Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 26 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli30...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Muweza wa yote,Mungu mwenye nguvu,Baba wa upendo,Baba wa baraka
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa wote walio hai..

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe ee Mungu wetu,hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni
Matendo yako ni makuu mno,Mtendo yako ni ya ajabu Jehovah
Neema yako yatutosha Yahweh...!!


Basi, nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni. Maana nikiwahuzunisha nyinyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha! Ndiyo maana niliwaandikia: Sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na nyinyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba mimi nikifurahi, nyinyi nyote pia mnafurahi. Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwaonesheni kwamba nawapenda mno.


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozitenda
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi, ila amewahuzunisha nyinyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi. Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha. Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa. Kwa hiyo nawasihi: Mwonesheni kwamba mnampenda. Madhumuni yangu ya kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo. Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe, kama kweli ninacho cha kusamehe, nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu, ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.


Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu Baba tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji  Yahweh tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatami,Jehovah ukatuongoze tuingiapo/tutokapo,Mungu wetu ukavitakase vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Yahweh ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo....
Yahweh tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu Jehovah tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Jehovah tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu....
Yahweh ukaonekane popote tupitapo Mungu wetu na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Jehovah ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana. Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia. Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote, wanaookolewa na wanaopotea. Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo? Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.
Baba wa Mbinguni tunarudisha sifa na utukufu kwako
Asante kwa kuwa nasi na kujibu maombi ya watoto wako
Yahweh umekuwa nasi tukuitapo,Baba wa Mbinguni ukuTUacha tuaibike
Mungu wetu mkono wako tumeuona Yahweh unastahili sifa Baba wa Mbinguni asante kwa matendo yako makuu,asante kwa uponyaji wako
asante kwa uwepo wako,asante kwa kutusikia na kututendea sawasawa na mapenzi yako..
Tukurudishie nini Mungu wetu kwa wema wako hakuna zaidi ya kukuabudu,kukusifu na kukutukuza siku zote za maisha yetu..!!



Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe. Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na kuishiriki hali yake ya kimungu. Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza imani yenu kwa fadhila, fadhila yenu kwa elimu, elimu yenu kwa kuwa na kiasi, kuwa na kiasi kwa uvumilivu, uvumilivu wenu kwa uchaji wa Mungu, uchaji wenu kwa urafiki wa kindugu, na urafiki wenu wa kindugu kwa mapendo. Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani. Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe. Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu na mko imara katika ukweli mlioupokea. Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya. Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi. Basi, nitajitahidi kusudi baada ya kufariki kwangu mweze kuyakumbuka mambo haya kila wakati.


Yahweh tunaomba ukawaguse na wengine wanaopitia shida/tabu..
Mungu wetu ukawaponye na walio wagonjwa Yahweh ukasike kulia kwao
Mungu wetu ukawavushe salama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu ukawaokoe wale walio katika vifungo vya yule mwovu
Mungu Baba ukawape chakula wenye njaa,Yahweh ukawanyanyue walio anguka Mungu wetu ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukaonekane kwa watoto wako wanaokuOmba kwa bidii na imani,Jehovah ukawape neema ya kujiombea,Yahweh ukasikie,Baba wa Mbinguni ukawajibu,Mungu wetu ukapokee sala/maombi yetu Jehovah ukawatendee sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami
Mungu akawabariki na amani ya Kristo iwe nayi Daima
Nawapenda.


Vita dhidi ya Waamaleki

1Siku ya tatu baadaye, Daudi na watu wake wakarudi Siklagi. Waamaleki walikuwa wamekwisha shambulia Negebu pamoja na mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto. 2Walikuwa wameteka wanawake na watu wote waliokuwa mjini humo, wakubwa kwa wadogo. Hao waliowateka, waliondoka nao wakiwa hai, bila ya kumwua mtu yeyote.
3Daudi na watu wake walipofika mjini waliukuta mji umeteketezwa, na wanawake, watoto wao wa kiume na wa kike, wamechukuliwa mateka. 4Ndipo Daudi na watu wake walipoangua kilio, wakalia hadi walipoishiwa nguvu. 5Wake wawili wa Daudi, Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali, nao pia walikuwa wamechukuliwa mateka.
6Sasa, Daudi alikuwa katika matatizo makubwa kwa kuwa watu wake walikuwa na uchungu rohoni mwao kwa kupoteza watoto wao; hivyo wakawa wanamtishia kumpiga mawe. Lakini Daudi alijipa moyo kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. 7Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibao cha kuhani.” Abiathari akampelekea. 8Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, genge hili nilifuate? Na je nitalikamata?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Lifuate kwani utalipata na kuwaokoa hao waliotekwa.”
9Kwa hiyo, Daudi akaondoka pamoja na wale watu 600 aliokuwa nao. Walipofika kwenye kijito cha Besori, wakawakuta baadhi ya watu waliotekwa wameachwa hapo. 10Lakini Daudi aliendelea kulifuatilia lile genge akiwa na watu 400, watu 200 wakabaki hapo kwani walichoka mno, wasiweze kuvuka kijito hicho. 11Wale watu waliokuwa na Daudi walimkuta mtu mmoja Mmisri nyikani, nao wakampeleka kwa Daudi. Wakampa mtu huyo mkate na maji. 12Pia walimpa kipande cha mkate wa tini na vishada viwili vya zabibu kavu. Alipomaliza kula, akapata nguvu, kwani alikuwa hajala wala kunywa kitu chochote kwa muda wa siku tatu, mchana na usiku. 13Daudi akamwuliza, “Bwana wako ni nani? Na umetoka wapi?” Yeye akamwambia, “Mimi ni kijana Mmisri. Ni mtumishi wa Mmaleki mmoja. Bwana wangu aliniacha nyuma siku tatu zilizopita kwa kuwa nilikuwa mgonjwa. 14Sisi tulishambulia sehemu ya jangwa wanamoishi Wakerethi, eneo la Yuda pamoja na sehemu ya jangwa unakoishi ukoo wa Kalebu, tukauteketeza kwa moto mji wa Siklagi.”
15Daudi akamwuliza, “Je, utaweza kunipeleka kwenye genge hilo?” Kijana akamjibu, “Ikiwa utaniapia kwa jina la Mungu kuwa hutaniua, wala kunitia mikononi mwa bwana wangu, nitakupeleka.” 16Yule kijana alimwongoza Daudi hadi genge lile lilipokuwa. Walipofika huko waliwakuta wateka nyara hao wakiwa wametawanyika kila mahali kwani walikuwa wakila na kunywa kwa sababu nyara walizoteka kutoka nchi ya Wafilisti na nchi ya Yuda zilikuwa nyingi sana. 17Daudi aliwapiga tangu asubuhi hadi siku ya pili jioni. Hakuna mwanamume yeyote aliyenusurika isipokuwa vijana 400 ambao walipanda ngamia na kukimbia. 18Daudi aliokoa kila kitu Waamaleki walichokuwa wamekiteka, hata na wake zake wawili. 19Chochote kilichokuwa chao, kiwe kikubwa au kidogo, mtoto wa kiume au wa kike, Daudi alikikomboa. 20Pia Daudi aliyarudisha makundi yote ya kondoo na ng'ombe, na watu wake wakawa wanaswaga wanyama hao wakiwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine30:20 kuelekea mbele ya wanyama wale wengine: Makala ya Kiebrania si dhahiri. wakisema, “Nyara za Daudi.”
21Daudi akawarudia wale watu 200 ambao waliachwa kwenye kijito cha Besori kwa sababu walikuwa wamechoka kumfuata. Wale watu walipomwona Daudi pamoja na wale waliokuwa pamoja naye, wakaenda kumlaki. Daudi alipofika karibu na watu hao, akawasalimu. 22Lakini watu wote waovu na baradhuli miongoni mwa watu waliofuatana na Daudi, wakasema, “Hatutawapa watu hawa nyara zozote tulizozikomboa kwani hawakwenda pamoja nasi. Ila wawachukue wake zao na watoto wao, waende zao.”
23Daudi akawaambia, “Sivyo ndugu zangu. Hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Mwenyezi-Mungu ametupa. Alitulinda salama, na akalitia mikononi mwetu genge lililokuja kutushambulia. 24Hakuna mtu atakayekubaliana na mawazo yenu! Yule aliyekwenda vitani na yule aliyebaki na mizigo yetu, kila mtu atapewa sehemu inayolingana na mwenzake.” 25Tangu siku hiyo Daudi alifanya uamuzi huo kuwa sheria na kanuni katika nchi ya Israeli hadi hivi leo.
26Daudi aliporejea Siklagi, aliwapelekea rafiki zake, ambao ni wazee wa Yuda, sehemu ya nyara akisema, “Nawapelekea zawadi kutoka nyara za maadui wa Mwenyezi-Mungu.” 27Zawadi hizo zilikuwa kwa ajili ya wakazi wa Betheli, wakazi wa Ramothi katika Negebu, wakazi wa Yatiri, 28wakazi wa Aroeri, wakazi wa Sifmothi, wakazi wa Eshtemoa, 29wakazi wa Rakali, wakazi wa miji ya Wayerameeli, wakazi wa miji ya Wakeni, 30wakazi wa Horma, wakazi wa Borashani, wakazi wa Athaki, 31na wakazi wa Hebroni. Daudi aliwapelekea pia wakazi wa miji yote ambako yeye na watu wake walitembelea.



1Samweli30;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: