Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 26 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Matendo,Leo Tunaanza Kitabu cha Waroma....1

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Matendo
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Waroma"
tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Umenitendea vema mimi mtumishi wako, kama ulivyoahidi, ee Mwenyezi-Mungu. Unifundishe akili na maarifa, maana nina imani sana na amri zako. Kabla ya kuniadhibu nilikuwa nikikosea, lakini sasa nashika neno lako.

Zaburi 119:65-67

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Wewe ni mwema na mfadhili; unifundishe masharti yako. Wenye kiburi wanasema uongo juu yangu, lakini mimi nashika kanuni zako kwa moyo wote. Mioyo yao imejaa upumbavu, lakini mimi nafurahia sheria yako.

Zaburi 119:68-70

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Nimefaidika kutokana na taabu yangu, maana imenifanya nijifunze masharti yako. Sheria uliyoweka ni bora kwangu, kuliko mali zote za dunia.

Zaburi 119:71-72

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


1Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu.

2Hapo kale, Mungu aliwaahidi watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu. 3Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kuhusu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi; 4kuhusu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka kwa wafu. 5Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii. 6Nyinyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo.
7Basi, nawaandikia nyinyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Shukrani kwa Mungu
8Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote. 9Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni 10daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa. 11Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha. 12Ndiyo kusema, tutaimarishana: Imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha nyinyi.
13Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine. 14Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu. 15Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu nyinyi mlioko huko Roma.
Nguvu ya Habari Njema
16Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza na wasio Wayahudi pia. 17Kwa maana Habari Njema inaonesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho; kama ilivyoandikwa: “Mwadilifu1:17 Mwadilifu kwa imani ataishi: Au Mwadilifu ataishi kwa amani. kwa imani ataishi.”
Kosa la binadamu
18Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane. 19Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhihirisha. 20Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea! 21Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza. 22Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu. 23Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao.
24Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao. 25Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina.
26Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile. 27Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke, wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu.
28Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya. 29Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, 30na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao; 31hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine. 32Wanajua kwamba sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.


Waroma1;1-32
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: