Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 31 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 45....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Nitatafakari juu ya kazi zako, na kuwaza juu ya matendo yako makuu. Kila ufanyacho ee Mungu, ni kitakatifu. Ni mungu gani aliye mkuu kama Mungu wetu? Wewe ni Mungu unayetenda maajabu; wewe umeyaonesha mataifa uwezo wako.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Kwa mkono wako wa nguvu uliwakomboa watu wako; uliwakomboa wazawa wa Yakobo na Yosefu. Maji yalipokuona, ee Mungu, maji yalipokuona, yaliogopa mno; naam, bahari ilitetemeka hata vilindini. Mawingu yalichuruzika maji, ngurumo zikavuma angani, mishale ya umeme ikaangaza kila upande. Kishindo cha ngurumo yako kilitokea katika kimbunga, umeme wako ukauangaza ulimwengu; dunia ikatikisika na kutetemeka.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Wewe uliweka njia yako juu ya bahari; ulitembea juu ya maji yale mengi, lakini nyayo zako hazikuonekana. Uliwaongoza watu wako kama kondoo, chini ya uongozi wa Mose na Aroni.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Mwenyezi-Mungu amteua Koreshi
1Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Koreshi:
“Wewe ni mfalme wangu niliyekuteua;
mimi naitegemeza nguvu yako
ili uyashinde mataifa mbele yako,
na kuzivunja nguvu za wafalme.
Mimi nayafungua malango ya mji mbele yako,
na hakuna lango litakalofungwa.
2Mimi nitakutangulia,
na kuisawazisha milima mbele yako.
Nitaivunjavunja milango ya shaba,
na kuvikatakata vizuizi vyake vya chuma.
3Nitakupa hazina zilizofichwa gizani,
na mali iliyo mahali pa siri,
upate kutambua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu,
Mungu wa Israeli, ninayekuita kwa jina lako.
4Kwa ajili ya mtumishi wangu Yakobo,
naam, kwa ajili ya mteule wangu Israeli,
nimekuita kwa jina lako;
nimekupa jina la heshima ingawa wewe hunijui.
5“Mimi ni Mwenyezi-Mungu, wala hakuna mwingine;
hakuna Mungu mwingine ila mimi.
Ninakuimarisha ingawa wewe hunijui,
6ili watu wote, toka mashariki hadi magharibi,
wajue kwamba hakuna Mungu mwingine ila mimi;
mimi ni Mwenyezi-Mungu na hakuna mwingine.
7Mimi hufanya mwanga na kuumba giza;
huleta fanaka na kusababisha balaa.
Mimi Mwenyezi-Mungu hutenda vitu hivi vyote.
8Enyi mbingu, nyesheni kutoka huko juu,
mawingu na yadondoshe uadilifu;
dunia na ifunuke, ichipushe wokovu,
na kuchanusha uadilifu pia!
Mimi, Mwenyezi-Mungu nimefanya hayo.”
Uwezo mkuu wa Mungu
9Ole wake mtu ashindanaye na Muumba wake,
mtu aliye chombo cha udongo
kushindana na mfinyanzi wake!
Je, udongo humwuliza anayeufinyanga:
“Unatengeneza nini hapa?”
Au kumwambia, “Kazi yako si kamili!”
10Ole wake mtoto amwambiaye baba yake,
“Kwa nini umenizaa?”
Au amwambiaye mama yake,
“Ya nini umenileta duniani?”
11Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli,
Mungu, Muumba wa Israeli asema:
“Je, mwathubutu kuniuliza juu ya watoto wangu,
au kuniamuru juu ya kazi zangu mwenyewe?
12Ni mimi niliyeifanya dunia,
na kuumba binadamu aishiye humo.
Mikono yangu ndiyo iliyozitandaza mbingu,
na jeshi lote la nyota liko kwa amri yangu.
13Ni mimi niliyemwamuru Koreshi kuchukua hatua,
atekeleze matakwa yangu.
Nitazifanikisha njia zake zote;
ataujenga upya mji wangu Yerusalemu,
na kuwapa uhuru watu wangu walio uhamishoni,
bila kutaka malipo wala zawadi.”
Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema.
14Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Utajiri wa Misri na bidhaa za Kushi,
pamoja na za watu wa Seba, majitu marefu,
zitakuja kwako mwenyewe wewe taifa la Israeli,
zote zitakuwa mali yako.
Watu hao watakutumikia wamefungwa minyororo;
watakusujudia na kukiri wakisema:
‘Kwako kuna Mungu wa kweli,
wala hakuna Mungu mwingine ila yeye.’”
15Kweli wewe ni Mungu uliyefichika,
Mungu wa Israeli, Mungu Mwokozi.
16Watengenezaji sanamu wataaibika na kufadhaika,
wote kwa pamoja watavurugika.
17Lakini taifa la Israeli litaokolewa na Mwenyezi-Mungu,
litapata wokovu wa milele.
Halitaaibishwa wala kufadhaishwa milele.
18Mwenyezi-Mungu, Mungu pekee,
ndiye aliyeiumba dunia,
ndiye aliyeiumba na kuitegemeza.
Hakuiumba iwe ghasia na tupu,
ila aliiumba ikaliwe na viumbe vyake.
Yeye asema sasa:
“Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu,
wala hakuna mwingine.
19Mimi sikunena kwa siri,
wala katika nchi yenye giza.
Mimi sikuwaambia wazawa wa Yakobo
wanitafute katika ghasia.
Mimi Mwenyezi-Mungu husema ukweli,
maneno yangu ni ya kuaminika.”
20Enyi watu wa mataifa mliosalia,
kusanyikeni pamoja mje!
Nyinyi mmekosa akili:
Nyinyi mwabeba sanamu za miti
na kumwomba mungu asiyeweza kuokoa watu.
21Semeni wazi na kutoa hoja zenu;
shaurianeni pamoja!
Ni nani aliyetangaza zamani matukio ya sasa?
Ni nani aliyetamka mambo haya zamani?
Je, haikuwa mimi Mwenyezi-Mungu?
Hakuna Mungu mwingine ila mimi!
Mimi ni Mungu wa haki na mwokozi;
hakuna mwingine ila mimi.
22Nigeukieni mimi mpate kuokolewa,
popote mlipo duniani.
Maana mimi ni Mungu, wala hakuna mwingine.
23Mimi nimeapa kwa nafsi yangu,
ninachotamka ni ukweli,
neno langu halitarudi nyuma:
Kila binadamu atanipigia magoti,
kila mtu ataapa uaminifu.
24“Watasema juu yangu,
‘Haki na nguvu viko kwa Mwenyezi-Mungu peke yake.’”
Wote waliomwakia hasira Mwenyezi-Mungu
watamjia yeye na kuaibishwa.
25Lakini wazawa wa Israeli
watapata ushindi kwake Mwenyezi-Mungu na kufurahi.


Isaya45;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: