Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 10 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 20....

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo.

Waroma 8:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu wa binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi.

Waroma 8:3

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho.

Waroma 8:4-5

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Wafanyakazi katika shamba la mizabibu
1“Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake. 2Akapatana nao kuwalipa fedha denari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu. 3Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi. 4Akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.’ 5Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo. 6Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, ‘Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?’ 7Wakamjibu: ‘Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.’ Naye akawaambia, ‘Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.’
8“Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, ‘Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.’ 9Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja fedha dinari moja. 10Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja. 11Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnungunikia yule bwana. 12Wakasema, ‘Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?’
13“Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa dinari moja? 14Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. 15Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?’”
16Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Yesu anasema mara ya tatu kuhusu kifo na ufufuo wake
(Marko 10:32-34; Luka 18:31-34)
17Yesu alipokuwa anakwenda juu Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia, 18“Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na waalimu wa sheria, nao watamhukumu auawe. 19Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.”
Ombi la mama wa Yakobo na Yohane
(Marko 10:35-45)
20Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu. 21Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.” 22Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.” 23Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.”
24Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili. 25Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao. 26Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; 27na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu. 28Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
Yesu anawaponya vipofu wawili
(Marko 10:46-52; Luka 18:35-43)
29Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata. 30Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” 31Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie!” 32Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?” 33Wakamjibu, “Bwana, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.” 34Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.

Mathayo20;1-34

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: