Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 18 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 36....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Maana maadui zangu wanasema vibaya juu yangu; wanaovizia uhai wangu wanafanya mipango, na kusema: “Mungu amemwacha; mfuateni na kumkamata, kwani hakuna wa kumwokoa!” Usikae mbali nami, ee Mungu; uje haraka kunisaidia, ee Mungu wangu. Wapinzani wangu wote waaibishwe na kuangamizwa; wenye kutaka kuniumiza wapate aibu na fedheha.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Lakini mimi nitakuwa na matumaini daima; tena nitakusifu zaidi na zaidi. Kinywa changu kitatamka matendo yako ya haki, nitatangaza mchana kutwa matendo yako ya wokovu ijapokuwa hayo yanapita akili zangu. Nitataja matendo yako makuu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu; nitatangaza kuwa ndiwe mwadilifu peke yako.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Ee Mungu, wewe umenifunza tangu ujana wangu; tena na tena, natangaza matendo yako ya ajabu. Usiniache, ee Mungu, niwapo mzee mwenye mvi, hata nivitangazie vizazi vijavyo nguvu yako.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Waashuru wanatishia Yerusalemu
(2Fal 18:13-37; 2Nya 32:1-19)
1Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia,36:1 Ashuru iliishambulia Yuda mwaka 701 K.K. mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka. 2Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu kutoka Lakishi na jeshi kubwa kumwendea mfalme Hezekia. Jemadari alisimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea uwanda wa Dobi. 3Nao walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa ikulu, Shebna aliyekuwa katibu, pamoja na mwandishi Yoa mwana wa Asafu.
4Ndipo mkuu wa matowashi wa Ashuru alipowaambia, “Mwambieni Hezekia kuwa mfalme mkuu wa Ashuru anamwuliza, ‘Je, unategemea nini kwa ukaidi wako huo? 5Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi?
6 36:6 Taz Eze 29:6-7 Angalia! Sasa unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeuegemea. Hivyo ndivyo Farao, mfalme wa Misri alivyo, kwa wote wale wanaomtegemea.’ 7Lakini hata kama mkiniambia, ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,’ je, si huyohuyo ambaye Hezekia aliziharibu madhabahu zake na kuwaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, ‘Mnapaswa kuabudu mbele ya madhabahu hii?’ 8Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru; mimi nitawapatieni farasi 2,000, kama mtaweza kupata wapandafarasi. 9Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu aliye na cheo cha chini sana wakati mnategemea Misri kupata magari ya vita na wapandafarasi! 10Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia ‘Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!’”
11Kisha Eliakimu, Shebna na Yoa wakamjibu mkuu wa matowashi, “Tafadhali sema nasi kwa lugha ya Kiaramu maana tunaielewa. Usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikia.” 12Yule mkuu wa matowashi akawaambia, “Je unadhani bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu wenyewe tu? Maneno yangu ni pia kwa watu wanaokaa ukutani! Muda si muda wao kama vile nyinyi itawabidi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe!”
13Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 14Hiki ndicho anachosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa. 15Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu hakika atatuokoa na mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 16Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru anasema: ‘Muwe na amani nami, na kujisalimisha kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe na ya matunda ya mtini wake mwenyewe na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe. 17Mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapelekeni katika nchi kama hii yenu; nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mkate36:17 mkate: Tafsiri nyingine: Ngano. na mashamba ya mizabibu.’ 18Angalieni basi Hezekia asiwahadae akisema kwamba Mwenyezi-Mungu atawaokoeni. Je, kuna yoyote kati ya miungu ya mataifa aliyewahi kuokoa nchi yake mkononi mwa mfalme wa Ashuru? 19Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria mkononi mwangu? 20Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao katika mkono wangu, hata iwe kwamba Mwenyezi-Mungu ataweza kuuokoa mji wa Yerusalemu mkononi mwangu?”
21Lakini watu walinyamaza, wala hawakumjibu neno kama vile walivyoamriwa na mfalme akisema, “Msimjibu.” 22Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa mkuu wa ikulu, katibu Shebna, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi, wakamwendea mfalme Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruliwa, wakamweleza maneno ya mkuu wa matowashi.


Isaya36;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: