Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 1 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 13....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mwanangu kutoka kwangu wakati mimi nipo usingizini, akamlaza kifuani pake. Halafu akaichukua maiti ya mwanawe, akailaza kifuani pangu.

1 Wafalme 3:20

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Nilipoamka asubuhi na kutaka kumnyonyesha mwanangu, nikakuta mtoto amefariki. Nilipochunguza sana, nikagundua kuwa hakuwa mwanangu niliyemzaa.”

1 Wafalme 3:21

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Wa kwangu ndiye aliye hai na wa kwako ndiye aliyekufa”. Naye mwanamke wa kwanza akasema, “La! Mtoto wako ndiye aliyekufa, wangu ni huyo aliye hai!” Basi, wakaendelea kubishana hivyo mbele ya mfalme.

1 Wafalme 3:22

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.




Mfano wa mpanzi
(Marko 4:1-9; Luka 8:4-8)
1Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa. 2Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashuani, akaketi. Watu wote walisimama kwenye ukingo wa ziwa, 3naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano.
“Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. 4Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. 5Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. 6Jua lilipochomoza, ziliteketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. 7Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga. 8Nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: Nyingine punje mia, nyingine sitini na nyingine thelathini. 9Mwenye masikio na asikie!”
Shabaha ya kusema kwa mifano
(Marko 4:10-12; Luka 8:9-10)
10Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?” 11Yesu akawajibu, “Nyinyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa. 12Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 13Ndio maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi. 14Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya:
‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa.
Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.
15Maana akili za watu hawa zimepumbaa,
wameyaziba masikio yao,
wameyafumba macho yao.
La sivyo, wangeona kwa macho yao,
wangesikia kwa masikio yao,
wangeelewa kwa akili zao,
na kunigeukia, asema Bwana,
nami ningewaponya.’
16“Lakini heri yenu nyinyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia. 17Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.
Maelezo ya mfano wa mpanzi
(Marko 4:13-20; Luka 8:11-15)
18“Basi, nyinyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi. 19Yeyote asikiaye neno juu ya ufalme wa Mungu bila kuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. 20Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na mara akalipokea kwa furaha. 21Lakini halishiki na mizizi ndani yake; huendelea kulizingatia neno hilo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya neno hilo, anakata tamaa mara. 22Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali hulisonga neno hilo, naye hazai matunda. 23Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu asikiaye neno hilo na kuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini.”
Mfano wa magugu
24Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja, akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake. 26Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana. 27Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, ‘Bwana, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?’ 28Yeye akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya hivyo’. Basi, watumishi wake wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayangoe?’ 29Naye akawajibu, ‘La, msije labda mnapokusanya magugu, mkangoa na ngano pia. 30Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: Kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu.’”
Mfano wa mbegu ya haradali
(Marko 4:30-32; Luka 13:18-19)
31Yesu akawaambia watu mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake. 32Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikisha ota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, hata ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake.”
Mfano wa chachu
(Luka 13:20-21)
33Yesu akawaambia mfano mwingine: “Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga madebe mawili na nusu, hata unga wote ukaumuka.”
Kutumia mifano
(Marko 4:33-34)
34Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano, 35Taz Zab 78:2 ili jambo lililonenwa na nabii litimie:
“Nitasema nao kwa mifano;
nitafichua yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu.”
Yesu anafafanua mfano wa magugu
36Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani.”
37Yesu akawaambia, “Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu. 38Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu. 39Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika. 40Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati; 41Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, 42na kuwatupa katika tanuri ya moto, na huko watalia na kusaga meno. 43Kisha, wale wema watangara kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie!
Mfano wa hazina iliyofichika
44“Ufalme wa mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.
Mfano wa lulu
45“Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. 46Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile.
Mfano wa wavu wa samaki
47“Tena, ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina. 48Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa. 49Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: Malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema, 50na kuwatupa hao wabaya katika tanuri ya moto. Huko watalia na kusaga meno.”
Hazina mpya na ya kale
51Yesu akawauliza, “Je, mmeelewa mambo haya yote?” Wakamjibu, “Naam.” 52Naye akawaambia, “Hivyo basi, kila mwalimu wa sheria anayekuwa mwanafunzi wa ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.”
Yesu anakataliwa huko Nazareti
(Marko 6:1-6; Luka 4:16-30)

53Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo, 54akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi lao hata wakashangaa, wakasema, “Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu? 55Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi, amepata wapi haya yote?” 57Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!” 58Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao. 


Mathayo13;1-58

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: