Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 21 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 37....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

Nguvu na uadilifu wako, ee Mungu, vyafika mpaka mbingu za juu. Wewe umefanya mambo makuu mno. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe?
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Umenifanya nione taabu nyingi ngumu, lakini utanirudishia tena uhai, wewe utaniinua tena kutoka huko chini. Utaniongezea heshima yangu, na kunifariji tena. Nitakusifu pia kwa kinubi, kwa sababu ya uaminifu wako, ee Mungu wangu; nitakuimbia sifa kwa zeze, ewe Mtakatifu wa Israeli.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Nitapaza sauti kwa furaha, ninapokuimbia wewe sifa zako, na roho yangu itakusifu maana umeniokoa. Nitatamka uadilifu wako mchana kutwa, maana waliotaka kuniumiza wameaibishwa na kufedheheshwa.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

Mfalme anaomba shauri kwa nabii Isaya
(2Fal 19:1-7)
1Basi, mfalme Hezekia aliposikia habari hiyo alirarua mavazi yake, akavaa vazi la gunia, akaingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 2Aliwaamuru Eliakimu, mkuu wa ikulu, Shebna, katibu, na wazee wa makuhani, wamwendee nabii Isaya mwana wa Amozi, wakiwa wamevaa mavazi ya magunia. 3Nao wakamwambia Isaya, “Hezekia anasema hivi, ‘Leo ni siku ya huzuni, siku ya kukemewa, na ya dharau. Sisi tumekuwa kama mama anayetaka kujifungua mtoto, lakini hana nguvu ya kumzaa. 4Inawezekana kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wako alisikia maneno ya mkuu wa matowashi ambaye ametumwa na mfalme wa Ashuru, bwana wake, ili kumtukana Mungu aliye hai, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako atapinga maneno aliyoyasikia; kwa hiyo waombee watu waliobaki.’”
5Basi, hao watumishi wa mfalme Hezekia walipokwisha fika kwa Isaya, 6yeye akawaambia, “Mwambieni bwana wenu kwamba Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Usiogope kwa sababu ya maneno ya watumishi wa mfalme wa Ashuru uliyoyasikia, maneno ambayo wameyasema kunidharau. 7Tazama nitamfanya mfalme asikie uvumi halafu atarudi katika nchi yake, na huko nitamfanya auawe kwa upanga.’”
Waashuru wanatishia tena
(2Fal 19:8-19)
8Kisha yule mkuu wa matowashi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru alikuwa ameondoka Lakishi, aliondoka na kumkuta akishambulia mji wa Libna. 9Halafu aliposikia habari kwamba Tirhaka mfalme wa Kushi anakuja kupigana naye, alituma wajumbe kwa Hezekia, akisema, 10“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: ‘Usikubali Mungu wako unayemtegemea akudanganye kwa kukuahidi kwamba Yerusalemu hautatekwa na mfalme wa Ashuru. 11Wewe umekwisha sikia jinsi wafalme wa Ashuru walivyozitenda nchi nyingine na kuziangamiza kabisa. Je, unadhani wewe utaokoka? 12Je, miungu ya mataifa iliokoa Gozani, Harani, Resefu na Waedeni waliokaa Telasari, mataifa ambayo wazee wangu waliyaangamiza? 13Wako wapi wafalme wa Hamathi, Arpadi, Sefarvaimu, Hena na Iva?’”
14Mfalme Hezekia alipokea barua kutoka kwa wajumbe na kuisoma. Kisha akaenda na kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaiweka mbele ya Mwenyezi-Mungu. 15Halafu akamwomba Mwenyezi-Mungu akisema; 16“Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, unayeketi katika kiti cha enzi juu ya viumbe wenye mabawa.37:16 viumbe wenye mabawa: Taz Kut 25:52; Kiebrania: Makerubi. Wewe ndiwe uliyeumba mbingu na dunia. 17Ee, Mwenyezi-Mungu, fumbua macho uone, tega sikio lako, uyasikie matusi yote ambayo Senakeribu amepeleka na kukutukana wewe Mungu uliye hai. 18Ee Mwenyezi-Mungu, ni kweli kwamba wafalme wa Ashuru wameangamiza mataifa yote na nchi zao. 19Waliweza kuitupa miungu yao motoni, kwa sababu haikuwa miungu kweli bali sanamu za miti au mawe zilizochongwa na mikono ya watu. 20Sasa ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, utuokoe makuchani mwa Senakeribu, ili falme zote za dunia zijue kwamba wewe peke yako ndiwe uliye Mwenyezi-Mungu.”
Ujumbe wa Isaya kwa mfalme
(2Fal 19:20-37)
21Kisha Isaya mwana na Amozi, alituma ujumbe kwa Hezekia akisema, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: Kwa kuwa umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru, 22basi huu ndio ujumbe wangu kuhusu huyo mfalme:
Mji wa Siyoni, naam, Yerusalemu,
unakudharau na kukutukana.
Yerusalemu, mji mzuri
unakutikisia kichwa kwa dhihaka.
23Wewe umemtukana nani?
Umemkashifu nani?
Umethubutu kumbeza nani kwa majivuno?
Ni mimi Mungu, Mtakatifu wa Israeli!
24Umewatumia watumishi wako kunidhihaki mimi Bwana;
wewe umesema, ‘Kwa magari yangu mengi ya vita,
nimekwea vilele vya milima,
mpaka kilele cha Lebanoni.
Nimeangusha mierezi yake mirefu,
na misonobari mizurimizuri.
Nimevifikia vilele vyake
na ndani ya misitu yake mikubwa.
25Nimechimba visima na kunywa maji yake,
na nilikausha vijito vya Misri
kwa nyayo za miguu yangu.’
26“Je, hujasikia ewe Senakeribu kwamba
nilipanga jambo hili tangu zamani?
Ninachotekeleza sasa nilikipanga zamani.
Nilikuweka uifanye miji yenye ngome
kuwa rundo la magofu.
27Wakazi wake wakiwa wameishiwa nguvu,
wametishika na kufadhaika.
Wamekuwa kama mimea shambani,
kama nyasi changa shambani,
kama majani yaotayo juu ya paa
au kama ngano kabla hazijakomaa
ambazo hunyauka upepo mkavu uvumapo.
28Lakini, nakujua wewe Senakeribu;
najua kila unachofanya na kuacha kufanya;
najua mipango yako dhidi yangu.
29Kwa vile umefanya mipango dhidi yangu
na nimeusikia ufidhuli wako,
nitatia ndoana yangu puani mwako,
na lijamu yangu kinywani mwako.
Nitakurudisha njia ileile uliyojia.”
30“Na hii ndiyo itakuwa ishara kwako Hezekia: Mwaka huu na mwaka ujao mtakula kinachomea chenyewe bila kupandwa. Lakini katika mwaka wa tatu mtapanda na kuvuna mavuno; mtapanda mizabibu na kula matunda yake. 31Wale watakaobaki katika ukoo wa Yuda wataongezeka na kuwa wengi kama vile mti unavyotoa mizizi yake udongoni na kuzaa matunda juu. 32Maana kutakuwa na watu watakaosalia huko Yerusalemu; naam, huko mlimani Siyoni kutakuwako watu wachache watakaosalimika.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amedhamiria kukamilisha hayo.
33Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu, wala kuupiga mshale wala kuingia kwa ngao wala kuuzingira. 34Atarudi kwa njia ileile aliyojia na wala hataingia katika mji huu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimetamka hayo. 35Naam, kwa ajili ya heshima yangu mimi na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi nitaulinda na kuuokoa mji huu.”
36Basi, wakati wa usiku malaika wa Mwenyezi-Mungu aliingia kambini mwa Waashuru na kuwaua watu 185,000. Halafu kulipopambazuka watu hao wote walionekana wakiwa maiti. 37Kisha Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda kwake, akakaa Ninewi. 38Siku moja, wakati Senakeribu alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki mungu wake, wanawe wawili, Adrameleki na Sharezeri, walimuua kwa upanga, halafu wakakimbilia nchini Ararati. Naye Esar-hadoni, mwanawe, akatawala badala yake.

Isaya37;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: