Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 16 April 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 104...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Ndugu zangu, watu wa Mungu ambao mmeitwa na Mungu, fikirini juu ya Yesu Mtume na Kuhani Mkuu wa imani tunayoiungama. Yeye alikuwa mwaminifu kwa Mungu aliyemteua kufanya kazi yake kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Lakini Yesu anastahili heshima kubwa kuliko Mose maana mjenzi wa nyumba hupata heshima zaidi kuliko hiyo nyumba yenyewe. Kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ndiye mjenzi wa vitu vyote.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Mose alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Bwana kama mtumishi, na alinena juu ya mambo ambayo Mungu atayasema hapo baadaye. Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana mwenye mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. Sisi wenyewe ni nyumba yake kama tukiendelea kuwa hodari na thabiti katika kile tunachotumainia.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Kumsifu Muumba
1 Taz Ebr 1:7 Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, wewe ni mkuu mno!
Umejivika utukufu na fahari.
2Umejizungushia mwanga kama vazi,
umezitandaza mbingu kama hema;
3umejenga makao yako juu ya maji ya mbingu.
Umeyafanya mawingu kuwa gari lako;
waruka juu ya mabawa ya upepo,
4waufanya upepo kuwa mjumbe wako,
moto na miali yake kuwa watumishi wako.
5Dunia umeiweka imara juu ya misingi yake,
ili isitikisike milele.
6Uliifunika dunia kwa bahari kama vazi,
na maji yakaimeza milima mirefu.
7Ulipoyakaripia, maji yalikimbia,
yaliposikia ngurumo yako yalitimka mbio.
8Yaliporomoka toka milimani hadi mabondeni,
mpaka pale mahali ulipoyatengenezea.
9Uliyawekea hayo maji mipaka,
yasije yakaifunika tena dunia.
10Umetokeza chemchemi mabondeni,
na mikondo yake ipite kati ya vilima.
11Hizo zawapatia maji wanyama wote porini.
Humo pundamwitu huzima kiu zao.
12Ndege hujenga viota vyao katika miti ya hapo,
hutua katika matawi yake na kuimba.
13Toka juu angani wainyeshea milima mvua,
nayo dunia waitosheleza kwa baraka yako.
14Waotesha nyasi kwa ajili ya mifugo,
na mimea kwa matumizi ya binadamu
ili naye ajipatie chakula chake ardhini:
15Divai ya kumchangamsha,
mafuta ya zeituni ya kumfurahisha,
na mkate wa kumpa nguvu.
16Miti mikubwa ya Mwenyezi-Mungu yapata maji ya kutosha;
naam, mierezi ya Lebanoni aliyoiotesha.
17Humo, ndege hujenga viota vyao;
korongo hufanya maskani yao katika misonobari.
18Milima mirefu ni makao ya mbuzimwitu;
na pelele hupata maficho yao miambani.
19Umeuumba mwezi utupimie majira;
jua nalo lajua wakati wa kutua.
20Waleta giza, usiku waingia;
nao wanyama wote wa porini wanatoka:
21Wanasimba hunguruma wapate mawindo,
humngojea Mungu awape chakula chao.
22Jua lichomozapo hurudi makwao,
na kujipumzisha mapangoni mwao.
23Hapo naye binadamu huenda kwenye shughuli zake;
na kufanya kazi zake mpaka jioni.
24Ee Mwenyezi-Mungu, umetenda mambo mengi mno!
Yote umeyafanya kwa hekima!
Dunia imejaa viumbe vyako!
25Mbali kule iko bahari - kubwa na pana,
ambamo kumejaa viumbe visivyohesabika,
viumbe hai, vikubwa na vidogo.
26 Taz Zab 74:14 Ndimo zinamosafiri meli,
na lile dude Lewiyathani uliloliumba licheze humo.
27Wote wanakungojea wewe,
uwapatie chakula chao kwa wakati wake.
28Wanaokota chochote kile unachowapa;
ukifumbua mkono wako wanashiba vinono.
29Ukiwapa kisogo, wanaogopa;
ukiondoa pumzi yao, wanakufa,
na kurudi mavumbini walimotoka.
30Ukiwapulizia pumzi yako, wanaishi tena;
wewe waipa dunia sura mpya.
31Utukufu wa Mwenyezi-Mungu udumu milele;
Mwenyezi-Mungu apendezwe na matendo yake mwenyewe.
32Huitazama dunia nayo hutetemeka,
huigusa milima nayo hutoa moshi!
33Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote;
nitamsifu Mungu wangu muda wote niishipo.
34Upendezwe, ee Mwenyezi-Mungu, na mawazo yangu haya;
maana furaha yangu naipata kwako.
35Wenye dhambi waondolewe duniani,
pasiwe na waovu wowote tena!
Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu!
Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Zaburi104;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: