Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 31 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 2...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Muweza wa yote,Alfa na Omega,Mungu wa walio hai,Mungu wenye nguvu
Mungu mwenye huruma,Mungu anayetenda,anayejibu,Mponyaji wetu
Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu
hakuna kama wewe ee Baba wa Mbinguni,Neema yako yatutosha Mfalme wa amani..!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu..!!

Siku moja, watozaushuru na wenye dhambi wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakaanza kunungunika: “Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao.” Yesu akawajibu kwa mfano: “Hivi, mmoja wenu akiwa na kondoo 100, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu.

Tunakuja mbele zako ee Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mfalme wa amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,Yeyye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

“Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.”

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukavibariki  vyote tunavyoenda kugusa/kutumia,Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika  kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo...
Mungu wetu tunaomba Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu
Yahweh ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Jehovah tukawe salama moyoni Yahweh ukatupe macho ya kuona masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh ukatufanye chombo chema Jehovah tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume. Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake. Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. Akaomba kazi kwa mwananchi mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. Alipoanza kupata akili, akafikiri: ‘Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu. “Mwanae akamwambia: ‘Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.’ Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: ‘Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! Mchinjeni ndama mnono; tule na kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu; alikuwa amekufa, kumbe yu hai; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kufanya sherehe. “Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani, akasikia vifijo na ngoma. Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: ‘Kuna nini?’ Huyo mtumishi akamwambia: ‘Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.’ Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. Lakini yeye akamjibu: ‘Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwanambuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.’ Baba yake akamjibu: ‘Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu,Mungu wetu ukawape macho ya rohoni wanaokutafuta kwa bidii na imani,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako,Yahweh ukawaamshe na kuwasimamisha waliopotea..
Mungu wetu ukawasamehe wote waliokwenda kinyume nawe 
na wameamua kukurudia/kutubu na kukutafuta wewe..
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Neema yako ikawe nao,amani ikatawale katika maisha yao,furaha na baraka ziwafuate..
Mungu wetu ukawaongoze na kuwalinda,Baba wa Mbinguni ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwa kuwa nami/kunisoma
Mungu aendelee kuwalinda na kuwabariki katika yote ..
Pendo lenu likadumu na Mungu akawatendee sawasawa na mapenzi yake
Nawapenda.

Daudi anafanywa mfalme wa Yuda

1Baada ya mambo haya, Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri, akasema, “Je, niende kwenye mji mmojawapo wa miji ya Yuda?” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nenda!” Daudi akamwuliza, “Niende mji upi?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nenda kwenye mji wa Hebroni.” 2Hivyo, Daudi alikwenda Hebroni, pamoja na wake zake wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali, kutoka mji wa Karmeli. 3Aliwachukua watu wake, kila mtu akiwa pamoja na jamaa yake; nao wakafanya makao yao katika miji iliyokuwa kandokando ya Hebroni.
4Watu wa Yuda walimwendea Daudi huko Hebroni wakampaka mafuta awe mfalme wao.
Daudi aliposikia kuwa watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Shauli, 5aliwatuma watu huko Yabesh-gileadi na ujumbe: “Mwenyezi-Mungu na awabariki kwa maana mlionesha utii wenu kwa Shauli, bwana wenu, kwa kumzika. 6Sasa, Mwenyezi-Mungu awafadhili na kuwa mwaminifu kwenu. Nami nitawatendea mema kutokana na jambo mlilolitenda. 7Lakini muwe imara na mashujaa. Shauli, bwana wenu, amekufa, na watu wa Yuda wamenipaka mafuta niwe mfalme wao.”

Ishboshethi anafanywa mfalme wa Israeli

8Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli alikuwa amemchukua Ishboshethi mwana wa Shauli na kumpeleka huko Mahanaimu. 9Huko, Abneri akamtawaza Ishboshethi kuwa mfalme wa nchi ya Gileadi, Ashuru,2:9 Ashuru; au Asheri. Yezreeli, Efraimu na Benyamini na Israeli yote.
10Ishboshethi alikuwa na umri wa miaka arubaini alipoanza kuitawala Israeli, naye alitawala kwa muda wa miaka miwili. Lakini kabila la Yuda lilimfuata Daudi. 11Daudi alikuwa mfalme wa kabila la Yuda kwa muda wa miaka saba na nusu, makao yake yalikuwa huko Hebroni.

Vita kati ya watu wa Israeli na watu wa Yuda

12Abneri mwana wa Neri, pamoja na maofisa wa Ishboshethi, mwana wa Shauli, waliondoka Mahanaimu na kwenda Gibeoni. 13Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wengine wa Daudi, nao walitoka na kukutana na Abneri na watu aliokuwa nao kwenye bwawa lililoko huko Gibeoni. Kikosi kimoja upande mmoja wa bwawa na kingine upande mwingine. 14Abneri akamwambia Yoabu, “Waruhusu vijana wapambane mbele yetu!” Yoabu akamjibu, “Sawa.” 15Ndipo vijana ishirini na wanne wakatolewa: Upande wa kabila la Benyamini na Ishboshethi mwana wa Shauli, vijana kumi na wawili; na upande wa Daudi vijana kumi na wawili.
16Kila mmoja alimkamata adui yake kichwani, akamchoma mpinzani wake upanga, hivyo wote wawili wakaanguka chini, wamekufa. Hivyo, mahali hapo pakaitwa Helkath-hazurimu.2:16 Helhath-hazurimu: Maana yake ni mashamba ya mapanga. Mahali hapo pako huko Gibeoni. 17Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Abneri na watu wa Israeli walipigwa vibaya na watu wa Daudi. 18Wana watatu wa Seruya: Yoabu, Abishai na Asaheli walikuwapo hapo. Asaheli alikuwa na mbio kama paa. 19Asaheli alimfuatia Abneri moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto. 20Abneri alipoangalia nyuma na kumwona Asaheli, alimwambia, “Je, ni wewe Asaheli?” Yeye akamjibu, “Naam, ni mimi.” 21Abneri akamwambia, “Geukia kulia au kushoto, umkamate kijana mmoja na kuchukua nyara zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfuatia. 22Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, “Acha kunifuatia. Kwa nini nikuue? Nitawezaje kuonana na kaka yako Yoabu?” 23Lakini Asaheli alikataa. Hivyo Abneri akampiga mkuki tumboni kinyumenyume,2:23 Hivyo … kinyumenyume: Makala ya Kiebrania si dhahiri. na mkuki huo ukatokeza mgongoni kwa Asaheli. Asaheli akaanguka chini, na kufa papo hapo. Watu wote waliofika mahali alipofia Asaheli, walisimama kimya. 24Lakini Yoabu na Abishai walimfuatia Abneri. Jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye mlima wa Ama, ulioko mashariki ya Gia, katika barabara iendayo jangwa la Gibeoni. 25Watu wa kabila la Benyamini wakajikusanya pamoja wakawa nyuma ya Abneri, hivyo wakaunda kikosi chao; nao wakasimama juu ya mlima. 26Kisha Abneri akamwita Yoabu, “Je, tutapigana siku zote? Je, huoni kwamba mwisho utakuwa mchungu? Je, utaendelea kwa muda gani bila kuwashawishi watu wako waache kuwaandama ndugu zao?” 27Yoabu akamwambia, “Naapa kwa Mungu aliye hai, kwamba kama hungesema jambo hilo, hakika watu wangu wangeendelea kuwaandama ndugu zao hadi kesho asubuhi.” 28Hivyo, Yoabu akapiga tarumbeta na watu wakaacha kuwafuatia watu wa Israeli, wala hawakupigana zaidi. 29Abneri na watu wake walipita bonde la Araba usiku kucha. Wakavuka mto Yordani, wakatembea mchana kutwa hadi Mahanaimu. 30Yoabu aliporudi kutoka kumfuatia Abneri, aliwakusanya watu wake wote, akagundua kuwa watumishi kumi na tisa wa Daudi walikosekana, licha ya Asaheli. 31Lakini watumishi wa Daudi walikuwa wamewaua watu 360 kutoka kabila la Benyamini pamoja na watu wa Abneri. 32Yoabu na watu wake waliuchukua mwili wa Asaheli, wakauzika kwenye kaburi la baba yake, lililoko huko Bethlehemu. Yoabu na watu wake walitembea usiku kucha, na kulipokucha wakafika mjini Hebroni.

2Samweli2;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 30 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Leo tunaanza kitabu cha -2Samueli1...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Leo tunaanza kitabu cha 2 Samweli Mungu akatubariki na akatupe macho ya rohoni tukapate kuelewa,kukumbuka  na kujifunza zaidi,ikawe faida kwetu na wengine..
Ee Mungu tunaomba ukatuongoze..

Siku moja, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongamana, wanasikiliza neno la Mungu. Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa. Wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao. Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua. Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, “Endesha mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki.” Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu.” Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika. Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama. Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, “Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!” Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile. Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.


Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...
Utukuzwe Mungu wetu,Mungu mwenye nguvu,Baba wa Upendo,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote,Alfa na omega,Mungu wa walio hai,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane,Mponyaji wetu,Hakuna lilikogumu kwako,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu,Hakuna kama wewe Mfalme wa Amani..!!

Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika!” Mara ule ukoma ukamwacha. Naye Yesu akamwamuru: “Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuoke na yule mwovu na kazi zake zote..
Mfalme wa amani tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Siku moja, Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na waalimu wa sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponya wagonjwa. Mara watu wakaja, wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani, wamweke mbele ya Yesu. Lakini, kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya paa, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu. Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.” Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!” Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.” Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu. Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.”


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Baba wa Mbinguni nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia..
Baba wa Mbinguni ukabariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Mungu wetu tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Yahweh ukaonekane katika maisha yetu na popote tupitapo Yahweh na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Nuru yako ikaangze katika maisha yetu,Amani ikatawale katika nyumba zetu,Upendo ukadumu kati yetu na tuka nene yaliyo yako Mungu wetu..
Tukawe barua njema Yahweh na tukasomeke kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!” Naye akaacha yote akamfuata. Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakawanungunikia wanafunzi wake wakisema: “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” Yesu akawajibu, “Wenye afya hawamhitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

Yahweh tunaomba ukawabariki na kuwatendea wenye shida/tabu
Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa na ukawape uvumilivu na imani wanaowauguza..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawafungue walio katika vifungo vya yule mwovu,Mungu wetu tazama walio magerezani pasipo na hatia Yahweh tunaomba ukawatendee na haki ikapatikane..
Jehovah tunaomba ukawape chakula wenye njaa Baba wa Mbinguni ukabariki Mashamba na kazi zao za mikono..
Mungu wetu tazama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Yahweh tunaomba ukawavushe salama,Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale wote walikwenda kinyume nawe na wakaomba na kutubu Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweke huru..
Jehovah tunaomba ukawafariji wafiwa,Yahweh ukawe tumaini kwa waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..

Watu wengine wakamwambia, “Wafuasi wa Yohane Mbatizaji hufunga mara kwa mara na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa.” Yesu akawajibu, “Je, wale walioalikwa harusini hutakiwa wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao? La! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.” Yesu akawaambia mfano huu: “Watu hawakati kiraka cha nguo mpya na kukitia katika vazi kuukuu; kama wakifanya hivyo, watakuwa wamelikata hilo vazi jipya, na pia hicho kiraka hakitachukuana na hilo vazi kuukuu. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; kwani hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya. Hakuna mtu anayetamani kunywa divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani kwani husema ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’”

Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Mielele..
Amina..!!!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami
Mungu wetu mwenye nguvu akawalinde na kuwabariki
Msipungukiwe katika mahitaji yenu Baba wa Mbinguni akawape kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.Daudi anahabarishwa juu ya kifo cha Shauli

1Baada ya kifo cha Shauli, Daudi alirudi baada ya kuwashinda Waamaleki, akakaa Siklagi kwa muda wa siku mbili. 2Siku iliyofuata, mtu mmoja kutoka kambi ya Shauli, mavazi yake yakiwa yamechanwa kwa huzuni na akiwa na mavumbi kichwani alimwendea Daudi. Alipomfikia Daudi, alijitupa chini mbele yake akamsujudia. 3Daudi akamwambia, “Unatoka wapi?” Naye akamwambia, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.” 4Daudi akamwambia, “Niambie mambo yalivyokuwa huko.” Yule mtu akamjibu, “Watu wetu wameyakimbia mapigano na wengi wetu wameuawa. Zaidi ya hayo, Shauli na mwanawe Yonathani pia wameuawa.” 5Daudi akamwuliza yule kijana, “Unajuaje kuwa Shauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”
6Yule kijana akamjibu, “Kwa bahati, nilikuwapo mlimani Gilboa. Nilimwona Shauli ameegemea mkuki wake na magari ya wapandafarasi ya adui zake yalikuwa yanamsonga sana. 7Shauli alipotazama nyuma, aliniona, akaniita. Nilipoitika, 8yeye aliniuliza mimi ni nani, nami nikamwambia kuwa mimi ni Mmaleki. 9Hapo, akaniambia, ‘Karibia uniue maana nimejeruhiwa vibaya na maumivu ni makali. Lakini bado ningali hai’. 10Hivyo, nilikwenda karibu naye na kumuua, kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa akianguka chini, hataweza kuishi zaidi. Lakini taji iliyokuwa kichwani pake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, vyote nimekuletea wewe, bwana wangu.”
11Daudi akayashika mavazi yake na kuyararua kwa huzuni. Hata watu waliokuwa pamoja na Daudi wakafanya vivyo hivyo. 12Wakaomboleza, wakalia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Shauli, Yonathani mwanawe, na nchi ya Waisraeli, watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wengi wao waliuawa vitani. 13Daudi akamwuliza yule kijana aliyempasha habari, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Mimi ni Mmaleki, lakini ninaishi katika nchi yako kama mgeni.” 14Daudi akamwuliza, “Ilikuwaje wewe hukuogopa kuunyosha mkono wako na kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta?” 15Kisha, Daudi akamwita mmoja wa vijana wake akamwambia, “Muue mtu huyu!” Yule kijana alimpiga yule Mmaleki, naye akafa. 16Daudi akasema, “Uwajibike wewe mwenyewe kwa kifo chako, maana umejishuhudia wewe mwenyewe kwa mdomo wako ukisema, ‘Nimemuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta.’”

Daudi aomboleza kifo cha Shauli na Yonathani

17Daudi aliimba ombolezo lifuatalo kwa ajili ya Shauli na mwanawe Yonathani. 18Daudi alisema watu wa Yuda wafundishwe ombolezo1:18 ombolezo: Kiebrania: Upinde. hilo, nalo limeandikwa katika kitabu cha Yashari.1:18 Yashari: Au Mnyofu. Daudi aliimba,
19“Walio fahari yako, ee Israeli,
wameuawa milimani pako.
Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!
20Jambo hilo msiuambie mji wa Gathi
wala katika mitaa ya Ashkeloni.
La sivyo, wanawake Wafilisti watashangilia,
binti za wasiotahiriwa, watafurahi.
21“Enyi milima ya Gilboa,
msiwe na umande au mvua juu yenu.
Wala mashamba yenu1:21 mashamba yenu: Kiebrania: Mashamba ya dhabihu. daima yasitoe chochote.
Maana huko ngao za shujaa zilitiwa najisi,
ngao ya Shauli haikupakwa mafuta.
22“Upinde wa Yonathani kamwe haukurudi nyuma,
upanga wa Shauli kamwe haukurudi bure,
daima ziliua wengi.
Naam, ziliua mashujaa.
23“Shauli na Yonathani,
watu wa ajabu na wakupendeza.
Maishani na kifoni hawakutengana.
Walikuwa wepesi kuliko tai,
naam, wenye nguvu kuliko simba.
24“Wanawake wa Israeli, mlilieni Shauli!
Aliwavika mavazi mekundu ya fahari,
aliyatarizi mavazi yenu kwa dhahabu.
25“Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!
Wamekufa wakiwa katika mapambano.
Yonathani analala,
akiwa ameuawa milimani.
26Nasikitika kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani.
Umekuwa kwangu daima mtu wa kupendeza,
pendo lako kwangu limekuwa la ajabu,
la ajabu kuliko la mwanamke.
27“Jinsi gani mashujaa wameanguka,
na silaha zao zimeachwa, hazina kazi.”


2Samweli1;1-27


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 29 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli31...Mwisho wa Kitabu cha 1 Samweli..Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

haleluyah Mungu wetu yu nmwema sana..
Tunamshukuru Mungu wetu kwa kutupa neema ya kumaliza kusoma/kupitia na kujifunza katika katika kitabu.
Leo tunamalizia na  1 Swamweli na kesho  tutaanza 2 Samweli
Ikimpendeza Mungu wetu...
Isiwe ndiyo mwisho wa kujifunza/kupitia/kurudia tena vitabu
vyote tulivyopitia huko nyuma,ni vyema kuwa tunarudia kusoma ili kujifunza na kuelewa zaidi,pia tusisite kuomba msaada kwa wengine pale tusipoelewa..
Mungu akatuongoze na kutupa shauku/kiu ya kutaka kujifunza zaidi na kuelewa na kutenda yote sawasawa na mapenzi yake...
Kuna swala "MUDA/NAFASI" ya kusoma ili nitaliongelea wakati mwingine lakini ukiamua kitu na ukamuomba Mungu hutokosa muda wa kusoma NENO..


Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wote wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi, zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, zikateketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikamea, zikakua na kuzaa: Moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia.” Kisha akawaambia, “Mwenye masikio na asikie!”

Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu,si kwamba sisi ni wema sana si kwamba sisi ni wazuri mno si kwa akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii ni kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu..

Asante Baba wa Mbinguni  kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante Mungu wetu kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu.
utukuzwe Mungu wetu,unastahili sifa Baba wa Mbinguni,unastahili kuabudiwa Yahweh,unastahili kuhimidiwa Jehovah,unastahili kutukuzwa
Mungu Baba....
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu mno..
Neema yako yatutosha Mungu wetu..!


Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. Naye akawaambia, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri ya ufalme wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, ili, ‘Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe.’”
Yahweh tunakuja mbele zako tukinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe  katika majaribu Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Basi, Yesu akawauliza, “Je, nyinyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? Mpanzi hupanda neno la Mungu. Watu wengine ni kama walio njiani ambapo neno lilipandwa. Lakini mara tu baada ya kulisikia, Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu walisikiapo hilo neno hulipokea kwa furaha. Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno, mara wanakata tamaa. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaosikia hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia.”

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Jehovha tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako...
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..Yesu akaendelea kuwaambia, “Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. Mwenye masikio na asikie!” Akawaambia pia, “Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.”

Mafalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh ukatuongoze tutokapo/tuingiapo Baba wa Mbinguni tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Mungu Baba tukawe salama moyoni Yahweh ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia Neno lako na kulitii..


Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.”
Jehovah tukanene yaliyo yako,Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo Yahweh na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh neema yako na fadhili zako ziwe nasi Baba wa Mbinguni Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu..
Jehovah ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.” Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.

Yahwe tunaomba ukawabariki na kuwaponya wagonjwa Mungu wetu ukawape uvumilivu na imani wanaowauguza..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape chakula wenye njaa Yahweh ukabariki mashamba/vyanzo vyao.
Mungu wetu tunaomba kuwavushe salama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Jehovah tunaomba ukawe tumaini kwa wote waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka..
Mungu wetu tunaomba ukawafariji wafiwa ukawape moyo uvumilivu na nguvu..
Yahweh ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu Mungu wetu ukawafungue walio katika vifungo vya yule mwovu Baba wa Mbinguni tazama walio magerezani pasipo na hatia Mungu wetu tunaomba ukawatendee na haki ikapatikane..
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Mungu Baba ukawasamehe wale walio kwenda kinyume nawe Mungu wetu walionguka/potea Baba wa Mbinguni ukasikie kuomba kwao Yahweh ukawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..


Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke ziwa, twende ngambo.” Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Vilevile mashua nyingine zilimfuata. Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji. Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, “Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?” Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, “Kimya! Tulia!” Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?” Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, “Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?”

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utufu hata Milele..
Amina..!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba akadumishe pendo lenu Yahweh akawatendee sawasawa na mapenzi yake..
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikawe nanyi Daima..
Nawapenda. 
Kifo cha Shauli na wanawe

(Kumb 10:1-12)

1Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti, na kuuawa katika mlima wa Gilboa. 2Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua, wana wa Shauli. 3Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi vibaya. 4Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanichoma upanga na kunidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe, na kuuangukia. 5Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia aliuangukia upanga wake, akafa pamoja na Shauli. 6Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, na wanawe watatu, pia na mtu aliyembebea silaha pamoja na watu wake wote katika siku hiyohiyo moja. 7Nao Waisraeli waliokuwa upande wa pili wa bonde, na wengine waliokuwa upande wa mashariki wa mto Yordani walipoona kuwa Waisraeli wamekimbia, naye Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao, wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo.
8Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa walizikuta maiti za Shauli na wanawe mlimani Gilboa. 9Walikata kichwa cha Shauli na kumvua silaha zake; halafu waliwatuma wajumbe katika nchi yao yote ya Filistia kutangaza habari njema nyumbani mwa sanamu zao na kwa watu. 10Zile silaha zake waliziweka nyumbani mwa Maashtarothi; kisha wakautundika mwili wake kwenye ukuta wa mji wa Beth-sheani.
11Lakini wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi waliposikia Wafilisti walivyomtendea Shauli, 12mashujaa wote waliondoka, wakasafiri usiku kucha, wakaondoa mwili wa Shauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-sheani; wakaja nayo mpaka Yabeshi na kuiteketeza huko. 13Baadaye, wakaichukua mifupa yao na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi; nao wakafunga kwa muda wa siku saba.1Samweli31;1-13

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.