Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 17 April 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 43...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

“Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uhai, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Kweli naja upesi.” Amina. Njoo Bwana Yesu! Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amina.
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Mwenyezi-Mungu anarudi hekaluni
1Kisha, yule mtu akanipeleka kwenye lango linaloelekea mashariki. 2Utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea upande wa mashariki. Pamoja nao kulikuwapo mshindo wa kuja kwake kama mshindo wa maji mengi, nchi ilingaa kwa utukufu wake. 3Maono hayo yalikuwa kama maono niliyoyaona Mungu alipokuja kuuangamiza mji wa Yerusalemu. Pia yalifanana na maono niliyoyaona karibu na mto Kebari. Nikaanguka kifudifudi.
4Nao utukufu wa Mwenyezi-Mungu uliingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya lango la mashariki. 5Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua na kunipeleka kwenye uwanja wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 6Yule mtu akiwa anasimama karibu nami, nilisikia mtu fulani akisema kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu; 7naye akaniambia, “Wewe mtu! Hapa ndipo mahali pa kiti changu cha enzi, mahali niwekapo nyayo za miguu yangu. Nitakaa miongoni mwa watu wa Israeli milele. Na Waisraeli hawatalitia unajisi jina langu, wao wenyewe, wala wafalme wao kwa kuziabudu sanamu au kuzika maiti43:7 Kuzika maiti za … au Kujenga minara ya ukumbusho kwa … za wafalme wao mahali hapa. 8Wafalme wao walijenga vizingiti na miimo ya ikulu zao karibu na vizingiti vya nguzo za hekalu langu, hivyo kati yangu na wao ulikuwa ni ukuta tu. Walilitia unajisi jina langu takatifu kwa machukizo yao waliyotenda, ndiyo maana nimewaangamiza kwa hasira yangu. 9Sasa na waache kuziabudu sanamu na waziondoe maiti za43:9 Waziondoe maiti za … au waondoe minara ya ukumbusho kwa … wafalme wao mbali nami, nami nitakaa miongoni mwao milele.
10“Sasa, ewe mtu, waeleze Waisraeli habari za nyumba ya Mungu na wajifunze ramani yake. Waaibike kutokana na machukizo yao waliyotenda. 11Wakiona aibu kutokana na matendo yao, waeleze ramani ya nyumba ya Mungu: Ramani yake yenyewe, milango ya kuingilia na kutokea, umbo lake lote, mipango ya kila kitu, kanuni zake na masharti yake. Waandikie hayo yote waziwazi ili waweze kuona yote yalivyopangwa na waweze kuzifuata kanuni na masharti yake. 12Hii ndiyo sheria kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Eneo lote linalozunguka nyumba ya Mwenyezi-Mungu juu ya mlima lazima liwe takatifu kabisa.”
Madhabahu hekaluni
13Vipimo vya madhabahu, vitakuwa vilevile kama vipimo vya hekalu. Kuuzunguka msingi wa madhabahu, kutakuwa na mfereji wenye kina cha sentimita 50 na upana wa sentimita 50, pamoja na ukingo wenye kina cha sentimita 25. 14Sehemu ya madhabahu itakayokuwa chini kabisa tokea juu ya msingi itakuwa na kimo cha mita 1. Sehemu itakayofuata itawekwa nyuma kutoka kwenye ukingo sentimita 50 kuzunguka, na kimo cha mita 2. Sehemu itakayofuata nayo itawekwa nyuma ya ukingo sentimita 50 kuzunguka. 15Sehemu hii ya juu, ambayo itatumika kuteketezea sadaka, itakuwa mraba, kila upande mita 2. Mjengo wa kona za sehemu hii ya juu zitainuka kuliko sehemu nyingine. 16Sehemu ya juu ya madhabahu itakuwa mraba, mita 6 kila upande. 17Sehemu ya katikati, itakuwa mraba, sentimita 7 kila upande, nayo itakuwa na ukingo pembeni wenye kimo cha sentimita 25. Kutakuwa na mfereji wenye upana wa sentimita 50. Na kutakuwa na vidato vya kupandia madhabahu upande wa mashariki.
Kuiweka wakfu madhabahu
18Bwana Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati madhabahu imejengwa, utaiweka wakfu kwa kutoa tambiko za kuteketezwa juu yake na kuinyunyizia damu ya wanyama waliotolewa sadaka. 19Wale makuhani walio wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki, ndio tu watakaonikaribia ili kunihudumia. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Utawapa fahali mchanga kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. 20Utatwaa damu yake na kuitia juu ya pembe nne za madhabahu na juu ya ncha nne za daraja na juu ya pambizo yake pande zote. Hivyo ndivyo utakavyoitakasa madhabahu na kuiweka wakfu. 21Utachukua pia fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi; watamteketeza katika mahali palipochaguliwa ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, lakini nje ya mahali patakatifu. 22Kesho yake, utatoa beberu asiye na dosari, kuwa sadaka ya kuondoa dhambi; madhabahu itatakaswa kama ilivyotakaswa kwa damu ya fahali. 23Utakapokwisha kuitakasa, utatwaa fahali mdogo asiye na dosari na kondoo dume mmoja asiye na dosari na 24kuwaleta mbele yangu. Makuhani watawapaka chumvi na kuwatoa kuwa tambiko ya kuteketezwa, kwa Mwenyezi-Mungu. 25Kwa muda wa siku saba, kila siku utatambika beberu mmoja awe sadaka ya kuondoa dhambi. Pia watatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja asiye na dosari. 26Hivyo kwa muda wa siku saba, utafanya upatanisho na kuitakasa, na hivyo kuiweka wakfu madhabahu. 27Baada ya siku hizo saba, tokea siku ya nane na kuendelea, makuhani watatoa sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani. Nami nitawakubali. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”



Ezekieli43;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)


"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: