Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 18 March 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 21...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: Tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, nyinyi mliusikia, mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu nyinyi mnaoamini.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
Tukijishusha  na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 

Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Ndugu, nyinyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Nyinyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi,
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni maadui za kila mtu! Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



Upanga wa Mwenyezi-Mungu
1 21:1 makala ya Kiebrania sura ya 21:6.Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu, ugeukie mji wa Yerusalemu, uhubiri dhidi ya sehemu zake za ibada, na kutoa unabii juu ya nchi ya Israeli. 3Waambie Waisraeli kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe naja kupambana nanyi. Nitauchomoa upanga wangu alani mwake na kuwaua watu wema na wabaya. 4Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu. 5Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani.
6“Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao. 7Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
8Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 9“Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi:
Upanga! Naam, upanga umenolewa,
nao umengarishwa pia.
10Umenolewa ili ufanye mauaji,
umengarishwa umetamete kama umeme!21:10 katika makala ya Kiebrania maneno yaliyobaki hayaeleweki.
11Umenolewa na kungarishwa
uwekwe mkononi mwa mwuaji.
12Wewe mtu, lia na kuomboleza
upanga huo umenyoshwa dhidi ya watu wangu,
dhidi ya wakuu wote wa Israeli.
Wataangamizwa kwa upanga pamoja na watu wangu.
Jipige kifua kwa huzuni.
13Hilo litakuwa jaribio gumu sana.21:13 Baada ya neno jaribio gumu tafsiri hii imeacha maneno kadhaa yasiyoeleweka, ambayo neno kwa neno ni: Itakuwaje kama hakuna fimbo ya kudharauliwa? Taz mwisho wa aya 15 ambayo nayo maana yake si dhahiri.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
14Wewe mtu, tabiri!
Piga makofi,
upanga na ufanye kazi yake,
mara mbili, mara tatu.
Huo ni upanga wa mauaji
nao unawazunguka.
15Kwa hiyo wamekufa moyo
na wengi wanaanguka.
Ncha ya upanga nimeiweka katika malango yao yote.
Umefanywa ungae kama umeme,
umengarishwa kwa ajili ya mauaji.
16Ewe upanga, shambulia kulia, shambulia kushoto;
elekeza ncha yako pande zote.
17Nami nitapiga makofi,
nitatosheleza ghadhabu yangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Uamuzi wa Yerusalemu
18Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 19“Wewe mtu! Chora njia mbili ambapo utapitia upanga wa mfalme wa Babuloni. Njia zote mbili zianzie katika nchi moja. Mwanzoni mwa kila njia utaweka alama ya kuonesha upande mji uliko. 20Utachora njia upanga utakapopitia kwenda kuufikilia mji wa Raba wa Waamoni, na njia nyingine inayoelekea mji wenye ngome wa Yerusalemu nchini Yuda. 21Mfalme wa Babuloni anasimama mwanzoni mwa hizo njia mbili, kwenye njia panda, apate kupiga bao. Anatikisa mishale, anaviuliza shauri vinyago vya miungu yake na kuchunguza maini ya mnyama.21:21 maini ya mnyama: Hapa Ezekieli anatuhabarisha baadhi ya njia za kupiga bao: Mishale miwili iliyotiwa alama tofauti ilitikiswa podoni na wa kwanza kutolewa ulitoa jibu. Vile vile watu walichunguza kufuatana na kanuni thabiti maini ya mnyama wa tambiko. 22Mshale unaodokezea ‘Yerusalemu’ umeangukia mkono wake wa kulia. Anaweka zana za kubomolea, anaamuru mauaji na kelele za vita zifanywe, zana za kubomolea malango zimewekwa, maboma na minara ya kuuzingira mji vimewekwa. 23Lakini watu wa Yerusalemu wataudhania kuwa ni utabiri wa uongo kwa sababu wamekula kiapo rasmi. Hata hivyo unabii huu utawakumbusha uovu wao na kusababishwa kukamatwa kwao. 24Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wote wataweza kuziona dhambi zenu. Kila mtu atajua jinsi mlivyo na hatia. Kila kitendo mnachotenda kinaonesha dhambi zenu. Nyinyi mmehukumiwa adhabu nami nitawatia mikononi mwa maadui zenu.
25“Nawe mtawala wa Israeli wewe ni mpotovu kabisa. Siku yako imefika, naam, siku ya adhabu yako ya mwisho. 26Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuambia hivi: Vua kilemba chako na taji yako kwani mambo hayatabaki kama yalivyokuwa. Walio chini watakwezwa, walio juu watashushwa! 27Uharibifu! Uharibifu! Hamna chochote katika mji huu nitakachosaza. Lakini kabla ya hayo atakuja yule ambaye nimempa mamlaka ya kuuadhibu, ambaye mimi nitampa mji huo.
Adhabu ya Waamoni
28“Ewe mtu, tabiri kuhusu Waamoni na maneno yao ya dhihaka kwa Waisraeli: Waambie kuwa nasema:
Upanga, upanga!
Upanga umenyoshwa kuua,
umenolewa uangamize,
umengarishwa ungae kama umeme.
29Wakati nyinyi mmetulia katika maono yenu madanganyifu na utabiri wenu wa uongo, upanga utakuwa tayari kukata shingo za waasi na waovu. Siku imewadia ambapo maovu yenu yataadhibiwa.
30“Sasa rudisha upanga alani mwake! Nitawahukumu mahali palepale mlipoumbwa, katika nchi mlipozaliwa. 31Nitawamwagia ghadhabu yangu. Moto wa ghadhabu yangu nitaupuliza juu yenu. Nitawatia mikononi mwa watu wakatili, watu hodari wa kuangamiza. 32Mtakuwa kuni motoni, damu yenu itamwagika katika nchi. Mtu hatawakumbuka tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Ezekieli21;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: