Mungu.
Utazameni mwamba mlimochongwa,
chimbo la mawe mlimochimbuliwa.
2Mkumbukeni Abrahamu babu yenu,
na Sara aliyewazaa nyinyi.
Abrahamu alikuwa hana mtoto wakati nilipomwita,
lakini nilimbariki na kumfanya kuwa na wengi.
3“Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji mji wa Siyoni,
nitaparekebisha mahali pake pote palipoharibika.
Nyika zake nitazifanya kama bustani ya Edeni,
majangwa yake kama bustani ya Mwenyezi-Mungu.
Kwake kutapatikana furaha na shangwe,
na nyimbo za shukrani zitasikika humo.
4“Nisikilizeni enyi watu wangu,
nitegeeni sikio enyi taifa langu.
Sheria na haki zitatoka kwangu mimi;
nazo zitakuwa mwanga wa mataifa.
5Nitaleta ukombozi hima;
wokovu nitakaoleta waanza kutokea.
Mimi mwenyewe nitayatawala mataifa.
Wakazi wa nchi za mbali wananingojea,
wanaitegemea nguvu yangu.
6Inueni macho mzitazame mbingu,
kisha tazameni dunia huko chini.
Mbingu zitatoweka kama moshi,
dunia itachakaa kama vazi,
na wakazi wake watakufa kama wadudu.
Lakini wokovu niuletao wadumu milele;
ukombozi wangu kamwe hautakoma.
7“Nisikilizeni enyi mjuao mambo ya haki,
ambao sheria zangu zimo mioyoni mwenu.
Msiogope dharau za watu,
wala kufadhaishwa na masimango yao.
8Maana wataliwa na nondo kama vile vazi;
viwavi watawala kama walavyo nguo ya sufu.
Lakini ukombozi niletao mimi utadumu milele;
wokovu wangu hautakuwa na mwisho.”
9Amka! Amka ee Mwenyezi-Mungu!
Jivike nguvu zako utuokoe.
Amka kama ulivyofanya hapo zamani,
nyakati za vizazi vya hapo kale.
Je, si wewe uliyemkatakata Rahabu,
ukalitumbua dude hilo la kutisha?
10Wewe ndiwe uliyeikausha bahari,
ndiwe uliyevikausha vilindi vya maji,
ukafanya njia katika vilindi vya bahari,
ili wale uliowakomboa wavuke humo.
11Watu wako uliowakomboa, ee Mwenyezi-Mungu, watarudi,
watakuja Siyoni wakiimba;
watajaa furaha ya milele,
watapata furaha na shangwe.
Huzuni na maombolezo vitatoweka kabisa.
12Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Mimi, naam mimi, ndimi ninayekufariji.
Kwa nini wewe unamwogopa mtu ambaye hufa,
binadamu ambaye hutoweka kama nyasi?
13Wewe umenisahau mimi Mwenyezi-Mungu Muumba wako,
niliyezitandaza mbingu,
na kuiweka misingi ya dunia!
Wewe waendelea kuogopa siku zote,
kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu wako,
kwamba yuko tayari kukuangamiza!
Lakini hasira yake itafika wapi?
14Wanaodhulumiwa watafunguliwa hima,
hawatakufa na kushuka shimoni,
wala hawatatindikiwa chakula.
15Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wako;
nivurugaye bahari, mawimbi yake yakanguruma;
Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina langu!
16Nimeyaweka maneno yangu mdomoni mwako;
nimekuficha katika kivuli cha mkono wangu.
Mimi nilizitandaza mbingu,
nikaiweka misingi ya dunia.
Mimi nawaambieni enyi watu wa Siyoni:
‘Nyinyi ni watu wangu.’”
Mwisho wa mateso ya Yerusalemu
17Amka ewe Yerusalemu!
Amka usimame wima!
Mwenyezi-Mungu amekunywesha kikombe cha ghadhabu yake,
nawe umeinywa mpaka tone la mwisho,
mpaka ukayumbayumba.
18Kati ya watoto wote uliowazaa
hakuna yeyote wa kukuongoza.
Hakuna hata mmoja wa kukushika mkono
kati ya watoto wote uliowalea.
19Majanga haya mawili yamekupata:
Uharibifu na maangamizi; njaa na mauaji.
Nani atakayekuonea huruma?
Nani atakayekufariji?
20Watoto wako wamezirai,
wamelala pembeni mwa kila barabara,
wako kama paa aliyenaswa wavuni.
Wamepatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu,
wamepatwa na adhabu ya Mungu wako.
21Basi, sikiliza ewe Yerusalemu unayeteseka;
sikiliza wewe uliyelewa, lakini sio kwa divai.
22Bwana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
awateteaye watu wake, asema hivi:
“Nimekuondolea kikombe cha kuyumbisha,
hutakunywa tena kikombe cha ghadhabu yangu.
23Nitawanywesha watesi wako kikombe hicho
waliokuambia ulale chini wapite juu yako;
wakaufanya mgongo wako kama ardhi,
kama barabara yao ya kupitia.”

Isaya51;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: