Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 8 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli16...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yumwema sana..
Tumshukuru Mungu katika yote..

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kendelea kuiona leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..

Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh,
Uabudiwe Jehovah,Unatosha Mungu wetu,Mataendo yako ni makuu sana,
Matendo yako ni ya ajabu,hakuna kama wewe Mungu wetu,Hakuna wa kufanana nawe Baba wa Mbinguni,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Mungu wetu..!!

Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. Basi, akawaambia watumishi wake, “Mtu huyu ni Yohane Mbatizaji, amefufuka kutoka kwa wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Kisa ni kwamba Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!” Herode alitaka kumuua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii. Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, “Nipe papa hapa katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.
Tazama Jana imepita Mungu wetu Leo  ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine Jehovah..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya 
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu Baba  nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Jehovaha tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini. Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao. Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na saa za mchana zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula.” Yesu akawaambia, “Si lazima waende, wapeni nyinyi chakula.” Lakini wao wakamwambia, “Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili.” Yesu akawaambia, “Nileteeni hapa.” Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu. Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa  katika ufanyaji/utendaji Baba wa Mbinguni tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Jehovah nasi
tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu
Yahweh tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote
wanaotuzunguka,Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki..
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Yahweh ukatuongoze tuingiapo/tutokapo Mungu Baba ukatupe neema ya kufuata njia zako 
Jehovah tukasimamie neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Baba wa Mbinguni tukawe salama moyoni Yahweh ukatupe macho ya kuona Jehovah ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo Yahweh na ijulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh tukawe barua njema na tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ngambo ya ziwa wakati yeye anayaaga makundi ya watu. Baada ya kuwaaga watu, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake, na wakati huo ile mashua ilikwisha fika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikumbwa na taabu kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga. Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji. Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliogopa sana, wakasema, “Ni mzimu!” Wakapiga yowe kwa hofu. Mara, Yesu akasema nao, “Tulieni, ni mimi. Msiogope!” Petro akamwambia, “Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako.” Yesu akasema, “Haya, njoo.” Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu. Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, “Bwana, niokoe!” Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, “Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?” Kisha wakapanda mashuani, na upepo ukatulia. Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.”

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
na ukawape uponyaji wagonjw, Mungu wetu ukawatendee muujiza wako
Yahweh ukawainue, Baba wa Mbinguni ukawaongoze  waganga,manesi na wahudumu wote,Mungu wetu ukaonekane Yahweh ukawape nguvu wanaowaguza,Jehovah ukawavushe salama wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu ukawaokoe na kuwaongoza
Yahweh tazama walio magerezani pasipo na hatia Mungu wetu haki ikatendeke,Yahweh walio katika vifungo vya yule mwovu Mungu wetu ukawaweke huru,Jehovah ukawaguse wote wenye shida/tabu waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka Mungu wetu ukawe tumaini lao,Yahweh ukawafariji wafiwa,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,Yahweh wakafuate njia zako Mungu wetu Nuru yako ikaangaze
katika maisha yao,Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukawasimamishe na kuwaongoza
Yahweh ukasikie kulia kwao Mungu wetu ukawafute machozi ya watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani,Mungu wetu ukasikie,ukapokee na ukatujibu sala/maombi yetu..
Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..

Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti. Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote, wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake. Nao wote waliomgusa walipona.
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa nami
Mungu wetu mwenye nguvu,Baba wa Upendo na  amani
akawaongoze katika yote..
Amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi Daima..
Nawapenda.





Daudi anapakwa mafuta kuwa mfalme

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Utamlilia Shauli mpaka lini? Wewe unajua kuwa mimi nimemkataa kuwa mfalme juu ya Israeli. Sasa, jaza upembe wako mafuta, uondoke. Nitakutuma kwa Yese wa mji wa Bethlehemu. Maana nimejipatia mfalme miongoni mwa wanawe.” 2Samueli akasema, “Nitawezaje kwenda? Kama Shauli akisikia habari hizo, ataniua!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Chukua ndama pamoja nawe, na ukifika huko useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko’. 3Mwalike Yese kwenye tambiko hiyo nami nitakuonesha la kufanya. Utampaka mafuta kwa ajili yangu mtu yule nitakayekutajia.”
4Samueli akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi-Mungu, akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji wakatoka kumlaki wakiwa wanatetemeka, wakamwuliza, “Je, umekuja kwa amani?”
5Samueli akawaambia, “Nimekuja kwa amani. Nimekuja kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Jitakaseni wenyewe halafu twendeni kutoa tambiko.” Samueli akamtakasa Yese pamoja na wanawe, akawakaribisha kwenye tambiko.
6Walipofika, na Samueli alipomwona Eliabu, alijisemea moyoni mwake, “Hakika, mpakwa mafuta wa Mwenyezi-Mungu ndiye huyu aliye mbele ya Mwenyezi-Mungu!” 7Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoyaangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni.” 8Kisha, Yese akamwita Abinadabu na kumleta mbele ya Samueli. Lakini Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.” 9Yese akamleta Shama. Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.” 10Yese aliwapitisha wanawe wote saba mbele ya Samueli lakini Samueli akamwambia, “Mwenyezi-Mungu hajamchagua yeyote kati ya hawa.” 11Halafu akamwambia, “Je, wanao wote wako hapa?”
Yese akajibu, “Bado yuko mdogo, lakini amekwenda kuchunga kondoo.” Samueli akamwambia, “Mtume mtu amlete; sisi hatutaketi chini, mpaka atakapokuja hapa.” 12Hivyo, Yese alituma mtu, naye akaletwa. Yule kijana alikuwa mwenye afya, mwenye macho maangavu na wa kupendeza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Sasa, huyu ndiye; inuka umpake mafuta.” 13Samueli akachukua upembe wake wenye mafuta akammiminia Daudi mafuta mbele ya kaka zake. Mara roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Daudi kwa nguvu, ikakaa tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samueli akarudi mjini Rama.

Daudi kwenye ukumbi wa Shauli

14Baadaye roho ya Mwenyezi-Mungu ilimwacha Shauli, na roho mwovu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ikamsumbua. 15Ndipo watumishi wake Shauli wakamwambia, “Tunajua kwamba roho mwovu kutoka kwa Mungu anakusumbua. 16Sasa, ee bwana wetu, amuru watumishi wako wanaokutumikia wamtafute mtu mwenye ufundi wa kupiga kinubi, na huyo roho mwovu kutoka kwa Mungu atakapokujia, mtu huyo atapiga kinubi, nawe utapata nafuu.”
17Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mtu huyo anayeweza kupiga kinubi vizuri, mniletee.” 18Kijana mmoja miongoni mwa watumishi akasema, “Nimemwona kijana mmoja wa Yese, wa mji wa Bethlehemu. Kijana huyo ana ujuzi wa kupiga kinubi. Huyo kijana ni shujaa, hodari wa kupigana vitani, ana busara katika kusema na mwenye umbo zuri; Mwenyezi-Mungu yuko pamoja naye.”
19Hivyo, Shauli alituma ujumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” 20Yese alimtuma Daudi kwa Shauli pamoja na punda aliyebeba mikate, kiriba cha divai na mwanambuzi. 21Daudi alipofika akaingia kumtumikia Shauli. Shauli alimpenda sana, hata akamfanya awe mwenye kumbebea silaha zake. 22Halafu Shauli alituma ujumbe kwa Yese na kusema, “Nampenda Daudi; mwache akae hapa anitumikie.” 23Kila mara, yule roho mwovu kutoka kwa Mungu alipomjia Shauli, Daudi alichukua kinubi chake na kuanza kukipiga, na roho huyo alimwacha Shauli, naye akaburudika na kupata nafuu.


1Samweli16;1-23
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


No comments: