Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 26 March 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 27...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ndugu, tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana. Ndio maana sisi tunajivunia nyinyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake, nyinyi mtastahili ufalme wake ambao kwa ajili yake mnateseka. Mungu atafanya jambo la haki: Atawalipa mateso wale wanaowatesa nyinyi na kuwapeni nafuu nyinyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake wenye nguvu na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Maombolezo juu ya Tiro
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Sasa ewe mtu, imba utenzi huu wa maombolezo juu ya mji wa Tiro, 3mji ule kando ya bahari, unaofanya biashara na mataifa ya pwani. Uambie: Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
Ewe Tiro, wewe umejigamba
u mzuri kwelikweli!
4Mipaka yako imeenea kwelikweli!
Umejengwa kama meli nzuri.
5Wajenzi wako walitumia misonobari kutoka Seniri
kupasua mbao zako zote;
walichukua mierezi kutoka Lebanoni
kukutengenezea mlingoti.
6Walichukua mialoni toka Bashani
wakakuchongea makasia yako;
walikitengenezea silaha
kwa misonobari ya kisiwa cha Kupro,
na kuipamba kwa pembe.
7Kitani kilichotariziwa kutoka Misri
kilikuwa kwa kupamba tanga lako
na kwa ajili ya bendera yako.
Chandarua chako kilitengenezwa
kwa rangi ya samawati na urujuani
kutoka visiwa vya Elisha.
8Watu wa Sidoni na Arvadi
walikuwa wapiga makasia wako.
Wenye hekima wako walikuwa ndani
wakifanya kazi kama wanamaji.
9Wazee wa Gebali na mafundi wao
walikuwa kwako kuziba nyufa zako.
Mabaharia waliokuwa wakipitia kwako
walifanya biashara nawe.
10Watu kutoka Persia, Ludi na Puti
walijiunga katika jeshi lako;
walirundika kwenye kambi zao za jeshi
ngao zao na kofia zao.
Wanajeshi hao walikupatia fahari.
11Watu wa Arvadi na wa Hele na jeshi lao walilinda kuta zako pande zote, nao watu wa Gamadi walilinda minara yako. Walitundika ngao zao kwenye kuta zako pande zote, na hivyo wakaukamilisha uzuri wako. 12Watu wa Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mwingi na wa kila namna. Walitoa fedha, chuma, bati, na risasi kupata bidhaa zako. 13Watu wa Yavani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, wakakupatia watumwa na vifaa vya shaba wapate bidhaa zako. 14Bidhaa zako uliziuza huko Beth-togarma ili kujipatia farasi wa mizigo na wa vita, ngamia na nyumbu. 15Watu wa Dedani27:15 Dedani: Tafsiri ya Kigiriki ni Rode. walifanya biashara nawe. Nchi nyingi za pwani zilikuwa masoko yako maalumu. Watu wake walikuletea pembe za ndovu na mipingo kulipia bidhaa zako. 16Watu wa Edomu27:16 Edomu: Hati nyingine: Aramu. walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako. Kwa kupata bidhaa zako walikupa akiki, vitambaa vya urujuani, vitambaa vilivyonakshiwa, kitani safi, matumbawe na yakuti. 17Hata watu wa Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walikupa ngano,27:17 makala ya Kiebrania ina maneno mawili yasiyoeleweka. zeituni, tini za mwanzoni, asali, mafuta na marhamu kulipia bidhaa zako. 18Watu wa Damasko walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako; walikupa divai kutoka Helboni na sufu nyeupe. 19Vedani na Yavani walisafirisha bidhaa zako toka Uzali; hata chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai ili kupata bidhaa zako. 20Watu wa Dedani walifanya biashara nawe kwa kukupatia matandiko ya farasi. 21Waarabu na wakuu wote wa nchi ya Kedari walikuwa wachuuzi wako wakuu katika biashara ya wanakondoo, kondoo madume na mbuzi. 22Wachuuzi wa Sheba na wa Rama walifanya biashara nawe; walikuletea viungo vya chakula, vito vya thamani na dhahabu kujipatia bidhaa zako safi. 23Wakazi wa miji ya Harani, Kane na Edeni na wachuuzi wa Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. 24Hao walifanya nawe biashara ya mavazi ya fahari, nguo za buluu zilizotariziwa, mazulia ya rangi angavu vifundo na kamba zilizosokotwa imara. 2527:25-36 Taz Ufu 18:11-19 Merikebu za Tarshishi ndizo zilikusafirishia bidhaa zako.
Basi kama meli katikati ya bahari
wewe ulikuwa umejaa shehena.
26Wapiga makasia wako walikupeleka mbali baharini.
Upepo wa mashariki umekuvunjavunja
ukiwa mbali katikati ya bahari.
27Utajiri wako wa bidhaa na mali,
wanamaji wako wote chomboni,
mafundi wako wa meli na wachuuzi wako,
askari wako wote walioko kwako,
pamoja na wasafiri walioko kwako,
wote wataangamia baharini,
siku ile ya kuangamizwa kwako.
28Mlio wa mabaharia wako utakaposikika,
nchi za pwani zitatetemeka.
29Hapo wapiga makasia wote
wataziacha meli zao.
Wanamaji na manahodha watakaa pwani.
30Wataomboleza kwa uchungu wa moyo juu yako,
na kulia kwa uchungu mkubwa;
watajitupia mavumbi vichwani mwao
na kugaagaa kwenye majivu.
31Wamejinyoa vichwa kwa ajili yako
na kuvaa mavazi ya gunia.
Watalia kwa uchungu wa moyo juu yako.
32Wataimba wimbo wa ombolezo juu yako;
‘Nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro
katikati ya bahari?’
33Bidhaa zako zilipowasili nchi za ngambo,
ulitosheleza mahitaji ya watu wengi!
Kwa wingi wa utajiri wa bidhaa zako
uliwatajirisha wafalme wa dunia.
34Lakini sasa umevunjikia baharini;
umeangamia katika vilindi vya maji.
Shehena yako na jamii ya mabaharia
vimezama pamoja nawe.
35Wakazi wote wa visiwani
wamepigwa na bumbuazi juu yako;
wafalme wao wameogopa kupindukia,
nyuso zimekunjamana kwa huzuni.
36Wachuuzi wa mataifa watakufyonya!
Umeufikia mwisho wa kutisha,
na hutakuwapo tena milele!”



Ezekieli27;1-36

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: