Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 24 March 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 25...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Unabii dhidi ya Amoni
1 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Wageukie Waamoni, ukatoe unabii dhidi yao. 3Waambie Waamoni: Sikilizeni neno la Bwana Mwenyezi-Mungu: Nyinyi mlifurahia kuona maskani yangu ikitiwa unajisi, nchi ya Israeli ikiangamizwa na watu wa Yuda wakipelekwa uhamishoni. 4Basi, nitawatia nyinyi mikononi mwa watu wa mashariki; watapiga hema zao kati yenu na kufanya makazi yao katika nchi yenu. Nao watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. 5Mji wa Raba nitaufanya kuwa malisho ya ngamia na nchi ya Amoni zizi la kondoo. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
6“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu mlipiga makofi, mkarukaruka kwa furaha na kushangilia sana juu ya nchi ya Israeli, 7basi, mimi nimeunyosha mkono dhidi yenu; nitawaacha mtekwe nyara na watu wa mataifa mengine. Nitawaangamizeni, nanyi hamtakuwa taifa tena wala kuwa na nchi. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Unabii dhidi ya Moabu
8Bwana Mwenyezi-Mungu alisema: “Kwa kuwa Moabu imesema kuwa Yuda ni sawa tu na mataifa mengine, 9mimi nitaifanya miji inayolinda mipaka ya Moabu ishambuliwe, hata miji ile bora kabisa, yaani Beth-yeshimothi, Baal-meoni na Kiriathaimu. 10Nitaitia nchi hiyo pamoja na nchi ya Amoni mikononi mwa watu wa mashariki iwe mali yao. Nchi ya Moabu25:10 makala ya Kiebrania ni: Amoni. haitakuwa taifa tena. 11Mimi nitaiadhibu nchi ya Moabu, nao watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
Unabii dhidi ya Edomu
12 Bwana Mwenyezi-Mungu alisema hivi: “Kwa kuwa Waedomu wamefanya kisasi na Yuda, wakawalipiza watu wa Yuda kisasi kibaya sana 13basi, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Nitanyosha mkono dhidi ya nchi ya Edomu na kuwaua watu wote na wanyama. Nitaifanya kuwa ukiwa kutoka mji wa Temani hadi mji wa Dedani, watu watauawa kwa upanga. 14Nitawafanya watu wangu Israeli walipize kisasi juu ya Waedomu nao watawatenda Waedomu kadiri ya hasira na ghadhabu yangu. Ndipo Waedomu watakapotambua uzito wa kisasi changu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.”
Unabii juu ya Filistia
15Bwana Mwenyezi-Mungu alisema hivi: “Kwa kuwa Wafilisti walifanya kisasi, wakawalipiza kisasi adui zao kwa ubaya sana na kuendelea kuwa maadui zao daima, 16basi, mimi Mwenyezi-Mungu nitanyosha mkono dhidi ya Wafilisti; nitawaangamiza hao Wakerethi na wakazi wa pwani. 17Nitawalipiza kisasi kikali kwa adhabu ya ghadhabu. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”


Ezekieli25;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: