Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 11 January 2021

Kikombe Cha Asubuhi; Matendo 18...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



“Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu.

Kutoka 23:20-21

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nikawaangamiza hao wote,

Kutoka 23:22-23

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


msiiname mbele ya miungu yao kuiabudu, wala kuitumikia, wala msiige mambo yao. Bali mtawaangamiza kabisa na kuzivunjavunja nguzo zao. Mtanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawabariki kwa chakula na maji na kuyaondoa magonjwa kati yenu.

Kutoka 23:24-25

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



 Paulo kule Korintho

1Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho. 2Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona, 3na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi. 4Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki.
5Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo. 6Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakunguta mavazi yake mbele yao akisema, “Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine.” 7Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto, ambaye nyumba yake ilikuwa karibu na lile sunagogi. 8Krispo, mkuu wa hilo sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa.
9Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: “Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo, 10maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu.” 11Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
12Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani. 13Wakasema, “Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na sheria.” 14Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, “Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni. 15Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina na sheria yenu, amueni nyinyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo hayo!” 16Basi, akawafukuza kutoka mahakamani. 17Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo.
Paulo anarudi tena Antiokia
18Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku nyingi. Kisha aliwaaga, akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka. 19Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika sunagogi, akajadiliana na Wayahudi. 20Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda. 21Bali alipokuwa anaondoka, alisema, “Mungu akipenda nitakuja kwenu tena.” Akaondoka Efeso kwa meli.
22Meli ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa, kisha akaenda Antiokia. 23Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote.
Apolo anahubiri Efeso na Korintho
24Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu. 25Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu. 26Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo njia ya Mungu kwa usahihi zaidi. 27Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini; 28kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.

Matendo18;1-28
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: