Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 8 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 18....

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Ukweli hudumu milele, lakini uongo ni wa kitambo tu. Wanaopanga maovu wamejaa udanganyifu moyoni, lakini wanaonuia mema hupata furaha.

Methali 12:19-20

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Waadilifu hawapatwi na jambo lolote baya, lakini waovu wamejaa dhiki. Midomo isemayo uongo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, lakini watu waaminifu ni furaha yake.

Methali 12:21-22

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Mwenye busara huficha maarifa yake, lakini wapumbavu hutangaza upumbavu wao. Kuwa na bidii kutampa mtu cheo, lakini uvivu utamfanya mtumwa.

Methali 12:23-24

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Ni nani aliye mkubwa?

(Marko 9:33-37; Luka 9:46-48)
1Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Ni nani aliye mkubwa zaidi katika ufalme wa mbinguni?” 2Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao, 3kisha akasema, “Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. 4Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni. 5Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi.
Vikwazo
(Marko 9:42-48; Luka 17:1-2)
6“Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari. 7Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.
8“Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili. 9Na jicho lako likikukosesha, lingoe na kulitupa mbali nawe. Afadhali kwako kuingia katika uhai ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili.
Mfano wa kondoo aliyepotea
(Luka 15:3-7)
10“Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa. Nawaambieni, malaika wao huko mbinguni wako daima mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. [ 11Maana Mwana wa Mtu alikuja kuwaokoa wale waliopotea.] (Taz Luka 19:10). 12Mnaonaje? Mtu akiwa na kondoo 100, akimpoteza mmoja, hufanyaje? Huwaacha wale tisini na tisa mlimani, akaenda kumtafuta yule aliyepotea. 13Akimpata, nawaambieni kweli, humfurahia huyo kuliko awafurahiavyo wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee.
Kusahihishana
15“Ndugu yako akikukosea, mwendee ukamwonye mkiwa nyinyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako. 16Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe. 17Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa, na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watozaushuru.
Kukataza na kuruhusu
18“Nawaambieni kweli, mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachofungua duniani kitafunguliwa mbinguni. 19Tena nawaambieni, wawili miongoni mwenu wakikubaliana hapa duniani kuhusu jambo lolote la kuomba, Baba yangu wa mbinguni atawafanyia jambo hilo. 20Kwa maana popote pale wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo kati yao.”
Mfano wa mtumishi asiyesamehe
21Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, “Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?” 22Yesu akamjibu, “Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba. 23Ndiyo maana ufalme wa mbinguni unafanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake. 24Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta 10,000. 25Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru auzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe. 26Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, ‘Unisubiri nami nitakulipa deni lote’. 27Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake.
28“Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha dinari 100. Akamkamata, akamkaba koo akisema, ‘Lipa deni lako!’ 29Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, ‘Unisubiri nami nitakulipa’. 30Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni.
31“Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia. 32Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, ‘Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote. 33Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?’
34“Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote. 35Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote.”

Mathayo18;1-34

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: