Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 31 March 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 30...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Filipo akamwambia, “Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka.” Yesu akamwambia, “Nimekaa nanyi muda wote huu, nawe Filipo hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: ‘Tuoneshe Baba?’
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake. Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, kwani ninakwenda kwa Baba. Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Mwenyezi-Mungu ataiadhibu Misri
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Toa unabii useme kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Ombolezeni na kusema: ‘Ole wetu siku ile!’
3Kwa maana, siku hiyo imekaribia;
siku ile ya Mwenyezi-Mungu iko karibu.
Hiyo itakuwa siku ya mawingu,
siku ya maangamizi kwa mataifa.
4Vita vitazuka dhidi ya Misri,
na wasiwasi mkuu utaikumba nchi ya Kushi,
wakati Wamisri wengi wataanguka wameuawa,
mali zao zitakapochukuliwa,
na misingi ya miji yao kubomolewa.
5“Watu wote waliofungamana na Wamisri, yaani watu wa Kushi, Puti, Ludi, Arabia yote na Libia wataangamia pamoja nao.
6“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Wote wanaoiunga mkono Misri wataangamia,
mashujaa wake wenye fahari wataangamizwa,
tangu Migdoli mpaka Syene watu watauawa vitani.
Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
7Misri itakuwa jangwa kama nchi zilizo jangwa
na miji yake itakuwa magofu kama miji iliyoteketezwa.
8Nitakapoiteketeza Misri kwa moto
na kuwavunjilia mbali wasaidizi wake wote
ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
9Siku hiyo, nitapeleka wajumbe kwenda kuwatisha
Waethiopia wanaojidhani kuwa salama.
Watatetemeka siku Misri itakapoangamia.
Naam! Kweli siku hiyo yaja!
10“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Nitamtumia Nebukadneza, mfalme wa Babuloni,
kukomesha utajiri wa nchi ya Misri.
11Nebukadneza mwenyewe pamoja na watu wake,
taifa katili kuliko mataifa yote,
watatumwa kuiangamiza nchi ya Misri.
Watachomoa panga zao dhidi ya Misri
na kuijaza nchi hiyo watu waliouawa.
12Nitaukausha mto Nili na vijito vyake,
na kuwauzia watu waovu nchi ya Misri.
Nitasababisha uharibifu nchini kote
kwa mkono wa watu wageni.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
13“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Nitaharibu vinyago vya miungu,
na kukomesha sanamu mjini Memfisi.
Hakutakuwa na mkuu tena huko Misri.
Nitasababisha hofu itawale nchini Misri.
14Mji wa Pathrosi nitaufanya kuwa mtupu,
mji wa Soani nitauwasha moto,
mji wa Thebesi nitauadhibu.
15Nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu,
ile ngome inayotegemewa na Misri;
na kuangamiza makundi ya Thebesi.
16Nitaiwasha moto nchi ya Misri.
Pelusiumu utashikwa na dhiki kubwa,
ukuta wa Thebesi utabomolewa,30:16 ukuta … utabomolewa: Makala ya Kiebrania si dhahiri.
nao Memfisi utakabiliwa na adui mchana wazi.
17Vijana wanaume wa Oni na Pi-besethi watauawa kwa upanga,
na wakazi wengine watachukuliwa uhamishoni.
18Huko Tahpanesi mchana utakuwa giza
wakati nitavunja mamlaka ya Misri
na kiburi chake kikuu kukomeshwa.
Wingu litaifunika nchi ya Misri
na watu wake watachukuliwa mateka.
19Ndivyo nitakavyoiadhibu Misri.
Na watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Kuvunjwa kwa nguvu za Misri
20Siku ya saba ya mwezi wa kwanza, mwaka wa kumi na moja tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 21“Wewe mtu! Nimeuvunja mkono wa Farao mfalme wa Misri, nao haukufungwa ili uweze kupona na kuweza kushika upanga. 22Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitapambana na Farao mfalme wa Misri. Nitaivunja mikono yake yote miwili, ule mzima na hata uliovunjika. Na upanga ulio mkononi mwake utaanguka chini. 23Nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa na kuwasambaza katika nchi nyingine. 24Mikono ya mfalme wa Babuloni nitaitia nguvu na kutia upanga wangu mkononi mwake. Lakini nitaivunja mikono ya Farao, naye atapiga kite mbele ya mfalme wa Babuloni kama mtu aliyejeruhiwa vibaya sana. 25Mikono ya mfalme wa Babuloni nitaiimarisha, lakini mikono ya Farao italegea. Hapo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. Nitakapotia upanga wangu mkononi mwa mfalme wa Babuloni, ataunyosha dhidi ya nchi ya Misri, 26nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”


Ezekieli30;1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: