Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 8 October 2019

Kikombe Cha Asubuhi;Isaya 28....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Wakati mfalme Daudi alipokuwa akikaa katika ikulu, siku moja alimwita nabii Nathani, na kumwambia, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mwerezi, lakini sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu linakaa hemani.” Nathani akamwambia Daudi, “Fanya chochote unachofikiria moyoni mwako, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe.”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Lakini usiku uleule, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Nathani, kusema, “Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Wewe hutanijengea nyumba ya kukaa.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Tangu wakati ule nilipowaongoza watu wa Israeli kutoka Misri mpaka hivi leo, sijaishi kwenye nyumba. Nimekuwa nikihama toka hema hadi hema, na toka makao hadi makao mengine. Je, kila mahali ambako nimekwenda na Waisraeli, nimepata kumwuliza mwamuzi wao yeyote niliyemwamuru awachunge watu wangu, “Kwa nini hukunijengea nyumba ya mierezi?” ’
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Onyo kwa ufalme wa kaskazini
1Ole wenye majivuno na walevi wa Efraimu,
fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka!
Naam, fahari iliyotawala bondeni kwenye rutubarutuba;
na vichwani kwao walio watu walevi kupindukia!
2Bwana amejichagulia mtu wake shujaa na mwenye nguvu,
ambaye ni kama mvua ya mawe na dhoruba kali,
kama tufani ya mafuriko makubwa;
kwa mkono wake atawatupa chini ardhini.
3Majivuno na fahari ya walevi wa Efraimu
yatakanyagwakanyagwa ardhini,
4fahari yake inatoweka kama ua linalonyauka;
fahari iliyotawala bondeni kwenye rutuba
itakuwa kama tini za mwanzo kabla ya kiangazi;
mtu akiziona huzichuma na kuzila mara moja.
5Siku ile Mwenyezi-Mungu wa majeshi atakuwa taji tukufu,
kama kilemba kizuri kwa watu wake watakaobaki hai.
6Waamuzi mahakamani atawaongoza kutenda haki,
nao walinzi wa mji atawapa nguvu.
Isaya na manabii walevi wa Yuda
7Lakini wako wengine waliolewa divai
na kuyumbayumba kwa sababu ya pombe;
naam, makuhani na manabii wamelewa mvinyo,
wamevurugika kwa divai.
Wanayumbayumba kwa pombe kali;
maono yao yamepotoka,
wanapepesuka katika kutoa hukumu.
8Meza zote zimetapakaa matapishi,
hakuna mahali popote palipo safi.
9Wao wananidhihaki na kuuliza:
“Huyu nabii ataka kumfundisha nani?
Je, anadhani atatueleza sisi ujumbe wake?
Je, sisi ni watoto wachanga
walioachishwa kunyonya juzijuzi?
10Anatufundisha kama watoto wadogo:
Sheria baada ya sheria,
mstari baada ya mstari;
mara hiki, mara kile!”
11 28:11-12 Taz 1Kor 14:21 Haya basi!
Mwenyezi-Mungu ataongea na watu hawa
kwa njia ya watu wa lugha tofauti
wanaoongea lugha ngeni.
12Hata hivyo yeye alikuwa amewaahidi:
“Nitawaonesheni pumziko,
nitawapeni pumziko enyi mliochoka.
Hapa ni mahali pa pumziko.”
Lakini wao hawakutaka kunisikiliza.
13Kwa hiyo kwao neno la Mwenyezi-Mungu litakuwa tu:
Sheria sheria, mstari mstari;
mara hiki, mara kile!
Nao watalazimika kukimbia
lakini wataanguka nyuma;
watavunjika, watanaswa na kutekwa.
Jiwe la msingi Siyoni
14Basi, sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu,
enyi wenye madharau mnaotawala watu wa Yerusalemu,
15“Nyinyi mnajidai mmefanya mkataba na kifo,
mmefanya mapatano na Kuzimu!
Nyinyi mwasema eti balaa lijapo halitawapata,
kwa sababu mmefanya uongo kuwa tegemeo lenu,
na udanganyifu kuwa kinga yenu!”
16 28:16 Taz Zab 118:22-23; Rom 9:33; 10:11; 1Pet 2:6 Basi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu:
“Tazama! Naweka mjini Siyoni jiwe la msingi,
jiwe ambalo limethibitika.
Jiwe la pembeni, la thamani,
jiwe ambalo ni la msingi thabiti;
jiwe lililo na maandishi haya:
‘Anayeamini hatatishika.’
17Nitatumia haki kama kipimo changu,
nitatumia uadilifu kupimia.”
Mvua ya mawe itaufagilia mbali uongo mnaoutegemea,
na mafuriko yataharibu kinga yenu.
18Hapo mkataba wenu na kifo utabatilishwa,
na mapatano yenu na Kuzimu yatafutwa.
Janga lile kuu litakapokuja
litawaangusheni chini.
19Kila litakapopitia kwenu litawakumba;
nalo litapita kila asubuhi, mchana na usiku.
Kusikia ujumbe huu tu kutakuwa kitisho.
20Kwenu itakuwa kama ajinyoshaye juu ya kitanda kifupi mno,
au kujifunika kwa blanketi lililo dogo mno!
21 28:21 Taz Yos 10:10-12; 2Sam 5:20; 1Nya 14:11 Maana Mwenyezi-Mungu atainuka kama kule mlimani Perazimu;
atawaka hasira kama kule bondeni Gibeoni.
Atatekeleza mpango wake wa ajabu;
atatenda kazi yake ya kustaajabisha.
22Basi, nyinyi msiwe na madharau
vifungo vyenu visije vikakazwa zaidi.
Maana nimesikia kuwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi
ameazimia kuiangamiza nchi yote.
Hekima ya Mungu
23Tegeni sikio msikilize ninayowaambieni;
sikilizeni kwa makini hotuba yangu.
24Je, alimaye ili kupanda hulima tu?
Je, huendelea kulima na kusawazisha shamba lake?
25La! Akisha lisawazisha shamba lake,
hupanda mbegu za bizari na jira,
akapanda ngano na shayiri katika safu,
na mipakani mwa shamba mimea mingineyo.
26Mtu huyo huwa anajua la kufanya,
kwa sababu Mungu wake humfundisha.
27Bizari haipurwi kwa mtarimbo
wala jira kwa gari la ng'ombe!
Ila bizari hupurwa kwa kijiti
na jira kwa fimbo.
28Mkulima apurapo ngano yake,
haendelei kuipura mpaka kuvunja punje zake.
Anajua jinsi ya kuipura kwa gurudumu,
bila kuziharibu punje za ngano.
29Ujuzi huu nao watoka kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Mipango yake Mungu ni ya ajabu,
hekima yake ni kamilifu kabisa.

Isaya28;1-29

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: