Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 28 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Waroma....3

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Niko hoi kwa kukungojea uniokoe; naweka tumaini langu katika neno lako. Macho yangu yanafifia nikingojea ulichoahidi. Nauliza: “Utakuja lini kunifariji?”

Zaburi 119:81-82

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Nimekunjamana kama kiriba katika moshi, hata hivyo sijasahau masharti yako. Mimi mtumishi wako nitasubiri mpaka lini? Utawaadhibu lini wale wanaonidhulumu? Wenye kiburi wamenichimbia mashimo, watu ambao hawafuati sheria yako.

Zaburi 119:83-85

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Amri zako zote ni za kuaminika; watu wananitesa bila haki; unisaidie! Karibu wangefaulu kuniangamiza, lakini mimi sijavunja kanuni zako. Unisalimishe kadiri ya fadhili zako, nipate kuzingatia maamuzi uliyotamka.

Zaburi 119:86-88

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


1Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? 2Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. 3Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? 4Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:

“Kila usemapo,
maneno yako ni ya kweli;
na katika hukumu,
wewe hushinda.”
5Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). 6Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu?
7Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” 8Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili!
Hakuna mtu yeyote aliye mwadilifu
9Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. 10Taz Zab 14:1-3; 53:1-3 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
“Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu!
11Hakuna mtu anayeelewa,
wala anayemtafuta Mungu.
12Wote wamepotoka
wote wamekosa;
hakuna atendaye mema,
hakuna hata mmoja.
13 Taz Zab 5:9; 140:3 Makoo yao ni kama kaburi wazi,
ndimi zao zimejaa udanganyifu,
midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka.
14 Taz Zab 10:7 Vinywa vyao vimejaa laana chungu.
15Miguu yao iko mbioni kumwaga damu,
16popote waendapo husababisha maafa na mateso;
17njia ya amani hawaijui.
18 Taz Zab 36:1 Hawajali kabisa kumcha Mungu.”
19Tunajua kwamba sheria huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. 20Taz Zab 143:2 Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi.
Kukubaliwa na Mungu kwa imani
21Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. 22Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. 23Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. 24Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. 25Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; 26sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.
27Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini. 28Maana Mungu humkubali mtu kuwa mwadilifu kwa imani, wala si kwa kutimiza matakwa ya sheria. 29Au je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa mataifa mengine? Naam, wa watu wa mataifa mengine pia. 30Mungu ni mmoja, naye atawafanya Wayahudi kuwa waadilifu kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao. 31Je, tunaitumia imani kuibatilisha sheria? Hata kidogo; bali tunaipa sheria thamani yake kamili.

Waroma3;1-31
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: