Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 19 April 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 107...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Nyinyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu, tunawaombeni mfanye hata zaidi. Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana, kwamba sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. Basi, farijianeni kwa maneno haya.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.

KITABU CHA TANO
(Zaburi 107–150)
Sifa kwa Mungu mwema
1 Taz Zab 100:5; 106:1; 118:1; 136:1 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema;
kwa maana fadhili zake zadumu milele!
2Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu,
watu ambao aliwaokoa katika taabu,
3akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni:
Kutoka mashariki na magharibi,
kutoka kaskazini na kusini.107:3 kusini: Kiebrania: Bahari; yaani magharibi.
4Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu,
wasiweze kufikia mji wa kukaa.
5Waliona njaa na kiu;
wakavunjika moyo kabisa.
6Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso yao.
7Aliwaongoza katika njia iliyonyoka,
mpaka wakaufikia mji wa kukaa.
8Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
9Yeye huwatosheleza walio na kiu;
na wenye njaa huwashibisha mema.
10Baadhi waliishi katika giza na ukiwa,
wafungwa katika mateso na minyororo,
11kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu,
na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu.
12Walikuwa hoi kwa kazi ngumu,
wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia.
13Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso yao.
14Aliwatoa katika giza na ukiwa,
na minyororo yao akaivunjavunja.
15Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
16Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba,
na kukatakata fito za chuma.
17Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao,
waliteseka kwa sababu ya uovu wao;
18chakula kikawa kinyaa kwao,
wakawa nusura wafe.
19Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso yao.
20Kwa neno lake aliwaponya,
akawaokoa wasiangamie.
21Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
22Wamtolee tambiko za shukrani;
wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe.
23Baadhi walisafiri baharini kwa meli,
na kufanya shughuli zao humo baharini.
24Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu,
mambo ya ajabu aliyotenda huko.
25Aliamuru, akazusha dhoruba kali,
ikarusha juu mawimbi ya bahari.
26Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini;
uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo.
27Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi;
maarifa yao ya uanamaji yakawaishia.
28Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu,
naye akawaokoa katika mateso zao.
29Aliifanya ile dhoruba kali itulie,
nayo mawimbi yakanyamaza.
30Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu;
akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea.
31Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake;
kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu.
32Mtukuzeni katika kusanyiko la watu,
na kumsifu katika baraza la wazee.
33Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa,
chemchemi akazikausha kabisa.
34Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi,
kwa sababu ya uovu wa wakazi wake.
35Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji,
na nchi kame kuwa chemchemi za maji.
36Akawahamishia huko wenye njaa,
nao wakajenga mji wa kukalika.
37Walilima mashamba na kupanda mizabibu,
wakavuna mazao kwa wingi.
38Aliwabariki watu wake, wakaongezeka;
na idadi ya wanyama wao akaizidisha.
39Kisha walipopungua na kuwa wanyonge,
kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni,
40aliwadharau wakuu waliowatesa,
akawazungusha jangwani kusiko na njia.
41Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao,
akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo.
42Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi,
lakini waovu wote wananyamazishwa.
43Wenye hekima na wayafikirie mambo haya,
wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.



Zaburi107;1-43

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: