Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 23 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Tunamshukuru Mungu kwa kumaliza Kitabu cha Mathayo,Leo Tunaanza Kitabu cha Marko ....1



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kibali cha
 kupitia kitabu cha "Mathayo
"
Ni matumaini yangu kuna mengi tumejifunza/kufaidika
na kutupa mwanga/kuelewa kwenye kitabu hiki...

Leo tunapokwenda anza kupitia Kitabu cha"Marko"tunamuomba Mungu wetu akatupe kibali,macho ya rohoni
 na akili ya kuelewa katika kujifunza NENO lake...
Ee Mungu  tunaomba ukatuongoze...!!
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...


Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Lakini Kefa alipofika Antiokia nilimpinga waziwazi maana alikuwa amekosea. Awali, kabla ya watu kadhaa waliokuwa wametumwa na Yakobo kuwasili hapo, Petro alikuwa akila pamoja na watu wa mataifa mengine. Lakini, baada ya hao watu kufika, aliacha kabisa kula pamoja na watu wa mataifa mengine, kwa kuogopa kikundi cha waliosisitiza tohara.

Wagalatia 2:11-12

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote 
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Hata ndugu wengine Wayahudi walimuunga mkono Petro katika kitendo hiki cha unafiki, naye Barnaba akakumbwa na huo unafiki wao.

Wagalatia 2:13

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Basi, nilipoona kuwa msimamo wao kuhusu ukweli wa Injili haukuwa umenyooka, nikamwambia Kefa mbele ya watu wote: “Ingawa wewe ni Myahudi, unaishi kama watu wa mataifa mengine na si kama Myahudi! Unawezaje, basi kujaribu kuwalazimisha watu wa mataifa mengine kuishi kama Wayahudi?”

Wagalatia 2:14

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



 Mahubiri ya Yohane Mbatizaji

(Mat 3:1-12; Luka 3:1-18; Yon. 1:19-28)
1Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.1:1 Mwana wa Mungu: Baadhi ya hati hazina: Mwana wa Mungu. 2Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:
“Mungu alisema, ‘Namtuma mjumbe wangu akutangulie,
ambaye atakutayarishia njia yako.’
3Sauti ya mtu anaita jangwani:
‘Mtayarishieni Bwana njia yake,
nyosheni barabara zake.’”
4Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. 5Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.
6Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 7Naye alihubiri akisema, “Baada yangu anakuja mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. 8Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.”
Kubatizwa na kujaribiwa kwa Yesu
(Mat 3:13–4:11; Luka 3:21-22; 4:1-13)
9Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. 10Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. 11Taz. Zab. 2:7 Sauti ikasikika kutoka mbinguni: “Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe.”
12Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, 13akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamhudumia.
Yesu anawaita wavuvi wanne
(Mat 4:12-22; Luka 4:14-15; 5:1-11)
14Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, 15“Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!”
16Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. 17Yesu akawaambia, “Nifuateni nami nitawafanya nyinyi kuwa wavuvi wa watu.” 18Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. 19Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.
Mtu mwenye pepo mchafu
(Luka 4:31-37)
21Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika sunagogi, akaanza kufundisha. 22Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama waalimu wao wa sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.
23Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, 24akapaza sauti, “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!” 25Yesu akamkemea huyo pepo akisema, “Nyamaza! Mtoke mtu huyu.” 26Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. 27Watu wote wakashangaa, wakaulizana, “Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!” 28Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika eneo la Galilaya.
Yesu anawaponya watu wengi
(Mat 8:14-17; Luka 4:38-41)
29Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao. 30Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili. 31Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.
32Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo. 33Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango. 34Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.
Yesu anahubiri Galilaya
(Luka 4:42-44)
35Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali. 36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta. 37Walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta.” 38Yesu akawaambia, “Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo.” 39Basi, akaenda kila mahali huko Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.
Yesu anamponya mtu mwenye ukoma
(Mat 8:1-4; Luka 5:12-16)
40Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba: “Ukitaka, waweza kunitakasa!” 41Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, “Nataka! Takasika!” 42Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika. 43Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwambia, 44“Angalia usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” 45Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

Marko1;1-45

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: