Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 13 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 20...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


Heri watu wanaoishi bila kosa, wanaozingatia sheria ya Mwenyezi-Mungu. Heri wanaozingatia matakwa yake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote,

Zaburi 119:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


watu wasiotenda uovu kamwe, bali daima hufuata njia zake. Ee Mungu, umetupatia kanuni zako ili tuzishike kwa uaminifu.

Zaburi 119:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Laiti mwenendo wangu ungeimarika, kwa kuyafuata masharti yako! Nikizingatia amri zako zote, hapo kweli sitaaibishwa.

Zaburi 119:5-6

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Paulo anakwenda tena Makedonia na Ugiriki

1Ile ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia. 2Alipitia sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika Ugiriki 3ambako alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa kupitia Makedonia. 4Sopatro, mwana wa Pirho, kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia. 5Hao walitutangulia na kutungojea kule Troa. 6Sisi, baada ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja.
Kukutana na waumini wa Troa kwa mara ya mwisho
7Jumamosi jioni tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane. 8Katika chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka. 9Kijana mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa. 10Lakini Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, “Msiwe na wasiwasi maana kuna uhai bado ndani yake.” 11Kisha akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka. 12Wale watu walimchukua yule kijana hadi nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo kikubwa.
Safari kutoka Troa kwenda Mileto
13Sisi tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu. 14Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda Mitulene. 15Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto. 16Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana.
Paulo anawaaga wazee wa Efeso
17Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso wakutane naye. 18Walipofika kwake aliwaambia, “Mnajua jinsi nilivyokaa nanyi siku zote tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia. 19Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi. 20Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni. 21Niliwaonya wote – Wayahudi, kadhalika na watu wa mataifa, wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu. 22Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko. 23Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea. 24Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa kitu sana kwangu mradi tu nikamilishe ule utume wangu na ile kazi aliyonipa Bwana Yesu niifanye, yaani nishuhudie Habari Njema ya neema ya Mungu.
25“Nimepita miongoni mwenu nyote nikiuhubiri ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu atakayeniona tena. 26Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote. 27Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio lote la Mungu. 28Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho Mtakatifu amewaweka nyinyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo amejipatia kwa damu ya Mwanae. 29Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo. 30Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu. 31Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi.
32“Na sasa basi, ninawaweka nyinyi chini ya ulinzi wa Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga na kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake. 33Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala nguo za mtu yeyote. 34Mnajua nyinyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu. 35Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe: ‘Heri zaidi kutoa kuliko kupokea.’”
36Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao wote, akasali. 37Wote walikuwa wanalia, na kumwaga kwa kumkumbatia na kumbusu. 38Jambo lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi, wakamsindikiza hadi melini.

Matendo20;1-38
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: