Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 17 April 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 105...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Kwa hiyo, basi, kama asemavyo Roho Mtakatifu: “Kama mkisikia sauti yake leo, msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi kama wakati ule wa majaribio kule jangwani. Huko wazee wenu walinijaribu na kunichunguza, ingawa walishuhudia matendo yangu kwa miaka arubaini! Kwa sababu hiyo niliwakasirikia watu hao nikasema, ‘Fikira za watu hawa zimepotoka, hawajapata kamwe kuzijua njia zangu’. Basi, nilikasirika, nikaapa: ‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko.’
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Basi ndugu, jihadharini asije akawako yeyote miongoni mwenu aliye na moyo mbaya hivyo na asiyeamini hata kujitenga na Mungu aliye hai. Maadamu hiyo “Leo” inayosemwa katika Maandiko bado inatuhusu sisi, mnapaswa kusaidiana daima, ili mtu yeyote miongoni mwenu asidanganywe na dhambi na kuwa mkaidi. Maana sisi tunashirikiana na Kristo ikiwa tutazingatia kwa uthabiti tumaini tulilokuwa nalo mwanzoni.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Maandiko yasema hivi: “Kama mkisikia sauti yake leo, msiwe wakaidi kama wakati ule waliponiasi.” Ni akina nani waliosikia sauti ya Mungu wakamwasi? Ni wale wote walioongozwa na Mose kutoka Misri. Mungu aliwakasirikia akina nani kwa miaka arubaini? Aliwakasirikia wale waliotenda dhambi, maiti zao zikatapakaa kule jangwani. Mungu alipoapa: “Hawataingia mahali pangu pa pumziko,” alikuwa anawasema akina nani? Alikuwa anasema juu ya hao walioasi. Basi, twaona kwamba hawakuingia huko kwa sababu hawakuamini.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....Nawapenda.

Mungu na watu wake
(1Nya 16:8-22)
1Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, tangazeni ukuu wake;
yajulisheni mataifa mambo aliyotenda!
2Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa;
simulieni matendo yake ya ajabu!
3Jisifieni jina lake takatifu;
wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi.
4Tafuteni msaada kwa Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu;
mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima.
5Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda,
miujiza yake na hukumu alizotoa,
6enyi wazawa wa Abrahamu mtumishi wake,
enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake;
7Yeye ndiye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu;
hukumu zake zina nguvu duniani kote.
8Yeye hulishika agano lake milele,
hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu.
9Hushika agano alilofanya na Abrahamu,
na ahadi aliyomwapia Isaka.
10Alimthibitishia Yakobo ahadi yake,
alimhakikishia Israeli agano hilo la milele.
11Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani,
nayo itakuwa mali yenu wenyewe.”
12Watu wa Mungu walikuwa wachache; hawakuwa maarufu,
tena walikuwa wageni nchini Kanaani.
13Walitangatanga kutoka taifa hadi taifa;
kutoka nchi moja hadi nchi nyingine.
14Lakini Mungu hakuruhusu mtu awadhulumu;
kwa ajili yao aliwaonya wafalme:
15“Msiwaguse wateule wangu;
msiwadhuru manabii wangu!”
16Mungu alizusha njaa nchini mwao,
akaharibu chakula chao chote.
17Lakini aliwatangulizia mtu mmoja,
Yosefu aliyekuwa ameuzwa utumwani.
18Walimfunga miguu kwa minyororo,
na shingoni kwa nira ya chuma,
19Muda si muda alichotabiri kilitimia.
neno la Mwenyezi-Mungu lilimdhibiti.
20Mfalme wa Misri akaamuru afunguliwe;
mtawala wa mataifa akamwachilia huru.
21Alimweka kuwa mkurugenzi wa serikali yake,
na mkuu wa mali yake yote;
22awaongoze maofisa wake apendavyo,
na kuwafundisha wazee wake hekima.
23Ndipo Israeli akaingia nchini Misri;
Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.
24Mwenyezi-Mungu akawafanya watu wake wazae sana;
akawajalia nguvu kuliko maadui zao.
25Aliwafanya Wamisri wawachukie watu wake,
wakawatendea hila watumishi wake.
26Kisha akamtuma Mose mtumishi wake,
akamtuma na Aroni mteule wake.
27Wakafanya ishara za Mungu kati ya Wamisri,
na miujiza katika nchi hiyo ya Hamu.
28Mungu akaleta giza juu ya nchi;
lakini Wamisri wakakataa kutii amri zake.105:28 wakakataa kutii amri zake: Hivyo katika hati kadha za kale. Kiebrania: Wakatii.
29Akageuza mito yao kuwa damu,
akawaua samaki wao wote.
30Vyura wakaivamia nchi yao,
hata jumba la mfalme likajawa nao.
31Mungu akanena, kukazuka makundi ya nzi,
na viroboto katika nchi yote.
32Badala ya mvua akawapa mvua ya mawe,
na umeme uliomulika nchi yao yote;
33akaharibu mizabibu na mitini yao,
akaivunja pia miti ya nchi yao.
34Mungu akanena, kukazuka nzige,
na panzi maelfu yasiyohesabika;
35wakaitafuna mimea yote katika nchi,
wakayala mazao yao yote.
36Aliwaua wazaliwa wa kwanza nchini mwao,
chipukizi wa kwanza wa jamaa za Wamisri.
37Kisha akawatoa watu wa Israeli nchini,
wakiwa na fedha na dhahabu;
wala hakuna hata mmoja wao aliyejikwaa.
38Wamisri walifurahia kuondoka kwao,
kwani hofu iliwashika kwa sababu yao.
39Mungu alitandaza wingu juu ya watu wake,
na moto ili kuwaangazia usiku.
40Waliomba105:40 Waliomba: Makala nyingine za kale; Aliomba. naye akawaletea kware,
akawapa mkate kutoka mbinguni kwa wingi.
41Alipasua mwamba maji yakabubujika;
yakatiririka jangwani kama mto.
42Aliikumbuka ahadi yake takatifu,
aliyompa Abrahamu mtumishi wake.
43Basi akawatoa watu wake nchini,
wateule wake wakaimba na kushangilia.
44Aliwapa nchi za mataifa mengine
na kuwakabidhi mashamba ya wenyeji;
45kusudi watu wake watii masharti yake,
na kufuata sheria zake.
Asifiwe Mwenyezi-Mungu!

Zaburi105;1-45

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: