Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 5 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 14...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Makosa yenu yamewazuia msipate baraka hizo, dhambi zenu zimewafanya msipate mema. Naam, kuna walaghai miongoni mwa watu wangu, watu ambao hunyakua mali za wengine. Wako kama wawindaji wa ndege: Hutega mitego yao na kuwanasa watu.

Yeremia 5:25-26

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Kama vile kapu lililojaa ndege walionaswa, ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu. Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri, wamenenepa na kunawiri. Katika kutenda maovu hawana kikomo hawahukumu yatima kwa haki wapate kufanikiwa, wala hawatetei haki za watu maskini.

Yeremia 5:27-28

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


“Je, nisiwaadhibu kwa mambo haya? Je nitaacha kulipiza kisasi taifa kama hili? Jambo la ajabu na la kuchukiza limetokea katika nchi hii: Manabii wanatabiri mambo ya uongo, makuhani nao hutafuta faida yao wenyewe; na watu wangu wanaona jambo hilo kuwa sawa. Lakini mwisho utakapofika mtafanyaje?”

Yeremia 5:29-31

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Paulo na Barnaba huko Ikonio

1Kule Ikonio, mambo yalikuwa kama yalivyokuwa kule Antiokia; Paulo na Barnaba walikwenda katika sunagogi la Wayahudi wakaongea kwa uhodari hata Wayahudi wengi na Wagiriki wakawa waumini. 2Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili wawapinge hao ndugu. 3Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu. 4Watu wa mji huo waligawanyika: Wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume.
5Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe. 6Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani, 7wakawa wanahubiri Habari Njema huko.
Paulo na Barnaba huko Lustra na Derbe
8Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa kiwete tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe. 9Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa, 10akasema kwa sauti kubwa, “Simama wima kwa miguu yako!” Huyo mtu aliyelemaa miguu akainuka ghafla, akaanza kutembea. 11Umati wa watu walipoona alichofanya Paulo, walianza kupiga kelele kwa lugha ya Kilukaonia: “Miungu imetujia katika sura za binadamu!” 12Barnaba akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme. 13Naye kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua mbele ya mlango mkuu wa mji, naye pamoja na ule umati wa watu akataka kuwatambikia mitume.
14Barnaba na Paulo walipopata habari hizo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa: 15Taz Zab 146:6 “Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama nyinyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. 16Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda. 17Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: Huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha.” 18Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie.
19Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa. 20Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka, akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe.
Paulo na Barnaba wanarudi mjini Antiokia, Siria
21Baada ya Paulo na Barnaba kuhubiri Habari Njema huko Derbe na kupata wafuasi wengi, walifunga safari kwenda Antiokia kwa kupitia Lustra na Ikonio. 22Waliwaimarisha waumini wa miji hiyo na kuwatia moyo wabaki imara katika imani. Wakawaambia, “Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu.” 23Waliteua wazee katika kila kanisa kwa ajili ya waumini, kisha, kwa kusali na kufunga, wakawaweka chini ya ulinzi wa Bwana ambaye walikuwa wanamwamini.
24Baada ya kupitia katika nchi ya Pisidia, walifika Pamfulia. 25Baada ya kuhubiri ule ujumbe huko Perga, walikwenda Atalia. 26Kutoka huko walisafiri kwa meli wakarudi Antiokia ambako hapo awali walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi wa neema ya Mungu kwa ajili ya kazi ambayo sasa walikuwa wameitimiza.
27Walipofika huko Antiokia walifanya mkutano wa kanisa la mahali hapo, wakawapa taarifa juu ya mambo Mungu aliyofanya pamoja nao, na jinsi alivyowafungulia watu wa mataifa mengine mlango wa kuingia katika imani. 28Wakakaa pamoja na wale waumini kwa muda mrefu.

Matendo14;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: