Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 17 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 25....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

Waroma 8:28-29

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.

Waroma 8:30

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote?

Waroma 8:31-32

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.





 Mfano wa wasichana kumi

1“Wakati huo, ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi. 2Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. 3Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta. 4Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao. 5Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wasichana wote walisinzia, wakalala. 6Usiku wa manane kukawa na kelele: ‘Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.’ 7Hapo wale wasichana wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao. 8Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: ‘Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.’ 9Lakini wale wenye busara wakawaambia, ‘Hayatatutosha sisi na nyinyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!’ 10Basi, wale wasichana wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wasichana waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la harusi, kisha mlango ukafungwa. 11Baadaye wale wasichana wengine wakaja, wakaita: ‘Bwana, Bwana, tufungulie!’ 12Lakini yeye akawajibu, ‘Nawaambieni kweli, siwajui nyinyi.’” 13Kisha Yesu akasema, “Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
Mfano wa watumishi watatu
(Luka 19:11-27)
14“Wakati huo itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ngambo: Aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake. 15Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: Mmoja fedha talanta tano, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri. 16Mara yule aliyekabidhiwa fedha talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano. 17Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili. 18Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaenda, akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.
19“Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake. 20Mtumishi aliyekabidhiwa fedha talanta tano akaja amechukua talanta tano faida, akamwambia, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.’ 21Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’
22“Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, ‘Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.’ 23Bwana wake akamwambia, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.’
24“Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya. 25Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.’
26“Bwana wake akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya. 27Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake! 28Basi, mnyanganyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi. 29Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 30Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’
Hukumu ya mwisho
31“Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu. 32Mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi. 33Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.
34“Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, ‘Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; 36nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.’ 37Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme ‘Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji? 38Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika? 39Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?’ 40Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.’
41“Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake. 42Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji. 43Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.’
44“Hapo nao watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukukuhudumia?’ 45Naye atawajibu, ‘Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.’ 46Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uhai wa milele.”

Mathayo25;1-46

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: