Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 14 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 22....

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua

na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi.

Waroma 8:13

Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona....

Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi.

Waroma 8:12-13

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!”

Waroma 8:14-15

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Mfano wa karamu ya harusi
(Luka 14:15-24) 
1Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: 2“Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi. 3Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. 4Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’ 5Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, 6na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. 7Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. 8Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. 9Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’ 10Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni. 11“Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi. 12Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya. 13Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’” 14Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.” 

Kulipa kodi kwa Kaisari 
(Marko 12:13-17; Luka 20:20-26) 
15Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. 16Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. 17Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?” 18Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu? 19Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha. 20Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” 21Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” 22Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.

 Suala juu ya ufufuo 
(Marko 12:18-27; Luka 20:27-40) 
23Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. 24Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. 25Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. 26Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. 27Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. 28Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” 29Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. 30Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. 31Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, 32‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” 33Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake. 

Amri kuu 
(Marko 12:28-34; Luka 10:25-28) 
34Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. 35Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, 36“Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?” 37Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’. 38Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza. 39Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’. 40Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.”

 Suala juu ya Kristo
 (Marko 12:35-37; Luka 20:41-44)
 41Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza, 42“Nyinyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Wa Daudi.” 43Yesu akawaambia, “Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema: 44 Taz Zab 110:1 ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’ 45Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo ‘Bwana,’ anawezaje kuwa mwanawe?” 46Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.


Mathayo22;1-46

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: