Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 21 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 27....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



Baada ya miaka kumi na minne, nilikwenda tena Yerusalemu pamoja na Barnaba; nilimchukua pia Tito pamoja nami. Kwenda kwangu kulitokana na ufunuo alionipa Mungu. Katika kikao cha faragha niliwaeleza hao viongozi ujumbe wa Injili niliohubiri kwa watu wa mataifa. Nilifanya hivyo kusudi kazi yangu niliyokuwa nimefanya, na ile ninayofanya sasa, isije ikawa bure.

Wagalatia 2:1-2

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Lakini, hata mwenzangu Tito, ambaye ni Mgiriki, hakulazimika kutahiriwa, ingawa kulikuwa na ndugu wengine wa uongo waliotaka atahiriwe. Watu hawa walijiingiza kwa ujanja na kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika kuungana na Kristo Yesu, ili wapate kutufanya watumwa.

Wagalatia 2:3-4

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Hatukukubaliana nao hata kidogo ili ukweli wa Injili ubaki nanyi daima. Lakini watu hawa wanaosemekana kuwa ni viongozi – kama kweli walikuwa hivyo au sivyo, kwangu si kitu, maana Mungu hahukumu kwa kuangalia mambo ya nje – watu hawa hawakuwa na mawazo ya kuniongezea.

Wagalatia 2:5-6

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Yesu anapelekwa kwa Pilato

(Marko 15:1; Luka 23:1-2; Yoh 18:28-32)
1Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumuua. 2Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.
Kifo cha Yuda
(Mate 1:18-19)
3Hapo, Yuda, ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu vile vipande thelathini vya fedha. 4Akawaambia, “Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe.” Lakini wao wakasema, “Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako.” 5Naye akazitupa zile fedha hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga. 6Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, “Haifai kuziweka katika hazina ya hekalu kwa maana ni fedha za damu.” 7Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni. 8Ndio maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu. 9Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: “Walichukua vipande thelathini vya fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walimtia bei, 10wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.”
Pilato anamhoji Yesu
(Marko 15:2-5; Luka 23:3-5; Yoh 18:33-38)
11Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamwambia, “Wewe umesema.” 12Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno. 13Hivyo Pilato akamwuliza, “Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?” 14Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.
Yesu anapewa hukumu ya kifo
(Marko 15:6-15; Luka 23:13-25; Yoh 18:39–19:16)
15Ilikuwa kawaida wakati wa sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka. 16Wakati huo kulikuwa na mfungwa aliyejulikana sana, jina lake Baraba. 17Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, “Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba27:17 Baraba: Aliitwa pia Yesu. ama Yesu aitwaye Kristo?” 18Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.
19Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: “Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.” 20Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe. 21Mkuu wa mkoa akawauliza, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?” Wakamjibu, “Baraba!” 22Pilato akawauliza, “Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?” Wote wakasema, “Asulubiwe!” 23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?” Wao wakazidi kupaza sauti: “Asulubiwe!”
24Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe.” 25Watu wote wakasema, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!” 26Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa asulubiwe.
Askari wanamdhihaki Yesu
(Marko 15:16-20; Yoh 19:2-3)
27Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima. 28Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu. 29Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, “Shikamoo mfalme wa Wayahudi!” 30Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani. 31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
Yesu anasulubiwa
(Marko 15:21-32; Luka 23:26-43; Yoh 19:17-27)
32Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu. 33Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, mahali pa Fuvu la Kichwa, 34Taz. Zab 69:21 wakampa mchanganyiko wa divai na kitu kichungu. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.
35 Taz Zab 22:18 Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. 36Wakaketi, wakawa wanamchunga. 37Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lililoandikwa, “Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi.” 38Wanyanganyi wawili walisulubiwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.
39 Taz Zab 22:7; 109:25 Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema, 40“Wewe! Si ulijidai kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi, shuka msalabani!” 41Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na waalimu wa sheria na wazee walimdhihaki wakisema, 42“Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Ati yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini. 43Taz Zab 22:8 Alimtumainia Mungu na kusema ati yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka.” 44Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.
Yesu anakufa msalabani
(Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; Yoh 19:28-30)
45Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, giza likaikumba nchi yote. 46Taz Zab 22:1 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, “Eli, Eli, lema sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” 47Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, “Anamwita Elia.” 48Taz Zab 69:21 Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe. 49Wengine wakasema, “Acha tuone kama Elia anakuja kumwokoa.” 50Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.
51Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; 52makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa; 53nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika mji mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.
54Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
55Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia. 56Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.
Kuzikwa kwake Yesu
(Marko 15:42-47; Luka 23:50-56; Yoh 19:38-42)
57Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Arimathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe. 59Yosefu akauchukua ule mwili, akauzungushia sanda safi ya kitani, 60akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake. 61Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.
Kaburi linalindwa
62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato, 63Wakasema, “Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi kuliko ule wa awali.” 65Pilato akawaambia, “Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo.” 66Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.

Mathayo27;1-66

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: