Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 10 June 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Amosi 4...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Mbona mnanilalamikia? Nyinyi nyote mmeniasi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Niliwaadhibu watu wako bila kufanikiwa, wao wenyewe walikataa kukosolewa. Upanga wako uliwamaliza manabii wako kama simba mwenye uchu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Enyi watu! Sikilizeni ninachosema mimi Mwenyezi-Mungu: Je, nimekuwa jangwa kwa Israeli au nchi yenye giza nene? Kwa nini basi watu wangu waseme: ‘Sisi tu watu huru; hatutakuja kwako tena!’
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.

1Sikilizeni neno hili,
enyi wanawake ng'ombe wa Bashani
mlioko huko mlimani Samaria;
nyinyi mnaowaonea wanyonge,
mnaowakandamiza maskini,
na kuwaambia waume zenu:4:1 zenu: Au zao.
“Tuleteeni divai tunywe!”
Sikilizeni ujumbe huu:
2Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu Mtakatifu nimeapa:
“Tazama, siku zaja,
ambapo watu watawakokoteni kwa kulabu,
kila mmoja wenu kama samaki kwenye ndoana.
3Mtaburutwa hadi ukutani palipobomolewa,
na kutupwa nje.4:3 katika Kiebrania pameongezwa neno hapa ambalo maana yake si dhahiri.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
Israeli haijajirekebisha bado
4“Enyi Waisraeli,
nendeni basi huko Betheli mkaniasi!
Nendeni Gilgali mkalimbikize makosa yenu!
Toeni sadaka zenu kila asubuhi,
na zaka zenu kila siku ya tatu.
5Toeni tambiko ya shukrani ya mikate iliyochachushwa.
Tangazeni popote kwamba mmetoa kwa hiari;
kwani ndivyo mnavyopenda kufanya!
Mimi Bwana Mungu nimenena.
6“Mimi niliwanyima chochote cha kutafuna,
nikasababisha ukosefu wa chakula popote.
Hata hivyo hamkunirudia.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
7“Tena niliwanyima mvua
miezi mitatu tu kabla ya mavuno.
Niliunyeshea mvua mji mmoja,
na mji mwingine nikaunyima.
Shamba moja lilipata mvua,
na lingine halikupata, likakauka.
8Watu wa miji miwili, mitatu wakakimbilia mji mwingine,
wapate maji, lakini hayakuwatosha.
Hata hivyo hamkunirudia.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
9“Niliwapiga pigo la ukame na ukungu;
nikakausha bustani na mashamba yenu ya mizabibu;
nzige wakala mitini na mizeituni yenu.
Hata hivyo hamkunirudia.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
10“Niliwaleteeni ugonjwa wa tauni
kama ule nilioupelekea Misri.
Niliwaua vijana wenu vitani,
nikawachukua farasi wenu wa vita.
Maiti zilijaa katika kambi zenu,
uvundo wake ukajaa katika pua zenu.
Hata hivyo hamkunirudia.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
11“Niliwaangusha baadhi yenu kwa maangamizi
kama nilivyoangamiza Sodoma na Gomora.
Wale walionusurika miongoni mwenu,
walikuwa kama kijiti kilichookolewa motoni.
Hata hivyo hamkunirudia.
Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
12“Kwa hiyo, enyi Waisraeli, nitawaadhibu.
Na kwa kuwa nitafanya jambo hilo,
kaeni tayari kuikabili hukumu yangu!”
13Mungu ndiye aliyeifanya milima,
na kuumba upepo;
ndiye amjulishaye mwanadamu mawazo yake;
ndiye ageuzaye mchana kuwa usiku,
na kukanyaga vilele vya dunia.
Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lake!

Amosi4;1-13

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: