Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 30 March 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 29...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki/nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...


Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Yesu aliwaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....
Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi. Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda.”

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...
Thoma akamwuliza, “Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?” Yesu akamjibu, “Mimi ni njia, na ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu. Ikiwa mnanijua mimi, mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona.”
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.




Unabii dhidi ya Misri
1Siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Mgeukie Farao mfalme wa Misri, utoe unabii juu yake na nchi yote ya Misri. 3Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Mimi nitapambana na wewe mfalme wa Misri,
wewe mamba ulalaye mtoni Nili!
Wewe unafikiri kwamba Nili ni wako,
kwamba wewe ndiwe uliyeufanya!
4Basi, nitakutia ndoana tayani mwako,
na kufanya samaki wakwame magambani mwako.
Nitakuvua kutoka huko mtoni.
5Nitakutupa jangwani,
wewe na samaki hao wote.
Mwili wako utaanguka mbugani;
wala hakuna atakayekuokota akuzike.
Nimeutoa mwili wako
uwe chakula cha wanyama wakali na ndege.
6 29:6 Taz Isa 36:6 Hapo ndipo wakazi wote wa Misri watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
“Waisraeli walikutegemea wewe ee Misri, lakini umekuwa dhaifu kama utete. 7Walipokushika kwa mkono, ulivunjika na kutegua mabega yao. Walipokuegemea ulivunjika na kutetemesha viungo vyao. 8Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitazusha upanga dhidi yako na kuwaua watu na wanyama wako wote. 9Kwa sababu umesema kuwa mto Nili ni wako, kwamba ndiwe uliyeufanya, basi, nchi yako, Misri, itakuwa tupu na jangwa. Ndipo watu watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. 10Hakika nitakuadhibu wewe na mito yako; kwa hiyo nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na tupu toka Migdoli mpaka Syene hadi mipakani mwa Kushi. 11Hakuna mtu wala mnyama atakayepita huko. Haitakaliwa kwa muda wa miaka arubaini. 12Kati ya miji yote iliyoharibiwa, miji ya Misri itakuwa mitupu kwa miaka arubaini. Nitawatawanya Wamisri kati ya watu wa mataifa mengine na kuwasambaza katika nchi nyingine.
13“Lakini mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Baada ya miaka arubaini nitawakusanya Wamisri kutoka kwa mataifa walimotawanywa. 14Nitawafanikisha tena Wamisri. Nitawarudisha katika nchi ya Pathrosi, nchi yao ya asili. Huko watakuwa na ufalme usio na nguvu, 15ufalme dhaifu kuliko falme zote; wala hawataweza kujikuza juu ya mataifa mengine. Nitawafanya Wamisri wawe watu dhaifu hata wasiweze kuyatawala mataifa mengine tena. 16Misri haitakuwa tena na nguvu za kuweza kutegemewa na watu wa Israeli. Waisraeli watakumbuka jinsi walivyokosa kwa kutegemea nchi ya Misri. Waisraeli watatambua kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.”
Mfalme Nebukadneza ataishinda Misri
17Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, mwaka wa ishirini na saba tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 18“Wewe mtu! Nebukadneza,29:18 Nebukadneza: Au Nebukadreza. mfalme wa Babuloni, alilipa jeshi lake jukumu gumu la kuishambulia Tiro. Vichwa vyote vya wanajeshi wake vilipata upara na mabega yote yalichubuka. Lakini yeye, wala jeshi lake, hawakuambulia chochote kutokana na uvamizi huo alioufanya dhidi ya Tiro. 19Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitampa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, nchi ya Misri. Ataipora mali yake yote, na kuchukua utajiri wa Misri kuwa ujira wa jeshi lake. 20Nimempa nchi ya Misri kuwa ujira wa jasho lake kwa kuwa majeshi yake yalifanya kazi kwa ajili yangu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. 21Siku hiyo, nitawafanya Waisraeli wawe na nguvu na kukuwezesha wewe Ezekieli uongee miongoni mwao. Nao watapata kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”



Ezekieli29;1-21

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: