Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 6 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 5....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Nyinyi mwasema: ‘Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!’ Lakini mimi nawaambieni, angalieni mkaone jinsi mashamba yalivyo tayari kuvunwa. Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uhai wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna.’ Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho; wengine walifanya kazi, lakini nyinyi mnafaidika kutokana na jasho lao.”
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza weweJehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Wasamaria wengi wa kijiji kile walimwamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.” Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. Watu wengi zaidi waliamini kwa sababu ya ujumbe wake. Wakamwambia yule mama, “Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu.”
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.


Dhambi ya Yerusalemu
1Kimbieni huko na huko mjini Yerusalemu;
pelelezeni na kujionea wenyewe!
Chunguzeni masoko yake
mwone kama kuna mtu atendaye haki
mtu atafutaye ukweli;
akiwako, basi Mwenyezi-Mungu atausamehe Yerusalemu.
2Ingawa wanaapa: “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo”,
viapo vyao ni vya uongo.
3Ee Mwenyezi-Mungu, wewe watafuta daima uaminifu.
Umewatwanga, lakini hawakuona uchungu;
umewateketeza, lakini walikataa kukosolewa.
Wamezifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba;
wamekataa kabisa kurudi kwako.
4Ndipo nilipowaza:
“Hawa ni watu duni hawana akili;
hawajui matakwa ya Mwenyezi-Mungu,
hawajui Sheria ya Mungu wao.
5Nitawaendea wakuu niongee nao;
bila shaka, wao wanajua matakwa ya Mwenyezi-Mungu;
wanajua sheria ya Mungu wao.”
Lakini wote waliivunja nira yao.
Waliikatilia mbali minyororo yao.
6Kwa hiyo simba kutoka msituni atawaua;
mbwamwitu kutoka jangwani atawararua.
Chui anaivizia miji yao.
Kila atokaye humo atararuliwa vipandevipande,
kwa sababu dhambi zao ni nyingi,
maasi yao ni makubwa.
7Mwenyezi-Mungu anauliza:
“Nitawezaje kukusamehe ee Yerusalemu?
Watu wako wameniasi;
wameapa kwa miungu ya uongo.
Nilipowashibisha kwa chakula,
wao walifanya uzinzi,
wakajumuika majumbani mwa makahaba.
8Walikuwa kama farasi walioshiba wenye tamaa,
kila mmoja akimtamani mke wa jirani yake.
9Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya yote?
Nisilipize kisasi juu ya taifa kama hili?
10“Pandeni mpite katika mashamba yake ya mizabibu
mkaharibu kila kitu bila kumaliza kabisa.
Yakateni matawi yake,
kwani hayo si yangu mimi Mwenyezi-Mungu.
11Naam, watu wa Israeli na watu wa Yuda,
wamekosa kabisa uaminifu kwangu.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Matokeo ya kuachwa na Mungu
12Wamesema uongo juu ya Mwenyezi-Mungu
wamesema: “Hatafanya kitu;
hatutapatwa na uovu wowote;
hatutashambuliwa wala kuona njaa.
13Manabii si kitu, ni upepo tu;
maana neno lake Mungu halimo ndani yao.”
Basi hayo na yawapate wao wenyewe!
14Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Kwa kuwa wao wamesema jambo hilo,
sasa nitayafanya maneno niliyokupa wewe Yeremia kuwa moto.
Watu hawa watakuwa kuni,
na moto huo utawateketeza.
15“Nami Mwenyezi-Mungu nasema juu yenu enyi Waisraeli:
Mimi naleta taifa moja kutoka mbali,
lije kuwashambulia.
Taifa ambalo halishindiki,
taifa ambalo ni la zamani,
ambalo lugha yake hamuifahamu,
wala hamwezi kuelewa wasemacho.
16Mishale yao husambaza kifo;
wote ni mashujaa wa vita.
17Watayala mazao yenu na chakula chenu;
watawamaliza watoto wenu wa kike na wa kiume.
Watachinja makundi yenu ya kondoo na ng'ombe;
wataiharibu mizabibu yenu na mitini yenu.
Miji yenu ya ngome mnayoitegemea,
wataiharibu kwa silaha zao.
18“Lakini, hata katika siku hizo mimi Mwenyezi-Mungu nasema, sitawaangamiza na kuwamaliza kabisa. 19Na watu wenu watakapouliza ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametutendea mambo hayo yote?’ Wewe utawaambia, ‘Nyinyi mlimwacha Mwenyezi-Mungu, mkaitumikia miungu ya kigeni katika nchi yenu. Basi ndivyo mtakavyowatumikia watu wengine katika nchi isiyo yenu.’
Mungu awaonya watu wake
20“Watangazie wazawa wa Yakobo,
waambie watu wa Yuda hivi:
21Sikilizeni enyi wajinga na wapumbavu;
watu mlio na macho, lakini hamwoni,
mlio na masikio, lakini hamsikii.
22Mbona hamniogopi? Nauliza mimi Mwenyezi-Mungu!
Kwa nini hamtetemeki mbele yangu?
Mimi niliweka mchanga uwe mpaka wa bahari,
kizuizi cha daima ambacho bahari haiwezi kuvuka.
Ingawa mawimbi yanaupiga, hayawezi kuupita;
ingawa yananguruma, hayawezi kuuruka.
23Lakini watu hawa wana moyo wa ukaidi na uasi;
wameniacha wakaenda zao.
24Wala hawasemi mioyoni mwao;
‘Na tumche Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,
anayetujalia mvua kwa wakati wake,
anayetupatia mvua za masika na mvua za vuli;
na kutupa majira maalumu ya mavuno.’
25Makosa yenu yamewazuia msipate baraka hizo,
dhambi zenu zimewafanya msipate mema.
26Naam, kuna walaghai miongoni mwa watu wangu,
watu ambao hunyakua mali za wengine.
Wako kama wawindaji wa ndege:
Hutega mitego yao na kuwanasa watu.
27Kama vile kapu lililojaa ndege walionaswa,
ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu.
Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri,
28wamenenepa na kunawiri.
Katika kutenda maovu hawana kikomo
hawahukumu yatima kwa haki wapate kufanikiwa,
wala hawatetei haki za watu maskini.
29“Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya?
Je nitaacha kulipiza kisasi taifa kama hili?
30Jambo la ajabu na la kuchukiza
limetokea katika nchi hii:
31Manabii wanatabiri mambo ya uongo,
makuhani nao hutafuta faida yao wenyewe;5:31 hutafuta faida yao wenyewe: Tafsiri ya maneno magumu na ya pekee ya Kiebrania.
na watu wangu wanaona jambo hilo kuwa sawa. Lakini mwisho utakapofika mtafanyaje?”

Yeremia5;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: