Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 3 September 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 15....


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Apendaye nidhamu hupenda maarifa, bali asiyependa kuonywa ni mjinga. Mtu mwema hufadhiliwa na Mwenyezi-Mungu, lakini mwenye nia mbaya hulaaniwa na Mungu.

Methali 12:1-2

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Mtu hawi imara kwa kutenda maovu, lakini hakuna kiwezacho kumngoa mtu mwadilifu. Mke mwema ni taji ya fahari kwa mumewe; amwaibishaye mumewe ni kama kidonda mifupani mwake.

Methali 12:3-4

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Mawazo ya mwadilifu ni ya haki; mashauri ya mwovu ni ya udanganyifu. Maneno ya waovu lengo lake ni kuua, lakini maneno ya waadilifu huwaokoa wanaotishwa.

Methali 12:5-6

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



 Mapokeo ya mababu

(Marko 7:1-13)
1Kisha Mafarisayo na waalimu wa sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza, 2“Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu? Hawanawi mikono ipasavyo kabla ya kula!” 3Yesu akawajibu, “Kwa nini nanyi hamjali sheria ya Mungu ila mnapendelea mapokeo yenu wenyewe? 4Mungu amesema: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima auawe.’ 5Lakini nyinyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema: ‘Kitu hiki nimemtolea Mungu,’ 6basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe. 7Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:
8‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu,
lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
9Kuniabudu kwao hakufai,
maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’”
Mambo yanayomtia mtu unajisi
(Marko 7:14-23)
10Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe! 11Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.”
12Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?” 13Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utangolewa. 14Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.” 15Petro akasema, “Tufafanulie huo mfano.” 16Yesu akasema, “Hata nyinyi hamwelewi? 17Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutolewa nje chooni? 18Lakini mambo yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. 19Maana moyoni hutoka mawazo ya uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa. 20Hayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”
Imani ya mama mmoja
(Marko 7:24-30)
21Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni. 22Basi, mama mmoja Mkanaani wa nchi hiyo alimjia, akapaza sauti: “Bwana, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo.” 23Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, “Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele.” 24Yesu akajibu, “Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.” 25Hapo huyo mama akaja, akamsujudia, akasema, “Bwana, nisaidie.” 26Yesu akamjibu, “Si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” 27Huyo mama akajibu, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao.” 28Hapo Yesu akamjibu, “Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka.” Yule binti yake akapona wakati huohuo.
Yesu anawaponya watu wengi
29Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi. 30Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya. 31Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; watu wakamsifu Mungu wa Israeli.
Yesu anawapa chakula watu elfu nne
(Marko 8:1-10)
32Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende zao bila kula, wasije wakazimia njiani.” 33Wanafunzi wakamwambia, “Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?” 34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba na visamaki vichache.” 35Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini. 36Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu. 37Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu saba. 38Hao waliokula walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.

Mathayo15;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: