Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 7 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 17....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!


Mtu mwovu hunaswa kwa uongo wake mwenyewe, lakini mwadilifu hutoka katika taabu. Mtu hufanikiwa kutokana na maneno yake kama apatavyo matokeo ya kazi za mikono yake.

Methali 12:13-14

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Mpumbavu huiona njia yake kuwa sawa, lakini mwenye hekima husikiliza shauri. Udhia wa mpumbavu hujulikana mara, lakini mwerevu huyapuuza matukano.

Methali 12:15-16

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Msema kweli hutoa ushahidi wa kweli, lakini shahidi wa uongo hutamka udanganyifu. Maneno ya ovyo hujeruhi kama upanga, lakini asemayo mwenye hekima huponesha kidonda.

Methali 12:17-18

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.



 Yesu anageuka sura

(Marko 9:2-13; Luka 9:28-36)
1Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu. 2Huko, Yesu akageuka sura mbele yao, uso wake ukangaa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama mwanga. 3Mose na Elia wakawatokea, wakawa wanazungumza naye. 4Hapo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.”
5 Taz Zab 2:7 Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka hilo wingu: “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni.” 6Wanafunzi waliposikia hivyo wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana. 7Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, “Simameni, msiogope!” 8Walipoangalia juu hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake.
9Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: “Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu.” 10Kisha wanafunzi wakamwuliza, “Mbona waalimu wa sheria wanasema ni lazima kwanza Elia aje?” 11Yesu akawajibu, “Kweli, Elia atakuja kutayarisha mambo yote. 12Lakini nawaambieni, Elia amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao.” 13Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane Mbatizaji.
Yesu anamponya mtoto mwenye pepo
(Marko 9:14-29; Luka 9:37-43a)
14Walipoufikia tena ule umati wa watu, mtu mmoja alimwendea Yesu, akampigia magoti, 15akasema, “Bwana, mwonee huruma mwanangu kwa kuwa ana kifafa, tena anateseka sana; mara nyingi yeye huanguka motoni na majini. 16Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.” 17Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia nyinyi mpaka lini? Mleteni hapa huyo mtoto.” 18Basi, Yesu akamkemea huyo pepo, naye akamtoka, na yule mtoto akapona wakati huohuo.
19Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo?” 20Yesu akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, iwe ndogo hata kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: ‘Toka hapa uende pale,’ nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu. [ 21Pepo wa namna hii hawezi kuondolewa ila kwa sala na kufunga.”]
Yesu anaongea tena juu ya kifo na ufufuo wake
(Marko 9:30-32; Luka 9:43b-45)
22Walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu aliwaambia, “Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu. 23Watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika mno.
Kulipa zaka ya hekalu
24Walipofika Kafarnaumu watu wenye kukusanya fedha ya zaka ya hekalu walimwendea Petro, wakamwuliza, “Je, mwalimu wenu hulipa fedha ya zaka?” 25Petro akajibu, “Naam, hulipa.” Basi, Petro alipoingia ndani ya nyumba, kabla hata hajasema neno, Yesu akamwuliza, “Simoni, wewe unaonaje? Wafalme wa dunia hukusanya ushuru au kodi kutoka kwa kina nani? Kutoka kwa wananchi ama kutoka kwa wageni?” 26Petro akajibu, “Kutoka kwa wageni.” Yesu akamwambia, “Haya basi, wananchi hawahusiki. 27Lakini kusudi tusiwakwaze, nenda ziwani ukatupe ndoana; chukua samaki wa kwanza atakayenaswa, fungua kinywa chake, na ndani utakuta fedha taslimu ya zaka. Ichukue ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”

Mathayo17;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: