Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 19 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 24...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu...


Nagaagaa chini mavumbini; unipe tena uhai kama ulivyoahidi. Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako. Unifundishe namna ya kushika kanuni zako, nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu.

Zaburi 119:25-27

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Niko hoi kwa uchungu; unirudishie nguvu kama ulivyoahidi. Uniepushe na njia za upotovu; unifundishe kwa wema sheria yako.

Zaburi 119:28-29

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Nimechagua njia ya uaminifu; nimezingatia maagizo yako. Nazingatia maamuzi yako, ee Mwenyezi-Mungu; usikubali niaibishwe! Nitafuata maelekezo ya amri zako, maana unanipa maarifa zaidi.

Zaburi 119:30-32

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Wayahudi wanamshtaki Paulo

1Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania aliwasili Kaisarea pamoja na wazee kadhaa na wakili mmoja wa sheria aitwaye Tertulo. Walimwendea yule mkuu wa mkoa wakamweleza mashtaka yao juu ya Paulo. 2Paulo aliitwa, na Tertulo akafungua mashtaka hivi:
“Mheshimiwa Felisi, uongozi wako bora umeleta amani kubwa na marekebisho ya lazima yanafanywa kwa manufaa ya taifa letu. 3Tunalipokea jambo hili kwa furaha daima na kutoa shukrani nyingi kwako kila mahali. 4Lakini, bila kupoteza wakati wako zaidi, tunakusihi kwa wema wako, usikilize taarifa yetu fupi. 5Tumegundua kwamba mtu huyu ni wa hatari mno. Yeye huanzisha ghasia kati ya Wayahudi kila mahali duniani na pia ni kiongozi wa kile chama cha Wanazareti. 6Tena alijaribu kulikufuru hekalu, nasi tukamtia nguvuni. [Tulitaka kumhukumu kufuatana na sheria yetu. 7Lakini Lusia, mkuu wa jeshi, aliingilia kati, akamchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwetu. 8Kisha akaamuru washtaki wake waje mbele yako.] Kama ukimhoji wewe mwenyewe, utaweza kubainisha mambo haya yote tunayomshtaki kwayo.” 9Nao Wayahudi waliunga mkono mashtaka hayo wakisema kwamba hayo yote yalikuwa kweli.
Paulo anajitetea mbele ya Felisi
10Basi, mkuu wa mkoa alimwashiria Paulo aseme. Naye Paulo akasema, “Nafurahi kujitetea mbele yako nikijua kwamba umekuwa hakimu wa taifa hili kwa miaka mingi. 11Unaweza kujihakikishia kwamba si zaidi ya siku kumi na mbili tu zimepita tangu nilipokwenda kuabudu Yerusalemu. 12Wayahudi hawakunikuta nikijadiliana na mtu yeyote. Hawakunikuta nikichochea watu hekaluni, wala katika masunagogi yao, wala mahali pengine popote katika mji huo. 13Wala hawawezi kuthibitisha mashtaka waliyotoa juu yangu. 14Ninachokubali mbele yako ni hiki: Mimi ninamwabudu Mungu wa wazee wetu nikiishi kufuatana na njia ile ambayo wao wanaiita chama cha uzushi. Ninaamini mambo yote yaliyoandikwa katika vitabu vya sheria na manabii. 15Mimi namtumainia Mungu, na wao wanalo tumaini hilo, kwamba watu, wema na wabaya, watafufuka. 16Kwa hiyo ninajitahidi daima kuwa na dhamiri njema mbele ya Mungu na mbele ya watu.
17“Baada ya kukaa mbali kwa miaka kadhaa, nilirudi Yerusalemu ili kuwapelekea wananchi wenzangu msaada na kutoa tambiko. 18Wakati nilipokuwa nikifanya hayo ndipo waliponikuta hekaluni, nilipokuwa nimekwisha fanya ile ibada ya kujitakasa. Hakukuwako kundi la watu wala ghasia. 19Lakini kulikuwa na Wayahudi wengine kutoka mkoa wa Asia; hao ndio wangepaswa kuwa hapa mbele yako na kutoa mashtaka yao kama wana chochote cha kusema dhidi yangu. 20Au, waache hawa walio hapa waseme kosa waliloliona kwangu wakati niliposimama mbele ya Baraza lao kuu, 21isipokuwa tu maneno haya niliyosema niliposimama mbele yao: ‘Mnanihukumu leo hii kwa sababu ya kushikilia kwamba wafu watafufuliwa!’”
22Hapo, Felisi, ambaye mwenyewe alikuwa anaifahamu hiyo njia vizuri, aliahirisha kesi hiyo. Akawaambia, “Nitatoa hukumu juu ya kesi hiyo wakati Lusia, mkuu wa jeshi, atakapokuja hapa.” 23Kisha akamwamuru yule jemadari amweke Paulo kizuizini, lakini awe na uhuru kiasi, na rafiki zake wasizuiwe kumpatia mahitaji yake.
Paulo mbele ya Felisi na Drusila
24Baada ya siku chache, Felisi alifika pamoja na mkewe Drusila ambaye alikuwa Myahudi. Aliamuru Paulo aletwe, akamsikiliza akiongea juu ya kumwamini Yesu Kristo. 25Lakini wakati Paulo alipoanza kuongea juu ya uadilifu, juu ya kuwa na kiasi na juu ya siku ya hukumu inayokuja, Felisi aliogopa, akasema, “Kwa sasa unaweza kwenda; nitakuita tena nitakapopata nafasi.” 26Wakati huohuo alikuwa anatumaini kwamba Paulo angempa fedha. Kwa sababu hii alimwita Paulo mara kwa mara na kuzungumza naye.
27Baada ya miaka miwili, Porkio Festo alichukua nafasi ya Felisi, akawa mkuu wa mkoa. Kwa kuwa alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi, Felisi alimwacha Paulo kizuizini.

Matendo24;1-27
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: