Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 8 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 17...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,
afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..


“Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu. Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.

Kutoka 23:14-15

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.

Kutoka 23:16-17

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono ye
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


“Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.

Kutoka 23:18-19

Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.



 Fujo Thesalonike kutokana na mahubiri

1Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka Thesalonike ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi. 2Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake, akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akitumia Maandiko Matakatifu. 3Aliyaeleza na kuonesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na kufufuka kutoka kwa wafu. Akawaambia, “Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye Kristo.” 4Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila. Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa tabaka la juu, walijiunga nao.
5Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni, wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani. 6Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: “Watu hawa wamekuwa wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini. 7Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti: ‘Kuna mfalme mwingine aitwaye Yesu.’” 8Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi la watu. 9Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha wakawaacha waende zao.
Katika Berea
10Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi. 11Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa Thesalonike. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila yalikuwa kweli. 12Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa tabaka la juu na wanaume pia.
13Lakini, Wayahudi wa Thesalonike walipogundua kwamba Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu. 14Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila na Timotheo walibaki Berea. 15Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo.
Paulo anaongea na watu wa Athene
16Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa sanamu za miungu. 17Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano mahali pa hadhara pamoja na wote wale waliojitokeza. 18Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana naye. Wengine walisema, “Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?” Kwa kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema, “Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni.” 19Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema, “Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia. 20Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani.” 21Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya.
22Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago, akasema, “Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba nyinyi, kwa vyovyote, ni watu wa dini sana, 23maana nilipokuwa napita huko na huko nikiangalia sanamu zenu za ibada niliona madhabahu moja ambayo imeandikwa: ‘Kwa Mungu asiyejulikana.’ Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua, ndiye ninayemhubiri kwenu. 24Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana wa mbingu na dunia; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu. 25Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha kupumua na kuwapa kila kitu. 26Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi mataifa hayo yangeishi. 27Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko mbali na kila mmoja wetu. 28Kama alivyosema mtu mmoja:
‘Ndani yake yeye sisi tunaishi,
tunajimudu, na tuko!’
Ni kama washairi wenu wengine walivyosema:
‘Sisi ni watoto wake.’
29Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na binadamu. 30Mungu alifanya kana kwamba haoni nyakati zile watu walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu. 31Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka kwa wafu!”
32Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, “Tunataka kukusikia tena juu ya jambo hili!” 33Hivyo, Paulo aliwaacha, akatoka barazani. 34Lakini watu kadhaa waliandamana naye, wakawa waumini. Miongoni mwao walikuwa Dionisio wa Areopago, na mwanamke mmoja aitwaye Damari na wengineo.

Matendo17;1-34
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: