Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 10 April 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Ezekieli 38...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!

Ilikuwa haki tupu kwamba Mungu, ambaye huumba na kutegemeza vitu vyote, alimfanya Yesu kuwa mkamilifu kabisa kwa njia ya mateso, ili awalete watoto wengi waushiriki utukufu wake. Maana Yesu ndiye anayewaongoza kwenye wokovu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Yeye anawatakasa watu dhambi zao, naye pamoja na wale waliotakaswa, wote wanaye Baba mmoja. Ndiyo maana Yesu haoni aibu kuwaita hao, ndugu zake;
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

kama asemavyo: “Ee Mungu, nitawasimulia ndugu zangu matendo yako. Nitakusifu katika kusanyiko lao.” Tena asema: “Nitamwekea Mungu tumaini langu.” Na tena: “Mimi niko hapa pamoja na watoto alionipa Mungu.”
Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.

Mfalme Gogu chombo cha Mungu
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Mgeukie Gogu mfalme wa nchi ya Magogu ambaye ni mtawala mkuu wa Mesheki na Tubali. 3Toa unabii juu yake na kumwambia kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana nawe ewe Gogu mtawala wa Mesheki na Tubali. 4Mimi nitakuzungusha na kukutia ndoana matayani mwako, na kukutoa nje wewe pamoja na jeshi lako lote: Farasi na wapandafarasi na kundi kubwa la watu wamevaa mavazi ya vita, ngao na vigao mikononi, wanapunga mapanga yao. 5Wanajeshi kutoka Persia, Kushi na Puti wako pamoja nao; wote wana ngao na kofia za chuma. 6Pia vikosi kutoka Gomeri, Beth-togarma, upande wa kaskazini kabisa, na majeshi yao yote pamoja na majeshi kutoka mataifa mengine, yako pamoja nawe. 7Jitayarishe, ukae wewe mwenyewe na jeshi lako lote pamoja na wengine wote ulio nao, ukawalinde.
8“Baada ya siku nyingi utaitwa kuishambulia nchi ambayo watu wengi waliletwa kutoka mataifa mengi na sasa wanaishi bila vitisho vya vita. Utaishambulia milima ya Israeli ambayo hapo awali ilikuwa jangwa na mahame kwa muda mrefu, lakini sasa watu wote huko wanaishi kwa usalama. 9Utakwenda kasi kama tufani na kuifunika nchi kama wingu, wewe mwenyewe na jeshi lako lote na mataifa mengi yaliyo pamoja nawe.
10“Wewe Gogu! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile itakapofika utaanza kuwaza moyoni mwako na kupanga mipango miovu na kusema: 11‘Nitakwenda kuishambulia nchi isiyo na kuta, nchi ambako wananchi wake wanaishi kwa amani. Wote wanakaa katika miji isiyo na kuta; hawana makomeo wala malango.’ 12Utapora na kuteka mali za watu wanaokaa katika miji ambayo ilikuwa jangwa. Watu hao wamekusanywa kutoka mataifa na sasa wana mifugo na mali; nao wanakaa kwenye kitovu cha dunia. 13Wakazi wa Sheba na Dedani pamoja na wafanyabiashara wa Tarshishi na vitongoji vyake watakuuliza, ‘Je, umekuja kuteka nyara? Je, umekusanya jeshi lako ili kushambulia na kutwaa nyara na kuchukua fedha na dhahabu, mifugo na bidhaa, na kuondoka na nyara nyingi?’
14“Kwa hiyo, ewe mtu, toa unabii na kumwambia Gogu kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wakati taifa langu la Israeli linaishi kwa usalama, wewe utafunga safari38:14 wewe … safari: Makala ya Kiebrania: Je, wewe hutajua? 15kutoka kwenye maskani yako, huko mbali kabisa kaskazini, uje pamoja na watu wengi wakiwa wote wamepanda farasi: Jeshi kubwa na lenye nguvu. 16Utawakabili Waisraeli, kama wingu linalotanda juu ya nchi. Wakati huo nitakutuma uishambulie nchi yangu, ili mataifa yajue kwamba nimekutumia wewe Gogu ili nioneshe utakatifu wangu mbele yao.
17“Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, wewe ndiwe niliyesema habari zako hapo kale kwa njia ya watumishi wangu manabii wa Israeli, ambao walitabiri nyakati zile kuwa baadaye nitakuleta upambane na watu wa Israeli.”
Mungu atamwadhibu Gogu
18Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Siku ile Gogu atakapoishambulia nchi ya Israeli, nitawasha ghadhabu yangu. 19Mimi natamka rasmi kwa wivu na ghadhabu yangu kali kwamba siku hiyo kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi nchini Israeli. 20Samaki baharini na ndege warukao, wanyama wa porini, viumbe vyote vitambaavyo pamoja na watu wote duniani, watatetemeka kwa kuniona. Milima itaporomoshwa, magenge yataanguka na kuta zote zitaanguka chini. 21Nami nitasababisha kila namna ya tisho kumkabili Gogu.38:21 Nami … Gogu: Makala ya Kiebrania si dhahiri. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Wanajeshi wake wataanza kushambuliana wenyewe kwa mapanga yao. 22Nitamwadhibu Gogu kwa magonjwa mabaya na mauaji. Nitanyesha mvua nyingi, mvua ya mawe na moto wa madini ya kiberiti juu yake, juu ya vikosi vyake, na mataifa yale mengi yaliyo pamoja naye. 23Ndivyo nitakavyofanya mataifa yote yaone ukuu wangu na utakatifu wangu. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”


Ezekieli38;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)


"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: