Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 23 April 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 109...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Sikilizeni neno la Mwenyezi-Mungu, enyi msikiao neno lake mkatetemeka: “Ndugu zenu ambao wanawachukia, na kuwapiga marufuku kwa sababu yangu, wamesema kwa dharau ‘Mungu na aoneshe utukufu wake, nasi tuwaone nyinyi mkishinda!’ Lakini wao wenyewe ndio watakaoaibishwa!
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Sikilizeni, ghasia kutoka mjini, sauti kutoka hekaluni! Hiyo ni sauti ya Mwenyezi-Mungu akiwaadhibu maadui zake!
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

“Mji wangu mtakatifu, ni kama mama ajifunguaye bila kuona uchungu; kabla uchungu kuanza, amekwisha zaa mtoto. Ni nani aliyepata kusikia jambo kama hilo? Ni nani aliyewahi kuona jambo kama hilo? Je, nchi nzima yaweza kuzaliwa siku moja? Je, taifa zima laweza kuzaliwa mara moja? Maana Siyoni, mara tu alipoanza kuona uchungu, alijifungua watoto wake.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Lalamiko la mtu taabuni
(Kwa Mwimbishaji. Wimbo wa Daudi)
1Usinyamaze, ee Mungu ninayekusifu!
2Watu waovu na wadanganyifu wanishambulia,
wanasema uongo dhidi yangu.
3Wanasema maovu juu yangu,
na kunishambulia bila kisa.
4Ingawa niliwapenda, walinishtaki,
hata hivyo niliwaombea dua.
5Wananilipa uovu kwa wema wangu,
na chuki kwa mapendo yangu.
6Umweke hakimu mbaya dhidi ya adui yangu;
na mshtaki wake ampeleke mahakamani.
7Anapohukumiwa apatikane na hatia;
lalamiko lake lihesabiwe kuwa kosa jingine.
8 Taz Mate 1:20 Siku za maisha yake ziwe chache,
mtu mwingine na achukue kazi yake!
9Watoto wake wawe yatima,
na mke wake awe mjane!
10Watoto wake watangetange na kuombaomba;
wafukuzwe katika magofu ya nyumba zao!
11Anayemdai kitu amnyanganye mali yake yote;
na wageni wanyakue mapato ya jasho lake!
12Pasiwe na mtu wa kumwonea huruma,
au Kuwatunza watoto wake yatima!
13Wazawa wake wote wafe;
jina lake lisahauliwe katika kizazi kijacho!
14Mwenyezi-Mungu aukumbuke uovu wa wazee wake,
dhambi za mama yake zisifutwe kamwe!
15Mwenyezi-Mungu azikumbuke dhambi zao daima;
lakini wao wenyewe wasahauliwe duniani.
16Mwovu huyo hakujali kabisa kuwa na huruma,
ila aliwadhulumu maskini na fukara,
kadhalika na watu wanyonge mpaka kifo.
17Yeye alipenda kulaani watu,
laana na impate yeye mwenyewe.
Hakuwatakia wengine baraka,
basi, asipate baraka yeye mwenyewe.
18Kwake kulaani ni kama kuvaa nguo,
basi, laana hizo zimloweshe kama maji,
zimwingie mifupani mwake kama mafuta.
19Laana zimfunike kama nguo,
zimzunguke daima kama ukanda.
20Mwenyezi-Mungu awalipe hayo hao watu wanaonishtaki,
naam hao wanaosema mabaya dhidi yangu.
21Lakini ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wangu,
unitendee kadiri ya hisani yako;
uniokoe, kwa sababu ya wema wa fadhili zako!
22Mimi ni maskini na fukara;
nimejeruhiwa mpaka moyoni mwangu.
23Natoweka kama kivuli cha jioni;
nimepeperushwa kama nzige.
24Magoti yangu yamenyongonyea kwa mfungo;
nimebaki mifupa na ngozi.
25 Taz Mat 27:39; Marko 15:29 Nimekuwa dhihaka tupu kwa watu;
wanionapo hutikisa vichwa vyao kwa dharau.
26Unisaidie, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu;
uniokoe kadiri ya fadhili zako.
27Waoneshe watu kuwa ndiwe uliyetenda hayo,
wewe, ee Mwenyezi-Mungu, ndiwe uliyefanya hivyo.
28Waache walaani, lakini wewe unibariki;
wanaonishambulia waaibike, nami mtumishi wako nifurahi.
29Maadui zangu na wavishwe fedheha;
wajifunike aibu yao kama blanketi.
30Nitamshukuru sana Mwenyezi-Mungu kwa sauti;
nitamsifu kati ya kundi kubwa la watu,
31kwa maana yeye humtetea maskini,
humwokoa wakati anapohukumiwa.

Zaburi109;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: