Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 18 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 23...

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani; usinifiche amri zako. Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa ya kutaka kujua daima maagizo yako.

Zaburi 119:19-20

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Wewe wawakemea wenye kiburi, walaanifu, ambao wanakiuka amri zako. Uniepushe na matusi na madharau yao, maana nimeyazingatia maamuzi yako.

Zaburi 119:21-22

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu; mimi mtumishi wako nitayatafakari maamuzi yako. Masharti yako ni furaha yangu; hayo ni washauri wangu.

Zaburi 119:23-24

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.
1Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza kusema, “Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema mbele ya Mungu.” 2Hapo kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni. 3Basi, Paulo akamwambia, “Mungu mwenyewe atakupiga kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja sheria kwa kuamuru nipigwe?” 4Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo, “Unamtukana kuhani mkuu wa Mungu!” 5Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni kuhani mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: ‘Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu wako.’”


6
Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaza sauti yake mbele ya Baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu watafufuka.” 
7Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili. 8Kisa chenyewe kilikuwa hiki, Masadukayo hushikilia kwamba wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo husadiki hayo yote matatu. 9Kelele ziliongezeka na baadhi ya waalimu wa sheria wa kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu: “Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho au malaika ameongea naye.”
10Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome.
11Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo, akamwambia, “Jipe moyo! Umenishuhudia hapa Yerusalemu, utafanya vivyo hivyo mjini Roma.”
Wayahudi wanafanya mpango wa kumwua Paulo
12Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha. Wakala kiapo: “Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua Paulo.” 13Watu zaidi ya arubaini ndio waliokula njama kufanya hivyo. 14Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, “Sisi tumekula kiapo kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo tutakapokuwa tumemuua Paulo. 15Sasa basi, nyinyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumwua hata kabla hajafika karibu.”
16Lakini mtoto wa ndugu yake Paulo alisikia juu ya mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo. 17Hapo Paulo akamwita mmoja wa maaskari, akamwambia, “Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia.” 18Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa mkuu wa jeshi, akasema, “Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukuambia.” 19Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka mahali pa faragha, akamwuliza, “Una nini cha kuniambia?” 20Yeye akasema, “Wayahudi wamepatana wakuombe umpeleke Paulo Barazani wakijisingizia kwamba Baraza lingependa kupata habari kamili zaidi juu yake. 21Lakini wewe usikubali kwa maana kuna watu zaidi ya arubaini walio tayari kumvamia. Wameapa kutokula wala kunywa kitu mpaka watakapokuwa wamemuua. Sasa wako tayari, wanangojea tu uamuzi wako.” 22Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo.
Paulo anapelekwa kwa mkuu wa mkoa
23Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia, “Wekeni tayari askari 200, wapandafarasi sabini na askari 200 wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku. 24Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa.” 25Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi:
26“Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu!
27“Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja na askari nikamwokoa. 28Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa cha mashtaka yao. 29Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu ya sehemu kadha wa kadha za sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani. 30Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya njama za kumwua, niliamua kumleta kwako, nikawaambia washtaki wake walete mashtaka yao mbele yako.”
31Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa; wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri. 32Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha wale askari wapandafarasi waendelee na safari pamoja na Paulo. 33Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na kumweka Paulo chini ya mamlaka yake. 34Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia, 35akasema, “Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki wako kufika.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi wa Herode.

Matendo23;1-35
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: