Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 5 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 4....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Huyo mama akamwambia, “Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu.” Yesu akamwambia, “Mimi ninayeongea nawe, ndiye.” Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu, “Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?” Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, kula chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua nyinyi.” Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?” Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Wito wa toba
1Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Ukitaka kurudi ee Israeli, nirudie mimi.
Ukiviondoa vitu vya kuchukiza mbele yangu,
usipotangatanga huko na huko,
2ukiapa kwa ukweli, unyofu na uadilifu,
kwa kusema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo’,
ndipo mataifa yatakapopata baraka kwangu,
na kutukuka kwa sababu yangu.”
3Mwenyezi-Mungu awaambia hivi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu:
“Limeni mashamba yenu mapya;
msipande mbegu zenu penye miiba.
4Enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu,
jitakaseni kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu,
wekeni mioyo yenu wazi mbele yangu.4:4 wekeni … yangu: Kiebrania: Ondoeni govi za mioyo yenu.
La sivyo, ghadhabu yangu itachomoza kama moto,
iwake hata pasiwe na mtu wa kuizima,
kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
Yuda hatarini
5“Tangazeni huko Yuda,
pazeni sauti huko Yerusalemu!
Pigeni tarumbeta kila mahali nchini!
Pazeni sauti na kusema:
Kusanyikeni pamoja!
Kimbilieni miji yenye ngome!
6Twekeni bendera ya vita kuelekea Siyoni,
kimbilieni usalama wenu, msisitesite!
Mwenyezi-Mungu analeta maafa
na maangamizi makubwa kutoka kaskazini.
7Kama simba atokavyo mafichoni mwake,
mwangamizi wa mataifa ameanza kuja,
anakuja kutoka mahali pake,
ili kuiharibu nchi yako.
Miji yako itakuwa magofu matupu,
bila kukaliwa na mtu yeyote.
8Kwa hiyo, vaa vazi la gunia,
omboleza na kulia;
maana, hasira kali ya Mwenyezi-Mungu,
bado haijaondoka kwetu.
9Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku hiyo, mfalme na wakuu watakufa moyo; makuhani watapigwa na bumbuazi, na manabii watashangaa.” 10Kisha nikasema: “Aa, Mwenyezi-Mungu, hakika umewadanganya kabisa watu hawa na mji wa Yerusalemu! Uliwaambia mambo yatawaendea vema, kumbe maisha yao yamo hatarini kabisa!”
11Wakati huo, wataambiwa hivi watu hawa pamoja na mji wa Yerusalemu, “Upepo wa hari kutoka vilele vikavu vya jangwani utawavumia watu wangu. Huo si upepo wa kupepeta au kusafisha, 12bali ni upepo mkali sana utokao kwangu. Ni mimi Mwenyezi-Mungu nitakayetoa hukumu juu yao.”
Yuda imezingirwa na maadui
13Tazama! Adui anakuja kama mawingu.
Magari yake ya vita ni kama kimbunga,
na farasi wake waenda kasi kuliko tai.
Ole wetu! Tumeangamia!
14Yerusalemu, yasafishe maovu moyoni mwako,
ili upate kuokolewa.
Mpaka lini utaendelea kuwaza maovu?
15Sauti kutoka Dani inatoa taarifa;
inatangaza maafa kutoka vilima vya Efraimu.
16Inayaonya mataifa,
inaitangazia Yerusalemu:
“Wavamizi waja kutoka nchi ya mbali,
wanaitisha miji ya Yuda,
17wanauzingira Yerusalemu kama walinda mashamba,
kwa sababu watu wake wameniasi mimi Mwenyezi-Mungu.
18Yuda, mwenendo wako na matendo yako yamekuletea hayo.
Hayo ndiyo maafa yaliyokupata, tena ni machungu;
yamepenya mpaka ndani moyoni mwako.”
Yeremia awasikitikia watu wake
19Uchungu, uchungu!
Nagaagaa kwa uchungu!
Moyo wangu unanigonga vibaya.
Wala siwezi kukaa kimya.
Maana naogopa mlio wa tarumbeta,
nasikia kingora cha vita.
20Maafa baada ya maafa,
nchi yote imeharibiwa.
Ghafla makazi yangu yameharibiwa,
na hata mapazia yake kwa dakika moja.
21Hadi lini nitaona bendera ya vita
na kuisikia sauti ya tarumbeta?
22Mwenyezi-Mungu asema:
“Watu wangu ni wapumbavu,
hawanijui mimi.
Wao ni watoto wajinga;
hawaelewi kitu chochote.
Ni mabingwa sana wa kutenda maovu,
wala hawajui kutenda mema.”
Ono la Yeremia kuhusu maangamizi
23Niliiangalia nchi, lo! Imekuwa mahame na tupu;
nilizitazama mbingu, nazo hazikuwa na mwanga.
24Niliiangalia milima, lo, ilikuwa inatetemeka,
na vilima vyote vilikuwa vinayumbayumba.
25Nilikodoa macho wala sikuona mtu;
hata ndege angani walikuwa wametoweka.
26Niliona nchi yenye rutuba imekuwa jangwa,
na miji yake yote imekuwa magofu matupu,
kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi-Mungu.
27Maana Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Nchi nzima itakuwa jangwa tupu;
lakini sitaiharibu kabisa.
28Kwa hiyo, nchi itaomboleza,
na mbingu zitakuwa nyeusi.
Maana, nimetamka na sitabadili nia yangu;
nimeamua, wala sitarudi nyuma.
29Watakaposikika wapandafarasi na wapiga mishale,
kila mmoja atatimua mbio.
Baadhi yao watakimbilia msituni,
wengine watapanda majabali.
Kila mji utaachwa tupu;
hakuna mtu atakayekaa ndani.
30Nawe Yerusalemu uliyeachwa tupu,
unavalia nini mavazi mekundu?
Ya nini kujipamba kwa dhahabu,
na kujipaka wanja machoni?
Unajirembesha bure!
Wapenzi wako wanakudharau sana;
wanachotafuta ni kukuua.
31Nilisikia sauti kama ya mwanamke anayejifungua,
yowe kama anayejifungua mtoto wa kwanza.
Ilikuwa sauti ya Yerusalemu akitweta,
na kuinyosha mikono yake akisema,
‘Ole wangu!
Wanakuja kuniua!’”


Yeremia4;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: