Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 7 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 16...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


“Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake. Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

Kutoka 23:10-11

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



“Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe. Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako.

Kutoka 23:12-13

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.




 Timotheo anajiunga na Paulo na Sila

1Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki. 2Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio. 3Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki. 4Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie. 5Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.
Paulo anaona maono kule Troa
6Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia. 7Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa. 9Usiku huo, Paulo aliona maono ambayo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: “Vuka, uje Makedonia ukatusaidie.” 10Mara baada ya Paulo kuona maono hayo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema.
Kuongoka kwa Ludia
11Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli. 12Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa. 13Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo. 14Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema. 15Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.
Paulo na Sila wanatiwa nguvuni
16Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake. 17Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, “Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu.” 18Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, “Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!” Mara huyo pepo akamtoka.
19Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu. 20Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, “Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu. 21Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata.” 22Kundi la watu likajiunga likawashambulia; na wale mahakimu wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakaamuru wapigwe viboko. 23Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali. 24Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.
25Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza. 26Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana. 27Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka, na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua. 28Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: “Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa.”
29Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu. 30Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, “Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?” 31Wao wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote.” 32Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake. 33Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo. [ 34Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu].
35Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, “Wafungueni wale watu.” 36Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: “Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani.” 37Lakini Paulo alimjibu, “Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie.” 38Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa. 39Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule. 40Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.

Matendo16;1-40
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: