Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 2 April 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 32...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, “Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?” Yesu akamjibu, “Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye. Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

“Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi, lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. “Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi nyinyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Mlikwisha sikia nikiwaambieni: ‘Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.’ Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi. Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu; lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Farao analinganishwa na mamba
1Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa kumi na mbili tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Imba utenzi wa kuomboleza juu ya Farao, mfalme wa Misri.
Wewe Farao unajiona kuwa simba kati ya mataifa,
lakini wewe ni kama mamba tu majini:
Unachomoka kwa nguvu kwenye mito yako,
wayavuruga maji kwa miguu yako,
na kuichafua mito.
3Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema:
Nitautupa wavu wangu juu yako,
nao watu watakuvua humo kwa wavu wangu.
4Nitakutupa juu ya nchi kavu,
nitakubwaga uwanjani,
nitawafanya ndege wote watue juu yako,
na kuwashibisha wanyama wote wa porini kwa mwili wako.
5Nitatawanya nyama yako milimani,
na kujaza mabonde yote mzoga wako.
6Nchi nitainywesha damu yako mpaka milimani,
mashimo yatajaa damu yako.
7 32:7 Taz Isa 13:10; Mat 24:29; Marko 13:24-25; Luka 21:25; Ufu 6:12-13; 8:12 Nitakapokuangamiza, nitazifunika mbingu,
nitazifanya nyota kuwa nyeusi,
jua nitalifunika kwa mawingu,
na mwezi hautatoa mwangaza wake.
8Nitaifanya mianga yote mbinguni kuwa giza,
nitatandaza giza juu ya nchi.
Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
9“Nitaihuzunisha mioyo ya watu wengi, nitakapokupeleka utumwani kati ya mataifa, katika nchi ambazo huzijua.
10Nitayashtusha mataifa mengi kwa habari zako,
wafalme wao watatetemeka kwa sababu yako,
nitakaponyosha upanga wangu mbele yao.
Watatetemeka kila wakati,
kila mtu akihofia uhai wake,
siku ile ya kuangamia kwako.
11Kwa maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Upanga wa mfalme wa Babuloni utakufuatia.
12Watu wako wengi watauawa kwa mapanga ya mashujaa,
watu katili kuliko mataifa yote.
Watakomesha kiburi cha Misri na kuwaua watu wako wote.
13Nitaiangamiza mifugo yako yote kando ya mto Nili.
Maji yake hayatavurugwa tena na mtu
wala kwato za mnyama kuyachafua tena.
14Hapo nitayafanya maji yake yatulie
na kuitiririsha mito yake kama mafuta.
Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
15“Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na mali yake yote kuchukuliwa, nitakapowaua wakazi wake wote, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
16“Huo ndio utenzi wa maombolezo,
wanawake wa mataifa watauimba,
wataimba juu ya Misri na watu wake wote.
Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.”
Nchi ya wafu
17Siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza,32:17 mstari wa 17 makala ya Kiebrania si dhahiri na haina: Mwezi wa kwanza. mwaka wa kumi na mbili tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 18“Wewe mtu! Waombolezee watu wengi wa Misri. Wapeleke chini kwenye nchi ya wafu pamoja na mataifa mengine yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao chini kwa wafu. 19Waambie:
Nyinyi ni wazuri kuliko nani?
Nendeni kuzimu mlazwe pamoja na wasiomjua Mungu!
20Watu wa Misri wataangamia pamoja na watu waliouawa vitani. Upanga uko tayari kuangamiza Misri pamoja na watu wake wengi. 21Wakuu wenye nguvu pamoja na wasaidizi wao wakiwa huko shimoni kwa wafu watasema hivi: ‘Wamisri wameshuka chini kwa wafu, wanalala pamoja na watu wasiomjua Mungu, waliouawa vitani.’
22“Waashuru wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Wote waliuawa vitani, 23na makaburi yao yako sehemu za chini kabisa shimoni kwa wafu. Wanajeshi wao wote waliuawa vitani na makaburi yao yamewazunguka. Hapo awali, walipokuwa wanaishi bado, walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.
24“Waelamu pia wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao waliouawa vitani. Wote hao wasiomjua Mungu walishuka kwenye nchi ya wafu. Walipokuwa wanaishi bado walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Lakini sasa wanabeba aibu yao pamoja na wanaoshuka shimoni kwa wafu. 25Wamelazwa na jeshi lao miongoni mwa wale waliouawa vitani. Wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wake wote waliouawa vitani na ambao wote hawamjui Mungu.32:25 hawamjui Mungu: Kiebrania ni hawakutahiriwa. Walipokuwa bado wanaishi walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai, na sasa wako hapo wamejaa aibu pamoja na wale waliouawa vitani.
26“Watu wa Mesheki na wa Tabali wote wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Watu hao wote wasiomjua Mungu walikufa vitani, watu ambao walipokuwa hai walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. 27Hao wasiomjua Mungu hawakuzikwa pamoja na mashujaa wa kale,32:27 wa kale: Kiebrania ni wa wasiotahiriwa. ambao walikwenda kuzimu kwa wafu wakiwa na silaha zao, mapanga yao chini ya vichwa vyao na ngao zao32:27 ngao zao: Kiebrania: Uovu wao. juu ya miili yao. Mashujaa hao walipokuwa wanaishi bado walijaza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. 28Basi, nyinyi Wamisri mtaangamizwa na kulazwa miongoni mwa wasiomjua Mungu waliouawa vitani.
29“Waedomu wako huko pamoja na wafalme wao na wakuu wao wote. Walipokuwa bado hai walikuwa na nguvu sana, lakini sasa wamelazwa kwa wafu pamoja na wasiomjua Mungu waliouawa vitani.
30“Viongozi wote wa watu wa kaskazini wako huko pia; hata Wasidoni wote walikwenda kujiunga na wafu. Walipokuwa bado wanaishi, walisababisha vitisho kwa nguvu zao, lakini sasa hao wasiomjua Mungu wamelazwa chini kwa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. Wanashiriki aibu ya wale walioshuka shimoni kwa wafu.
31“Farao, atakapowaona hao wote atafarijika kwa ajili ya wingi wa majeshi yake yote; mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. 32Nilimfanya Farao aeneze vitisho katika nchi ya walio hai, lakini sasa yeye mwenyewe pamoja na jeshi lake lote watauawa vitani na kulazwa pamoja na wasiomjua Mungu, waliokufa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”



Ezekieli32;1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)


"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: