Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 9 December 2019

Kikombe Cha Asubuhi; Yeremia 6....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki
Nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu

Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, “Nabii hapati heshima katika nchi yake.” Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu. Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi. Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!” Huyo ofisa akamwambia, “Bwana, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao ataishi.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima. Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, “Jana saa saba mchana, homa ilimwacha.” Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: “Mwanao ataishi.” Hapo yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote. Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



Yerusalemu imezingirwa na maadui
1Enyi watu wa Benyamini,
ondokeni Yerusalemu mkimbilie usalama!
Pigeni tarumbeta mjini Tekoa;
onesheni ishara huko Beth-hakeremu,
maana maafa na maangamizi makubwa
yanakuja kutoka upande wa kaskazini.
2Mji wa Siyoni ni mzuri na mwororo,
lakini utaangamizwa.
3Watu wataujia kama wachungaji na makundi yao,
watapiga hema zao kuuzunguka kila mmoja sehemu yake,
wapate kuyaongoza makundi yao.
4Watasema: “Jitayarisheni kuushambulia Siyoni.
Haya! Tuanze kushambulia adhuhuri!
Bahati mbaya; jua linatua!
Kivuli cha jioni kinarefuka.
5Basi, tutaushambulia usiku;
tutayaharibu majumba yake ya kifalme.”
6Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema:
“Kateni miti yake,
rundikeni udongo kuuzingira Yerusalemu.
Mji huu ni lazima uadhibiwe,
maana hamna lolote ndani yake ila dhuluma.
7Kama kisima kinavyohifadhi maji yake yakabaki safi,
ndivyo Yerusalemu unavyohifadhi uovu wako.
Ukatili na uharibifu vyasikika ndani yake,
magonjwa na majeraha yake nayaona daima.
8Hilo na liwe onyo kwako ee Yerusalemu,
la sivyo nitakutupa kabisa kwa chuki;
nikakufanya uwe jangwa,
mahali pasipokaliwa na mtu.”
Watu wasiopenda kusikia
9Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Kusanyeni watu wote wa Israeli waliobaki
kama watu wakusanyavyo zabibu zote;
kama afanyavyo mchumazabibu,
pitisheni tena mikono yenu katika matawi yake.”
10Nitaongea na nani nipate kumwonya,
ili wapate kunisikia?
Tazama, masikio yao yameziba,6:10 yameziba: Kiebrania: Hayajatahiriwa.
hawawezi kusikia ujumbe wako.
Kwao neno lako, ee Mwenyezi-Mungu,
limekuwa jambo la dhihaka,
hawalifurahii hata kidogo.
11Nimejaa hasira ya Mwenyezi-Mungu dhidi yao.
Nashindwa kuizuia ndani yangu.
Mwenyezi-Mungu akaniambia:
“Imwage hasira barabarani juu ya watoto
na pia juu ya makundi ya vijana;
wote, mume na mke watachukuliwa,
kadhalika na wazee na wakongwe.
12Nyumba zao zitapewa watu wengine,
kadhalika na mashamba yao na wake zao;
maana nitaunyosha mkono wangu,
kuwaadhibu wakazi wa nchi hii.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
13Wote, tangu mdogo hadi mkubwa kabisa,
kila mmoja anatamani kupata faida isiyo halali.
Tangu manabii hadi makuhani,
kila mmoja wao ni mdanganyifu.
14Wameliponya jeraha la watu wangu juujuu,
wanasema; ‘Amani, amani’,
kumbe hakuna amani yoyote!
15Je, waliona aibu walipofanya machukizo hayo?
La! Hawakuona aibu hata kidogo.
Hawakujua hata namna ya kuona aibu.
Kwa hiyo wataanguka pamoja na wale waangukao;
wakati nitakapowaadhibu,
wataangamizwa kabisa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Israeli akataa njia ya Mungu
16Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Simameni katika njia panda, mtazame.
Ulizeni mjue juu ya matukio ya zamani.
Tafuteni mahali ilipo njia nzuri
muifuate nanyi mtapumzisha nafsi zenu.
Lakini wao wakasema:
‘Hatutafuata njia hiyo.’
17Kisha nikawawekea walinzi, nikawaambia:
‘Sikilizeni ishara ya tarumbeta.’
Lakini wao wakasema: ‘Hatutaisikiliza.’
18“Kwa hiyo, sikilizeni enyi mataifa;
enyi jumuiya ya watu jueni yatakayowapata.
19Sikiliza ee dunia!
Mimi nitawaletea maafa watu hawa
kulingana na nia zao mbaya.
Maana hawakuyajali maneno yangu,
na mafundisho yangu nayo wameyakataa.
20Ya nini kuniletea ubani kutoka Sheba,
na udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali?
Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliki,
wala tambiko zenu hazinipendezi.
21Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Tazama, nitawawekea watu hawa vikwazo
ambavyo vitawakwaza na kuwaangusha chini.
Akina baba na watoto wao wa kiume wataangamia,
kadhalika na majirani na marafiki.”
Mashambulizi kutoka kaskazini
22Mwenyezi-Mungu asema hivi:
“Tazameni, watu wanakuja toka nchi ya kaskazini;
taifa kubwa linajitayarisha kutoka mbali duniani.
23Wamezishika pinde zao na mikuki,
watu wakatili wasio na huruma.
Vishindo vyao ni kama ngurumo ya bahari.
Wamepanda farasi,
wamejipanga tayari kwa vita,
dhidi yako ewe Siyoni!”
24Waisraeli wanasema,
“Tumesikia habari zao,
mikono yetu imelegea;
tumeshikwa na dhiki na uchungu,
kama mwanamke anayejifungua.
25Hatuwezi kwenda mashambani,
wala kutembea barabarani;
maadui wameshika silaha mikononi,
vitisho vimejaa kila mahali.”
26Mwenyezi-Mungu asema,
“Jivikeni mavazi ya gunia, enyi watu wangu
na kugaagaa katika majivu.
Ombolezeni kwa uchungu,
kama mtu anayemwombolezea mwana wa pekee,
maana mwangamizi atakuja,
na kuwashambulia ghafla.
27Yeremia, wewe nimekuweka kuwa mchunguzi
na mpimaji wa watu wangu,
ili uchunguze na kuzijua njia zao.
28Wote ni waasi wakaidi,
ni watu wanaopitapita wakisengenya wengine,
wagumu kama shaba nyeusi au chuma;
wote hutenda kwa ufisadi.
29Mifuo inafukuta kwa nguvu,
risasi inayeyukia humohumo motoni;
ni bure kuendelea kuwatakasa watu wangu,
waovu hawawezi kuondolewa uchafu wao.
30Wataitwa ‘Takataka za fedha’,
maana mimi Mwenyezi-Mungu nimewakataa.”


Yeremia6;1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: