Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 10 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 30....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Kisha mfalme Daudi akaingia ndani ya hema na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu akaomba, “Mimi ni nani, ee Mwenyezi-Mungu, na nyumba yangu ni nini hata unitukuze hivi? Isitoshe, umenifanyia mengine zaidi: Umenitolea ahadi juu ya vizazi vyangu vijavyo ee Mwenyezi-Mungu! Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi mtumishi wako, kwa kunitukuza hivyo? Wewe unanijua mimi mtumishi wako.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Ee Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa kufuatana na moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote. Hakuna mwingine kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu, na yote tunayoyasikia yanathibitisha kwamba hakuna Mungu mwingine ila wewe.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Tena ni watu gani duniani ambao wanaweza kulinganishwa na watu wako wa Israeli ambao peke yao Mungu wao alikwenda kuwakomboa ili wawe watu wake? Wewe ulijifanyia jina kwa kutenda mambo makubwa na ya ajabu hapo ulipoyafukuza mataifa mbele ya watu wako ambao uliwakomboa kutoka Misri. Hata umejifanyia watu wako wa Israeli kuwa watu wako milele; nawe ee Mwenyezi-Mungu, umekuwa Mungu wao.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Ole wao watoto wanaoniasi,
wanaotekeleza mipango yao na si mipango yangu,
wanaofanya mikataba kinyume cha matakwa yangu!
Naam, wanarundika dhambi juu ya dhambi.
2Bila kunitaka shauri, wanafunga safari kwenda Misri,
kukimbilia usalama katika ulinzi wa Farao,
kupata mahali pa usalama nchini Misri.
3Lakini ulinzi wa Farao utakuwa aibu yenu,
na usalama nchini Misri utakuwa fedheha yenu.
4Maana ingawa maofisa wao wamefika Soani,
na wajumbe wao mpaka Hanesi,
5wote wataaibishwa na hao wasioweza kuwasaidia,
watu ambao hawawezi kuwapa msaada au faida,
ila tu kuwapa aibu na fedheha.”
6Kauli ya Mungu juu ya wanyama wa pande za Negebu:30:6 Negebu: Au, kusini. Namna nyingine ya kutaja Misri.
“Wajumbe wanapita katika nchi ya taabu na shida,
yenye simba, nyoka wa sumu na majoka.
Wamewabebesha wanyama wao mali zao,
kuwapelekea watu wasioweza kuwafaa kitu.
7Maana msaada wa Misri ni bure, haufai kitu;
kwa hiyo nimeipanga Misri jina:
‘Joka30:7 Joka: Kiebrania: Rahabu. lisilo na nguvu!’”
Watu wasiotii
8Mungu aliniambia:
“Sasa chukua kibao cha kuandikia,
uandike jambo hili mbele yao,
liwe ushahidi wa milele:
9Watu hawa ni waasi, watoto wasioaminika;
watu wasiopenda kusikia mafunzo ya Mwenyezi-Mungu.
10Huwaambia waonaji: ‘Msione maono’,
na manabii: ‘Msitutangazie ukweli,
bali tuambieni mambo ya kupendeza,
toeni unabii wa mambo ya udanganyifu tu.
11Geukeni na kuiacha njia ya ukweli;
msituambie tena juu ya Mungu, Mtakatifu wa Israeli.’”
12Kwa hiyo Mungu, Mtakatifu wa Israeli asema:
“Nyinyi mmeukataa ujumbe wangu;
mkapania kufanya dhuluma na udanganyifu.
13Basi, dhambi hii itawaleteeni maangamizi
kama ufa mkubwa katika ukuta mrefu;
utabomoka mara na kuanguka chini ghafla.
14Kuporomoka kwa ukuta huo,
ni kama kupasuka kwa chungu
ambacho kimepasuliwa vibaya sana,
bila kusalia kigae cha kuchukulia moto mekoni,
au kuchotea maji kisimani.”
15Bwana Mungu, Mtakatifu wa Israeli, asema:
“Mkinirudia na kutulia mtaokolewa;
kwa utulivu na kunitumainia mtapata nguvu.”
Lakini nyinyi hamkutaka.
16Badala yake mlisema,
“La! Sisi tutakimbia na farasi wenye mbio.”
Sawa, mtakimbia na farasi wenye mbio,
lakini farasi wa maadui zenu wana mbio zaidi.
17Watu wenu elfu moja watamkimbia askari mmoja adui;
na askari watano maadui watawakimbizeni nyote.
Mwishowe, watakaosalia
watakuwa kama mlingoti wa bendera mlimani,
kama alama iliyo juu ya kilima.
Wakati wa wokovu
18Hata hivyo, Mwenyezi-Mungu anangoja awafadhili,
atainuka na kuwaonea huruma.
Maana, Mwenyezi-Mungu ni Mungu atendaye haki.
Heri wote wale wanaomtumainia.
19Enyi watu wa Siyoni, enyi watu wa Yerusalemu, hakika nyinyi hamtaomboleza tena. Kweli Mungu atawahurumia; mara tu atakaposikia kilio chenu atawaitikeni. 20Ingawa Bwana atawalisha taabu na kuwanywesha dhiki, yeye ndiye Mwalimu wenu na hatajificha tena; nanyi mtamwona kwa macho yenu wenyewe. 21Mkienda kulia au kushoto, mtasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Njia ni hii; ifuateni.” 22Mtavifanya haramu vinyago vyenu vya miungu vilivyopakwa fedha na sanamu zenu zilizopakwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitu najisi, mkisema, “Poteleeni mbali!” 23Mtakapopanda mbegu zenu, Mwenyezi-Mungu atanyesha mvua kwa wakati wake, nazo zitakua na kuwapa mavuno mengi. Mifugo yenu nayo itapata malisho kwa wingi. 24Mafahali na punda wenu wa kulimia watapata malisho yaliyochambuliwa vizuri na kutiwa chumvi. 25Wakati utakapofika ambapo maadui watauawa na ngome zao kubomolewa, vijito vya maji vitatiririka kutoka kila mlima na kilima. 26Tena mwezi utawaka kama jua, nao mwanga wa jua utakuwa mara saba ya mwanga wake wa kawaida, kana kwamba mwanga wa siku saba umeangaza katika siku moja. Mambo haya yote yatatukia wakati Mwenyezi-Mungu atakapoyafunga na kuyaponya majeraha aliyowaletea watu wake.
Mungu ataiadhibu nchi ya Ashuru
27Tazameni, Mwenyezi-Mungu mwenyewe anakuja toka mbali!
Amewaka hasira na moshi wafuka;
midomo yake yaonesha ghadhabu yake,
maneno anayosema ni kama moto uteketezao.
28Pumzi yake ni kama mafuriko ya mto
ambao maji yake yanafika hadi shingoni.
Anakuja kuyachekecha mataifa kwa chekecheke ya maangamizi,
kuwafunga lijamu na kuwapeleka wasikotaka.
29Lakini nyinyi watu wa Yerusalemu mtaimba kwa furaha kama mfanyavyo wakati wa mkesha wa sikukuu. Mtajaa furaha kama watu wanaotembea kwa mdundo wa muziki wa filimbi kwenda mlimani kwa Mwenyezi-Mungu, Mwamba wa Israeli.
30Mwenyezi-Mungu atawafanya watu wote waisikie sauti yake tukufu na pigo la nguvu yake lionekane kwa hasira nyingi. Kutakuwa na ndimi za moto mkali, ngurumo, dhoruba na mvua ya mawe. 31Waashuru watajaa hofu watakaposikia sauti ya Mwenyezi-Mungu wakati atakapowachapa na fimbo yake. 32Kila pigo la adhabu ya Mwenyezi-Mungu juu ya Waashuru litaandamana na mdundo wa ngoma na zeze. Yeye mwenyewe binafsi atapigana na Waashuru. 33Naam, mahali pa kumteketeza mfalme wa Ashuru pamekwisha tayarishwa muda mrefu uliopita. Mahali penyewe ni shimo kubwa na pana. Moto upo na kuni kwa wingi. Mwenyezi-Mungu ataupulizia pumzi yake kama kijito cha madini ya kiberiti na kuuwasha.

Isaya30;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: