Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 16 July 2019

Kikombe Cha Asubuhi ; Methali 19...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Mtakusanya nyara zake zote katika uwanja wa hadhara wa mji na kuzichoma kwa moto kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wenu; mji huo utakuwa rundo la magofu milele, nao hautajengwa tena.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Msichukue kitu chochote kilichotolewa kiteketezwe, ili Mwenyezi-Mungu aache ile hasira yake kali, awaoneshe rehema na huruma, na kuwafanya muwe wengi sana kama alivyowaahidi babu zenu,
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

kama tu mtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkishika amri zake zote ninazowapa hivi leo, na kufanya yaliyo sawa mbele yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

1Afadhali maskini aishiye kwa unyofu,
kuliko mtu mpotovu wa maneno na mpumbavu.
2Haifai mtu kuwa bila akili;
mwenda harakaharaka hujikwaa.
3Mtu akijiangamiza kwa upumbavu wake,
huielekeza hasira yake dhidi ya Mwenyezi-Mungu.
4Mali huvuta marafiki wengi wapya,
lakini maskini huachwa bila rafiki.
5Shahidi mwongo hataacha kuadhibiwa;
asemaye uongo hataepa adhabu.
6Watu wengi hujipendekeza kwa wakuu;
kila mtu hutaka kuwa rafiki ya mtu mkarimu.
7Maskini huchukiwa na ndugu zake;
marafiki zake ndio zaidi: Humkimbia!
Hata awabembeleze namna gani hatawapata.19:7 Hata … hatawapata: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
8Ajipatiaye hekima anaipenda nafsi yake;
anayezingatia busara atastawi.
9Shahidi mwongo hatakosa kuadhibiwa;
asemaye uongo ataangamia.
10Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa,
tena ni vibaya zaidi mtumwa kuwatawala wakuu.
11Mwenye busara hakasiriki upesi;
kusamehe makosa ni fahari kwake.
12Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba,
lakini wema wake ni kama umande juu ya majani.
13Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake;
na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha.
14Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake,
lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
15Uzembe ni kama usingizi mzito;
mtu mvivu atateseka kwa njaa.
16Anayeshika amri anasalimisha maisha yake;
anayepuuza agizo atakufa.
17Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu;
Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema.
18Mrudi mwanao kungali bado na tumaini,
lakini usimwadhibu kiasi cha kumwangamiza.
19Mtu wa hasira kali lazima apate adhabu;
ukimwachia mara moja itakubidi kumwachia tena.19:19 ukimwachia … tena: Au ukimtoa kwenye matatizo hali yake huwa mbaya zaidi.
20Sikiliza shauri na kupokea mafundisho,
upate hekima ya kukufaa siku zijazo.
21Kichwani mwa mtu mna mipango mingi,
lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika.
22Kinachotakiwa kwa mtu ni uaminifu;
afadhali mtu maskini kuliko mtu mwongo.
23Kumcha Mwenyezi-Mungu kunaleta uhai;
amchaye hujaliwa pumziko la kutosheleza,
wala hatapatwa na baa lolote.
24Mvivu ni kama mtu atiaye mkono katika sahani ya chakula,
lakini hana nguvu ya kuuinua hadi mdomoni.
25Mwadhibu mwenye mzaha naye mjinga atapata akili;
mwonye mwenye busara naye atapata maarifa.
26Anayemdhulumu baba yake na kumfukuza mama yake,
ni mtoto asiyefaa na mpotovu.
27Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,
utapotea mara mbali na maneno ya hekima.
28Shahidi asiyefaa kitu huidhihaki haki;
na kinywa cha mwovu hubugia uovu.
29Adhabu iko tayari kwa wenye mzaha,
mijeledi imetayarishwa kuchapa migongo ya wapumbavu.

Methali19;1-29

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: