Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 11 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 8....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane. Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa. Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka. Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



1“Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, mifupa ya wafalme wa Yuda, mifupa ya wakuu wao, mifupa ya makuhani, mifupa ya manabii na mifupa ya wakazi wote wa Yerusalemu itachimbuliwa makaburini mwao. 2Itaachwa imetandazwa mbele ya jua na mwezi na sayari zote za mbinguni, vitu ambavyo walivipenda na kuvitumikia, wakavitaka shauri na kuviabudu. Mifupa hiyo haitakusanywa wala kuzikwa, bali itakuwa kama mavi juu ya ardhi. 3Watu wote waliobaki wa jamaa hii mbovu, mahali popote pale nilipowatawanya, wataona heri kufa kuliko kuishi. Ndivyo nisemavyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
Dhambi na adhabu
4“Wewe Yeremia utawaambia
kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Mtu akianguka, je hainuki tena?
Mtu akipotea, je, hairudii tena njia yake?
5Mbona basi, watu hawa wameacha njia iliyo sawa
na kuendelea katika upotovu wao?
Wanashikilia miungu yao ya uongo,
na kukataa kunirudia mimi!
6Mimi nilisikiliza kwa makini,
lakini wao hawakusema ukweli wowote.
Hakuna mtu anayetubu uovu wake,
wala kujiuliza; ‘Nimefanya nini?’
Kila mmoja wao anashika njia yake,
kama farasi akimbiliavyo moja kwa moja vitani.
7Hata korongo anajua wakati wa kuhama;
njiwa, mbayuwayu na koikoi,
hufuata majira yao ya kurudi.
Lakini watu wangu hawa hawajui kitu
juu ya amri zangu mimi Mwenyezi-Mungu.
8Mnawezaje kusema: ‘Sisi tuna hekima,
sisi tunayo sheria ya Mwenyezi-Mungu,’
hali waandishi wa sheria,
wameipotosha sheria yangu?
9Wenye hekima wenu wataaibishwa;
watafadhaishwa na kunaswa.
Wamelikataa neno la Mwenyezi-Mungu;
je, ni hekima gani hiyo waliyo nayo?
10Kwa hiyo, wake zao nitawapa watu wengine,
mashamba yao nitawapa wengine.
Maana, tangu mdogo hadi mkubwa,
kila mmoja ana tamaa ya faida haramu.
Tangu manabii hadi makuhani,
kila mmoja anatenda kwa udanganyifu.
11Wameliponya jeraha la watu wangu juujuu,
wakisema, ‘Kuna amani, kuna amani’,
kumbe hakuna amani yoyote!
12Je, waliona aibu walipotenda machukizo hayo?
La hasha! Hawakuona aibu hata kidogo.
Hata hawajui kuona haya.
Kwa hiyo, wataanguka pamoja na wale walioanguka;
nitakapowaadhibu, wataangamia.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
13“Mimi Mwenyezi-Mungu nasema:
Nilipotaka kukusanya chochote kutoka kwao,
sikupata zabibu hata moja juu ya mzabibu,
sikupata tini zozote juu ya mtini;
hata majani yao yamekauka.
Hata nilichokuwa nimewapa kimetoweka.”8:13 nimewapa … kimetoweka: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
14“Watu wanauliza: Kwa nini sisi tunakaa tu hapa?
Kusanyikeni, tuingie katika miji yenye ngome,
tukaangamie huko!
Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametupangia tuangamie,
ametupa maji yenye sumu tunywe,
kwa kuwa tumemkosea yeye.
15Tulitazamia kupata amani,
lakini hakuna jema lililotokea.
Tulitazamia wakati wa kuponywa,
badala yake tukapata vitisho.
16Sauti za farasi wao zinasikika,
kwa mlio wa farasi wao wa vita,
nchi nzima inatetemeka.
Wanafika na kuiharibu nchi na vyote vilivyomo,
kuangamiza mji pamoja na wote waishio humo.
(Mwenyezi-Mungu)
17“Basi nitawaleteeni nyoka;
nyoka wenye sumu wasioweza kurogwa na walozi,
nao watawauma nyinyi.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Huzuni ya Yeremia
18Huzuni yangu haiwezi kutulizwa,8:18 huzuni … kutulizwa: Maana katika Kiebrania si dhahiri.
moyo wangu wasononeka ndani yangu.
19Sikiliza kilio cha watu wangu,
kutoka kila upande katika nchi.
“Je, Mwenyezi-Mungu hayuko Siyoni?
Je, mfalme wake hayuko tena huko?”
(Mwenyezi-Mungu)
“Mbona wamenikasirisha kwa sanamu zao za miungu,
na vinyago vyao vya miungu ya kigeni?”
(Yeremia)
20“Mavuno yamepita, kiangazi kimekwisha,
nasi bado hatujaokolewa!
21Jeraha la watu wangu limeniumiza moyoni,
ninaomboleza na kufadhaika.
22Je, hakuna dawa ya kupaka huko Gileadi?
Je, hakuna mganga huko?
Mbona basi watu wangu hawajaponywa?


Yeremia8;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: