Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 22 July 2019

Kikombe Cha Asubuhi ; Methali 23...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!

“Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuondoa hatia. Sadaka hiyo ni takatifu kabisa. Mnyama wa sadaka ya kuondoa hatia atachinjiwa mahali wanapochinjiwa wanyama wa sadaka za kuteketezwa, na damu yake itarashiwa madhabahu pande zake zote.
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Mafuta yake yote: Mafuta ya mkia na yale yanayofunika matumbo yatatolewa na kuteketezwa pamoja na zile figo mbili pamoja na mafuta yake na ile sehemu bora ya ini.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kuhani ataviteketeza juu ya madhabahu kama sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni sadaka ya kuondoa hatia. Wanaoruhusiwa kula sadaka hiyo ni wanaume wa ukoo wa makuhani peke yao; ni sadaka takatifu kabisa. Italiwa katika mahali patakatifu.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.

- 6 -
1Ukiketi kula pamoja na mtawala,
usisahau hata kidogo uko pamoja na nani.
2Zuia sana hamu yako,
ikiwa wewe wapenda sana kula.
3Usitamani vyakula vyake vizuri,
maana vyaweza kukudanganya.
- 7 -
4Ikiwa unayo hekima ya kutosha,
usijitaabishe kutafuta utajiri.
5Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,
huwa kama umepata mabawa ghafla,
ukaruka na kutowekea angani kama tai.
- 8 -
6Usile chakula cha mtu bahili,
wala usitamani mapochopocho yake,
7maana moyoni mwake anahesabu unachokula.23:7 maana … unachokula: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
Atakuambia, “Kula, kunywa!”
Lakini moyoni mwake hayuko pamoja nawe.
8Utatapika vipande ulivyokula;
shukrani zako zote zitakuwa za bure.
- 9 -
9Usiseme maneno yako mbele ya mpumbavu,
maana atapuuza hekima ya maneno yako.
- 10 -
10Usiondoe alama ya mpaka wa zamani,
wala usiingilie mashamba ya yatima,
11maana Mungu, Mkombozi, ni mwenye nguvu,
naye ataitetea haki yao dhidi yako.
- 11 -
12Tumia akili zako kufuata mafundisho;
tumia masikio yako kusikiliza maarifa.
- 12 -
13Usiache kumrudi mtoto;
ukimchapa kiboko hatakufa.
14Ukimtandika kiboko,
utayaokoa maisha yake na kuzimu.
- 13 -
15Mwanangu, moyo wako ukiwa wenye busara,
moyo wangu pia utakuwa wenye furaha.
16Moyo wangu utashangilia,
mdomo wako utakaposema maneno yaliyo sawa.
- 14 -
17Moyo wako usiwaonee wivu wenye dhambi,
ila endelea kumcha Mwenyezi-Mungu siku zote.
18Hakika kuna kesho ya milele,
na tumaini lako halitakuwa bure.
- 15 -
19Sikia mwanangu, uwe na hekima;
fikiria sana jinsi unavyoishi.
20Usiwe mmoja wa walevi wa divai,
wala walafi wenye kupenda nyama,
21maana walevi na walafi wataishia kuwa maskini,
anayetumia siku yake kusinzia atavaa matambara.
- 16 -
22Msikilize baba yako aliyekuzaa,
wala usimdharau mama yako akizeeka.
23Nunua ukweli, wala usiuuze;
nunua hekima, mafunzo na busara.
24Baba wa mtoto mwadilifu atajaa furaha;
anayemzaa mtoto mwenye hekima atamfurahia.
25Wafurahishe baba na mama yako;
mama aliyekuzaa na afurahi.
- 17 -
26Mwanangu, nisikilize kwa makini,
shikilia mwenendo wa maisha yangu.
27Malaya ni shimo refu la kutega watu;
mwanamke mgeni ni kama kisima chembamba.
28Yeye hunyemelea kama mnyanganyi,
husababisha wanaume wengi kukosa uaminifu.
- 18 -
29Ni nani wapigao yowe?
Ni nani wenye huzuni?
Ni nani wenye ugomvi?
Ni nani walalamikao?
Ni nani wenye majeraha bila sababu?
Ni nani wenye macho mekundu?
30Ni wale ambao hawabanduki penye divai,
wale wakaao chonjo kuonja divai iliyokolezwa.
31Usiitamani divai hata kwa wekundu wake,
hata kama inametameta katika bilauri,
na kushuka taratibu unapoinywa.
32Mwishowe huuma kama nyoka;
huchoma kama nyoka mwenye sumu.
33Macho yako yataona mauzauza,
moyo wako utatoa mambo yaliyopotoka.
34Utakuwa kama mtu alalaye katikati ya bahari,
kama mtu alalaye juu ya mlingoti wa meli.
35Utasema, “Walinichapa, lakini sikuumia;
walinipiga, lakini sina habari.
Nitaamka lini?
Ngoja nitafute kinywaji kingine!”


Methali23;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: