Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 25 March 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 26...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo. Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo.
Wafilipi 3:17-18 
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
Tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema

ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.

Unabii juu ya Tiro
1Mnamo siku ya kwanza ya mwezi, mwaka wa kumi na moja tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Watu wa Tiro wameucheka mji wa Yerusalemu na kusema: ‘Aha! Yerusalemu mji ambao watu wote walipita, umeangamizwa! Sasa umetuachia nafasi; utajiri wake26:2 utajiri wake: Kiebrania: Nitakuwa tajiri. umeharibiwa!’ 3Basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Sasa nitapambana nawe ewe Tiro. Nitazusha mataifa mengi dhidi yako, nao watakuja kama mawimbi ya bahari. 4Wataziharibu kuta zako na kuibomoa minara yako. Nitafagilia mbali udongo wako na kukufanya kuwa jabali tupu. 5Utakuwa mahali pakavu katikati ya bahari, na wavuvi watakausha nyavu zao hapo; mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mataifa yatakuteka nyara, 6na miji iliyo jirani nawe huko bara itaangamizwa. Nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu
7“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kutoka kaskazini nitamleta Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, mfalme wa wafalme, akiwa na farasi, magari ya vita, wapandafarasi na jeshi kubwa, aje kukushambulia. 8Ataiangamiza miji iliyo jirani nawe huko bara. Kisha atajenga kuta za kukushambulia, atajaza udongo kwenye kuta zako na kuweka ukuta wenye ngao ili kukushambulia. 9Ataweka magogo yake ya kubomolea mbele ya kuta zako, na kwa mitalimbo ataivunjilia mbali minara yako. 10Farasi wa mfalme Nebukadneza ni wengi na vumbi watakalotimua litakufunika. Kuta zako zitatetemeka kwa mshindo wa wapandafarasi na magari ya vita na ya mizigo wakati atakapoingia kwenye malango yako kama watu waingiavyo mjini kupitia mahali palipobomolewa. 11Kwa kwato za farasi wake, ataikanyaga mitaa yako yote. Atawaua watu wako kwa panga; minara yako mikubwa ataiangusha chini. 12Utajiri wako watauteka pamoja na bidhaa zako. Watazibomoa kuta zako na kuziangusha nyumba zako za fahari; mawe, mbao na udongo ulivyotumia kujengea nyumba hizo watavitupa baharini. 13Nitakomesha muziki wa nyimbo zako. Sauti za vinubi vyako hazitasikika tena. 14Nitakufanya kuwa jabali tupu; utakuwa mahali pa wavuvi kukaushia nyavu zao, wala hutajengwa tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
15“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi wewe Tiro: Wakazi wa sehemu za pwani watatetemeka watakaposikia kishindo cha kuanguka kwako na mlio wa majeruhi na wa watu wanaouawa. 1626:16-18 Taz Ufu 18:9-10 Wakuu wote wa mataifa ya pwani watashuka toka viti vyao vya enzi, na kuvua mavazi yao ya heshima pamoja na nguo zao zilizotariziwa. Wakiwa wamejaa hofu, wataketi chini; nao watatetemeka wakati wote na kushangaa mno juu ya hayo yaliyokupata. 17Wataimba utenzi huu wa kuomboleza:
Umeangamizwa wewe mji maarufu,
umetoweka kutoka baharini!
Wakazi wake walieneza nguvu zao juu ya bahari,
ambapo walihofiwa na wote.
18Sasa watu wa bara wanatetemeka
kwa sababu ya kuanguka kwake;
wakazi wa pwani, wametishika kwa kutoweka kwako!
19“Maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitakufanya wewe Tiro kuwa mahame, kama miji isiyo na watu, nitakapoleta juu yako maji kutoka vilindi vya bahari, na maji mengi yatakufunika. 20Nitakuteremsha shimoni ili ujiunge na walioko huko, walioishi duniani zamani; nitakufanya ukae huko katika mahame milele. Hutakaliwa na watu milele na hutakuwa na nafasi miongoni mwa nchi za walio hai. 2126:21 Taz Ufu 18:21 Nitakufanya kuwa kitisho wala hutakuwapo tena; watu watakutafuta, lakini hawatakupata tena. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”


Ezekieli26;1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: