Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 9 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli17...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muweza wa yote Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,
Mungu wa Yatima na Wajane,Alfa na Omega,Yahweh,Jehovah,Adonai,Elohim,El Elyon,El Olam,El Qanna,El Shaddai,Emanueli- Mungu Pamoja nasi..!!

Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh..
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu..
Neema yako yatutosha ee Mungu wetu..!!
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..!!


Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Toa unabii dhidi ya wachungaji wa Israeli. Waambie hao wachungaji kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ole wenu nyinyi wachungaji wa Israeli, mnaojilisha nyinyi wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnakunywa maziwa, mnavaa mavazi ya manyoya yao na kondoo wanono mnawachinja na kuwala. Lakini hamwalishi hao kondoo. Walio dhaifu hamkuwapatia nguvu, wagonjwa hamkuwaponya, waliojeruhiwa hamkuwafungia dawa, waliotangatanga hamkuwarudisha na waliopotea hamkuwatafuta. Lakini mmetumia mabavu na ukatili kuwatawala. Basi, kwa kuwa hao kondoo hawakuwa na mchungaji walitawanywa, wakawa mawindo ya wanyama wakali. Naam, kondoo wangu walitawanywa, wakatangatanga milimani na vilimani. Kondoo walisambazwa duniani kote, na hapakuwa na mtu aliyejali juu yao wala kuwatafuta.

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
wakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu 
kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


“Basi, sikieni vizuri neno langu mimi Mwenyezi-Mungu, enyi wachungaji: Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, naapa kwamba: Nimechoka kuwaona kondoo wangu wamekuwa mawindo ya wanyama wakali kwa vile hapakuwa na mchungaji; wachungaji wangu hawakuwatafuta kondoo wangu, bali wamejilisha wao wenyewe badala ya kuwalisha kondoo wangu. Basi, nyinyi wachungaji, sikieni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana nanyi, enyi wachungaji. Nitawaondolea madaraka ya kuchunga kondoo wangu, wala sitakubali muwachunge tena. Hamtakuwa tena na nafasi ya kujinufaisha wenyewe. Nitawaokoa kondoo wangu makuchani mwenu, ili wasiwe chakula chenu tena.


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Jehovah tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwavyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mfalme wa amani ukatawale na amani yako ikatawale katika maisha yetu..
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh tukawe salama moyoni,ukatupe macho ya rohoni masikio ya kusikia sauti yako na kuitii,Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,amani na upendo visipungue,Jehovah ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



“Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe nitawatafuta kondoo wangu na kuwatunza. Kama mchungaji anavyowatafuta kondoo wake waliotawanyika, ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawarudisha kutoka kila mahali walipotawanyika siku yenye mawingu na giza nene. Nitawatoa kutoka kwa watu wa mataifa. Nitawakusanya kutoka nchi za mbali na kuwaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawachunga juu ya milima ya Israeli, kando ya vijito na katika sehemu zote za nchi zinazokaliwa na watu. Nitawapa malisho mazuri kwenye milima mirefu ya Israeli ambako yako malisho yao. Watapumzika huko kwenye mbuga za malisho mazuri; naam, watapata malisho mazuri juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitakuwa mchungaji wa kondoo wangu. Mimi mwenyewe nitawapumzisha. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Kondoo waliopotea nitawatafuta na waliotangatanga nitawarudisha nyumbani. Waliojeruhiwa nitawatibu, na wale walio dhaifu nitawapa nguvu. Kondoo wanono na wenye nguvu nitawaangamiza. Mimi nitawachunga kondoo kama itakiwavyo. “Na Nyinyi mlio kundi langu, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitaamua baina ya kondoo na kondoo; baina ya kondoo dume na mbuzi. Baadhi yenu mnakula malisho mazuri na pia kukanyagakanyaga yale yaliyobaki! Mnakunywa maji safi na yanayobaki mnayachafua kwa miguu yenu! Je, kondoo wangu wengine wale malisho yaliyokanyagwakanyagwa na kunywa maji yaliyochafuliwa? “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambia hivi: Mimi mwenyewe nitaamua kati ya kondoo wanono na kondoo dhaifu. Nyinyi mnawasukuma kwa mbavu na kwa mabega na kuwapiga pembe kondoo wote walio dhaifu mpaka mmewatawanya mbali na kundi. Lakini mimi nitawaokoa kondoo wangu wasiwe tena mawindo. Nitatoa hukumu juu ya kila kondoo. Nitamweka mchungaji mmoja juu yao, mfalme kama mtumishi wangu Daudi. Yeye atawalisha na kuwa mchungaji wao. Nami Mwenyezi-Mungu, nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitafanya nao agano la amani. Nitaondoa wanyama wakali katika nchi, ili kondoo wangu wakae mbugani kwa usalama na kulala msituni.

Mungu wetu tunarudisha sifa na shukrani kwa uponyaji wa wagonjwa wetu,Yahweh umekuwa msaada kwa wenye shida/tabu,Mungu wetu tumeona maajabu yako,Jehovah tunashuhudia utukufu wako kwa uliowagusa kwa mkono wako wenye nguvu..

“Nitawafanya waishi kandokando ya mlima wangu mtakatifu na kuwabariki. Nitawaletea mvua kwa wakati wake, nazo zitakuwa mvua za baraka. Miti mashambani itazaa matunda, ardhi itatoa mazao kwa wingi, nao wataishi salama katika nchi yao. Nitakapovunja nira zao za utumwa na kuwaokoa mikononi mwa hao waliowafanya kuwa watumwa ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Hawatakuwa tena mawindo ya mataifa mengine wala wanyama wa porini hawatawaua na kuwala. Wataishi kwa usalama na hakuna atakayewatisha. Nitawapa mashamba yenye rutuba ili wasiangamizwe tena na njaa nchini humo, wala kudharauliwa tena na mataifa mengine. Nao watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, niko pamoja nao na kwamba watu hao wa Israeli ni watu wangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nyinyi, kundi la kondoo wangu, ni nyinyi watu wangu, nami ni Mungu wenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Mungu Baba ukawaguse na wengine wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Yahweh ukawatendee na wengine walio katika vifungo vya yule mwovu,Mungu wetu ukaendelee kuwaponya wagonjwa wengine yahweh ukawape uvumilivu na nguvu wanaowaguza..
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea na kuombea wengine
Yahweh ukasikie kulia kwao Mungu wetu tunaomba ukawafute machozi ya watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani..
Jehovah ukawasamehe wale wote walikwenda kinyume nawe..
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami..
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba ukawe nanyi Diama..
Nawapenda.

Goliathi anapambana na Waisraeli

1Sasa, Wafilisti walikusanya majeshi yao huko Soko, mji ulioko katika Yuda, tayari kwa vita. Walipiga kambi katika sehemu moja iitwayo Efes-damimu kati ya Soko na Azeka. 2Shauli pamoja na Waisraeli walikusanyika, na kupiga kambi katika bonde la Ela. Wakajipanga tayari kupigana na Wafilisti. 3Wafilisti walisimama mlimani upande mmoja na Waisraeli walisimama mlimani upande mwingine, katikati yao kulikuwa na bonde. 4Kutoka kwenye kambi ya Wafilisti, alijitokeza shujaa mmoja aitwaye Goliathi, mwenyeji wa mji wa Gathi. Urefu wake ulikaribia mita tatu. 5Kichwani alivaa kofia ya shaba, na deraya ya shaba kifuani yenye uzito wa kilo 57. 6Miguu yake pia ilikuwa na kinga ya shaba na mabegani pake alibeba mkuki wa shaba. 7Mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo, na chembe cha mkuki huo, kilikuwa na uzito wa kilo saba. Ngao yake ilibebwa na mtu mwingine aliyemtangulia. 8Goliathi alisimama na kuwapigia kelele wanajeshi wa Israeli, akisema, “Mnafanya nini hapo? Je, mmekuja kupigana vita? Mimi ni Mfilisti, nyinyi ni watumwa wa Shauli. Chagueni mtu mmoja wenu aje kupigana nami. 9Akinishinda na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu. Lakini nikimshinda na kumuua basi, nyinyi mtakuwa watumwa wetu na kututumikia.” 10Kisha Mfilisti huyo aliendelea kusema kwa majivuno, “Nawataka wanajeshi wa Israeli siku hii kumtoa mtu mmoja aje kupigana nami.” 11Shauli pamoja na wanajeshi wote wa Israeli walipoyasikia maneno hayo ya Mfilisti huyo, walifadhaika na kuogopa sana.

Daudi kwenye kambi ya Shauli

12Daudi alikuwa mtoto wa Yese, Mwefrathi kutoka Bethlehemu katika Yuda. Yese alikuwa na watoto wanane wa kiume. Wakati Shauli alipokuwa mfalme, yeye alikuwa tayari mzee, mtu mwenye umri mkubwa.17:12 mtu mwenye umri mkubwa: Makala ya Kiebrania si dhahiri. 13Wana wakubwa watatu wa Yese, Eliabu mzaliwa wa kwanza, Abinadabu aliyefuata na Shama wa tatu, walikuwa wamekwenda pamoja na Shauli vitani. 14Daudi alikuwa ndiye mdogo wa wote. Wale watoto watatu wakubwa walikuwa wamekwenda na Shauli. 15Ingawa Daudi mara kwa mara alikwenda kwa Shauli, alirudi nyumbani Bethlehemu kuchunga kondoo wa baba yake.
16Kwa muda wa siku arubaini, asubuhi na jioni, yule Mfilisti Goliathi alijitokeza hadharani, akasimama na kuwakejeli wanajeshi wa Israeli.
17Siku moja, Yese alimwambia mwanawe Daudi, “Wapelekee kaka zako bisi kilo kumi na mikate kumi. Wapelekee haraka huko kambini. 18Na yule kamanda wao wa kikosi cha wanajeshi elfu mpelekee jibini hizi kumi. Kawaangalie kaka zako kama wanaendelea vizuri na kisha uniletee habari zao.” 19Wakati huo mfalme Shauli, kaka zake Daudi na wanajeshi wote wa Israeli walikuwa kwenye bonde la Ela, wanapigana na Wafilisti.
20Kesho yake, Daudi aliamka asubuhi na mapema, na kondoo akamwachia mchungaji. Alichukua chakula na kwenda kama alivyoagizwa na baba yake Yese. Alipofika kwenye kambi ya Waisraeli, aliwakuta wanajipanga kwenye sehemu yao ya vita na wanapiga kelele za vita. 21Majeshi ya Waisraeli na ya Wafilisti walijipanga tayari kupigana vita, majeshi yakiwa yanakabiliana ana kwa ana. 22Daudi alimkabidhi chakula mtu aliyetunza mizigo, akawakimbilia wanajeshi, akaenda kwa kaka zake na kuwasalimia. 23Alipokuwa anaongea nao, Goliathi yule shujaa wa Wafilisti kutoka Gathi alijitokeza mbele ya wanajeshi wa Israeli kama alivyozoea. Naye Daudi alimsikiliza vizuri sana. 24Waisraeli walipomwona Goliathi, walimkimbia, na kumwogopa sana. 25Waliambiana, “Je, mmemwona yule mtu aliyejitokeza? Ama kweli, amejitokeza kuwakejeli Waisraeli. Mfalme Shauli atampa mtu yeyote atakayemuua mtu huyo utajiri mwingi. Zaidi ya yote, atamwoza binti yake. Tena, watu wa jamaa ya baba yake watakuwa huru, hawatalipa kodi.”
26Daudi akawauliza wale waliokuwa karibu naye, “Je, mtu atakayemuua Mfilisti huyu na kuikomboa Israeli kutokana na aibu hii atafanyiwa nini? Ni nani huyu Mfilisti, mtu asiyetahiriwa, anayethubutu kuyatukana majeshi ya Mungu aliye hai?” 27Watu wakamwambia kama walivyokuwa wamesema hapo awali juu ya mtu atakayemuua Goliathi.
28Lakini Eliabu, kaka mkubwa wa Daudi alipomsikia Daudi akiongea na watu, alimkasirikia Daudi, akasema, “Kwa nini umekuja? Je, wale kondoo wachache umemwachia nani kule nyikani? Najua ujeuri wako na uovu wako. Umekuja tu kutazama vita.”
29Daudi akamjibu, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi kuuliza swali tu?” 30Daudi akamgeukia mtu mwingine akamwuliza swali hilohilo; na kila alipouliza, alipata jibu lilelile.
31Watu fulani ambao walimsikia Daudi alivyosema, walikwenda kumwambia Shauli. Naye Shauli akaagiza aitwe. 32Daudi akamwambia Shauli, “Mtu yeyote asitishike moyoni mwake kutokana na Mfilisti huyu. Mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana naye.” 33Shauli akamwambia Daudi, “Wewe huwezi kwenda kupigana na Mfilisti yule. Wewe ni kijana tu, lakini mtu huyo amekuwa vitani tangu ujana wake.” 34Daudi akasema, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo 35mimi humfuata na kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua. 36Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao. 37Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu.” Shauli akamwambia, “Nenda; naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nawe.” 38Shauli akamvisha Daudi mavazi yake ya kivita, akamvika kofia yake ya shaba kichwani na koti lake la kujikinga kifua. 39Daudi akajifunga upanga wa Shauli, akajaribu kutembea; lakini akashindwa kwa kuwa hakuyazoea mavazi kama hayo. Akamwambia Shauli, “Siwezi kwenda vitani nikiwa nimevaa mavazi haya, kwani mimi sijayazoea.” Kwa hiyo, akayavua. 40Daudi akachukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe matano mazuri kutoka kwenye kijito, akayatia katika mfuko wake wa mchungaji. Kombeo lake likiwa tayari mkononi mwake, akaanza kumwendea Goliathi Mfilisti.

Daudi anamshinda Goliathi

41Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake. 42Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza. 43Goliathi akamwuliza Daudi, “Sasa, hiyo fimbo ni ya nini? Unadhani mimi ni mbwa hata unijie kwa fimbo?” Mfilisti huyo akamlaani Daudi kwa miungu yake. 44Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu! Mwili wako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini!”
45Lakini Daudi akamwambia Goliathi, “Wewe unanijia kwa upanga, mkuki na sime. Lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa askari wa Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46Siku ya leo, Mwenyezi-Mungu atakutia mikononi mwangu. Nitakubwaga chini, nitakukata kichwa chako; na miili ya wanajeshi wa Wafilisti nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini. Ndipo dunia nzima itakapojua kuwa Mungu yuko katika Israeli. 47Watu wote waliokusanyika hapa leo, watajua kuwa Mwenyezi-Mungu hahitaji mikuki wala sime kuwaokoa watu. Hii ni vita ya Mwenyezi-Mungu, naye atawatia nyinyi nyote mikononi mwetu.”
48Goliathi akaanza tena kumwendea Daudi. Daudi akakimbia mbio kwenda kwenye mstari wa mapambano. 49Akatia mkono wake mfukoni mwake, akatoa jiwe moja, akalirusha kwa kombeo lake, akampiga nalo Goliathi kwenye paji la uso wake, jiwe likalipasua paji la Goliathi na kupenya ndani. Goliathi akaanguka chini kifudifudi. 50Ndivyo Daudi alivyomshinda Goliathi kwa kombeo lake na jiwe. Alimpiga yule Mfilisti na kumuua. Daudi hakuwa na upanga wowote mkononi mwake. 51Basi, akaenda mbio, akasimama juu ya Goliathi, akaufuta upanga wa Goliathi alani mwake, akamuua Goliathi kwa kumkata kichwa chake.
Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao ameuawa, wakatimua mbio. 52Ndipo watu wa Israeli na watu wa Yuda, walipoanza kupiga kelele za ushindi, wakawafuatilia Wafilisti hadi Gathi,17:52 Gathi: Makala ya Kiebrania “bonde”. kwenye malango ya Ekroni, hata Wafilisti waliojeruhiwa vitani walienea njiani tangu Shaarimu hadi Gathi na Ekroni. 53Waisraeli walipotoka kuwafuatilia Wafilisti, waliteka nyara kambi yao. 54Daudi alikichukua kichwa cha yule Goliathi, Mfilisti, akakipeleka mjini Yerusalemu. Lakini silaha za Goliathi akaziweka katika hema lake.

Daudi anapelekwa kwa Shauli

55Shauli alipomwona Daudi akienda kumkabili yule Mfilisti Goliathi, alimwuliza Abneri, kamanda wa jeshi lake, “Abneri, huyu ni kijana wa nani?” Abneri alijibu, “Mfalme, kama uishivyo, mimi sijui.” 56Mfalme Shauli akamwambia, “Basi, uliza yeye ni kijana wa nani.”
57Mara tu Daudi aliporudi kambini baada ya kumuua Goliathi, Abneri alimchukua na kumpeleka kwa Shauli. Wakati huo Daudi alikuwa bado amechukua kichwa cha Goliathi mikononi mwake. 58Shauli akamwuliza Daudi, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?” Daudi akajibu, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese, kutoka mji wa Bethlehemu.”


1Samweli17;1-58
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: