Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 24 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 40....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu. Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande 50,000 vya fedha. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Tumaini la kuponywa katika Yerusalemu
1Mungu wenu asema:
“Wafarijini watu wangu,
nendeni mkawafariji.
2Semeni na wenyeji wa Yerusalemu kwa upole,
waambieni kwamba utumwa wao umekwisha,
wamesamehewa uovu wao.
Mwenyezi-Mungu amewaadhibu maradufu
kwa sababu ya dhambi zao zote.”
3Sauti ya mtu anaita jangwani:
“Mtayarishieni Mwenyezi-Mungu njia,
nyosheni barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu.
4Kila bonde litasawazishwa,
kila mlima na kilima vitashushwa;
ardhi isiyo sawa itafanywa sawa,
mahali pa kuparuza patalainishwa.
5Kisha utukufu wa Mwenyezi-Mungu utafunuliwa,
na watu wote pamoja watauona.
Mwenyezi-Mungu mwenyewe ametamka hayo.”
6Sikiliza! Kuna sauti inasema, “Tangaza!”
Nami nikauliza, “Nitangaze nini?”
Naye: “Tangaza: Binadamu wote ni kama majani;
uthabiti wao ni kama ua la shambani.
7Majani hunyauka na ua hufifia,
Mwenyezi-Mungu avumishapo upepo juu yake.
Hakika binadamu ni kama majani.
8Majani hunyauka na ua hufifia,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
9Nenda juu ya mlima mrefu,
ewe Siyoni, ukatangaze habari njema.
Paza sauti yako kwa nguvu,
ewe Yerusalemu, ukatangaze habari njema.
paza sauti yako bila kuogopa.
Iambie miji ya Yuda:
“Mungu wenu anakuja.”
10Bwana Mungu anakuja na nguvu,
kwa mkono wake anatawala.
Zawadi yake iko pamoja naye,
na tuzo lake analo.
11Atalilisha kundi lake kama mchungaji,
atawakusanya wanakondoo mikononi mwake,
atawabeba kifuani pake,
na kondoo wanyonyeshao atawaongoza polepole.
Mungu wa Israeli hana kifani
12Nani awezaye kupima maji ya bahari kwa konzi yake,
kuzipima mbingu kwa mikono yake?
Nani awezaye kuutia udongo wa dunia kikombeni;
kuipima milima kwa mizani
au vilima kwa kipimo cha uzani?
13 Nani awezaye kuiongoza akili ya Mwenyezi-Mungu,
au kuwa mshauri wake na kumfunza?
14Mwenyezi-Mungu alimtaka nani shauri,
ndipo akapata kuwa mwenye ujuzi?
Nani aliyemfunza njia za haki?
Nani aliyemfundisha maarifa,
na kumwonesha namna ya kuwa na akili?
15Kwake mataifa ni kama tone la maji katika ndoo,
ni kama vumbi juu ya mizani.
Kwake visiwa ni vyepesi kama vumbi laini.
16Kuni zote za Lebanoni
na wanyama wake wote
havitoshi kwa sadaka ya kuteketezwa mbele yake.
17Mataifa yote si kitu mbele yake;
kwake ni vitu duni kabisa na batili.
18Mtamlinganisha Mungu na nini basi,
au ni kitu gani cha kumfananisha naye?
19Je, anafanana na kinyago?
Hicho, fundi hukichonga,
mfua dhahabu akakipaka dhahabu,
na kukitengenezea minyororo ya fedha!
20Au ni sanamu ya mti mgumu?
Hiyo ni ukuni mtu anaochagua,
akamtafuta fundi stadi,
naye akamchongea sanamu imara!
21Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Je, hamkuambiwa tangu mwanzo?
Je, hamjafahamu mwanzo wa dunia?
22Dunia iliumbwa na huyo aketiye juu ya mbingu;
kutoka huko wakazi wa dunia ni kama panzi!
Yeye amezitandaza mbingu kama pazia,
na kuzikunjua kama hema la kuishi.
23Yeye huwaporomosha wakuu wenye nguvu,
watawala wa dunia huwafanya kuwa si kitu.
24Mara tu wanaposimikwa na kuanza kuota,
hata kabla hawajatoa mizizi kama miti udongoni,
Mwenyezi-Mungu akiwapulizia hunyauka,
kimbunga huwapeperusha kama makapi!
25Mungu Mtakatifu auliza hivi:
“Nani basi, mtakayemlinganisha nami?
Je, kuna mtu aliye kama mimi?”
26Inueni macho yenu juu mbinguni!
Je, ni nani aliyeziumba nyota hizo?
Ni yule aziongozaye kama jeshi lake,
anayeijua idadi yake yote,
aziitaye kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu yeye ni mwenye nguvu nyingi,
hakuna hata moja inayokosekana.
27Enyi watu wa Israeli wazawa wa Yakobo,
kwa nini mnalalamika na kusema:
“Mwenyezi-Mungu hatujali sisi!
Mungu wetu hajali haki yetu!”
28Je, nyinyi bado hamjui?
Je, hamjapata kusikia?
Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu wa milele;
yeye ndiye Muumba wa kila kitu duniani.
Yeye hafifii kamwe wala kuishiwa nguvu.
Maarifa yake hayachunguziki.
29Yeye huwapa uwezo walio hafifu,
wanyonge huwapa nguvu.
30Hata vijana watafifia na kulegea;
naam, wataanguka kwa uchovu.
31Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu,
watapata nguvu mpya.
Watapanda juu kwa mabawa kama tai;
watakimbia bila kuchoka;
watatembea bila kulegea.


Isaya40;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: