Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 30 April 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Danieli 4...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako

Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya?
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.” Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia. Wakapaita mahali hapo Bokimu. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....

Nawapenda.

Ndoto ya pili ya mfalme Nebukadneza
1“Mimi mfalme Nebukadneza, nawaandikia watu wa makabila yote, mataifa yote na lugha zote kote duniani. Nawatakieni amani tele! 2Nimeona vema kuwajulisha ishara na maajabu ambayo Mungu Mkuu amenionesha.
3Jinsi gani zilivyo kubwa ishara zake Mungu!
Maajabu yake ni makuu mno!
Ufalme wake ni ufalme wa milele;
enzi yake yadumu kizazi hata kizazi.
4“Mimi, Nebukadneza, nilikuwa ninaishi raha mstarehe nyumbani kwangu na kufana katika ikulu yangu. 5Lakini nikaota ndoto iliyonitisha; nikiwa nimelala kitandani, mawazo na maono kichwani mwangu yaliniogopesha. 6Hivyo, nikaamuru wenye hekima wote wa Babuloni waletwe mbele yangu ili wanieleze maana ya ndoto hiyo. 7Ndipo waganga, walozi, Wakaldayo na wanajimu wakaletwa. Nikawasimulia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunieleza maana yake. 8Baadaye, akaja Danieli, anayeitwa pia Belteshaza, jina la mungu wangu, ambaye roho ya miungu4:8 miungu: Au Mungu. mitakatifu imo ndani yake. Nami nikamsimulia ndoto yangu, nikasema: 9Ee Belteshaza, uliye mkuu wa waganga, nafahamu kuwa roho ya miungu4:9 miungu: Au Mungu. mitakatifu imo ndani yako, na kwamba hakuna fumbo lililo gumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu; niambie maana yake.
10“Nilipokuwa nimelala, niliona maono haya: Niliona mti mrefu sana katikati ya dunia. 11Mti uliendelea kukua, ukawa imara na kilele chake kikafika mbinguni. Uliweza kuonekana kutoka kila mahali duniani. 12Majani yake yalikuwa mazuri. Ulikuwa umejaa matunda, kiasi cha kuitosheleza dunia nzima. Wanyama wote wa porini walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Viumbe vyote vilipata chakula kutoka mti huo.
13“Nilipokuwa nimelala kitandani, niliona maono: Mlinzi mtakatifu alishuka kutoka mbinguni. 14Akapaaza sauti akisema, ‘Kateni mti huu na kuyakatakata matawi yake. Pukuteni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na watoroke chini yake na ndege kutoka matawi yake. 15Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini, kwenye majani mabichi ya kondeni kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini na kula nyasi mbugani. 16Akili yake ya utu ibadilishwe, awe na akili ya mnyama kwa miaka saba. 17Hii ni hukumu iliyotangazwa na walinzi; ni uamuzi wa walio watakatifu, ili wanaadamu wote kila mahali wapate kutambua kuwa Mungu Mkuu anayo mamlaka juu ya falme zote za wanaadamu; yeye humpa ufalme mtu yeyote ampendaye, humfanya mfalme hata mtu duni wa mwisho.’
18“Hii ndiyo ndoto niliyoota mimi Nebukadneza. Sasa, wewe Belteshaza, nieleze maana yake; kwani wenye hekima wote katika ufalme wangu hawawezi kuniambia maana yake; lakini wewe utaweza kwa kuwa roho ya miungu4:18 miungu: Au Mungu. mitakatifu imo ndani yako.”
Danieli anaeleza maana ya ndoto
19Hapo, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akamwambia, “Belteshaza, ndoto hii, wala maana yake visikufadhaishe!” Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii na maana yake ingewahusu adui zako! 20Mti uliouona ukiwa mkubwa na wenye nguvu, ambao matawi yake marefu yalifika mbinguni, nao ukionekana kutoka kila mahali duniani, 21majani yake yakiwa mazuri, na matunda yake mengi ya kulisha viumbe vyote, wanyama wa porini wakipata kivuli chini yake, na ndege wa angani wakikaa katika matawi yake, 22basi, ni wewe ee mfalme ambaye umekuwa mkubwa na mwenye nguvu. Ukuu wako umefika mpaka mbinguni, na ufalme wako umeenea mpaka miisho ya dunia. 23Kisha ukaona tena, ee mfalme, Mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akaamuru: ‘Ukateni mti huu, mkauangamize. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini kwenye majani mabichi ya kondeni, kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini kwa miaka saba.’
24“Hii basi, bwana wangu, ndiyo maana ya ndoto yako, kadiri ya uamuzi wa Mungu Mkuu juu yako: 25Wewe utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini, utakula majani kama ng'ombe; utalowa kwa umande wa mbinguni. Utakaa katika hali hiyo kwa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye. 26Tena amri ile ya kukiacha kisiki na mizizi ya mti huo ardhini ina maana hii: Wewe utarudishiwa tena ufalme wako hapo utakapotambua kwamba Mungu wa mbinguni ndiye atawalaye. 27Kwa sababu hiyo, ee mfalme, sikiliza shauri langu. Achana na dhambi zako na maovu yako, utende haki na kuwaonea huruma waliodhulumiwa; huenda muda wako wa fanaka ukarefushwa!”
Maana ya ndoto inatimia
28Hayo yote yalimpata mfalme Nebukadneza. 29Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme Nebukadneza alikuwa anatembea juu ya dari ya ikulu ya mji wa Babuloni. 30Basi, akasema kwa sauti, “Tazama Babuloni, mji mkuu nilioujenga kwa nguvu zangu uwe makao yangu ya kifalme na kwa ajili ya utukufu wangu!” 31Mara tu alipotamka maneno hayo, sauti kutoka mbinguni ikatamka: “Ewe mfalme Nebukadneza, sikiliza ujumbe huu juu yako! Ufalme umekutoka! 32Utafukuzwa mbali na wanaadamu! Utaishi pamoja na wanyama wa porini kondeni, na utakula majani kama ng'ombe! Utakaa katika hali hiyo kwa muda wa miaka saba, na mwishowe utatambua kwamba Mungu Mkuu ndiye mwenye uwezo juu ya falme za wanaadamu, na humpa ufalme mtu yeyote amtakaye.”
33Mara moja jambo hilo juu ya mfalme Nebukadneza likatekelezwa. Alifukuzwa mbali na wanaadamu, akawa anakula majani kama ng'ombe. Alilowa kwa umande wa mbinguni, na nywele zake zikawa ndefu kama manyoya ya tai, na kucha zake kama za ndege.
Nebukadneza anamsifu Mungu
34“Mwishoni mwa ile miaka saba, mimi Nebukadneza niliinua macho yangu kutazama juu mbinguni na akili zangu zikanirudia. Nilimshukuru Mungu Mkuu na kumheshimu yeye aishiye milele:
Kwa sababu enzi yake ni enzi ya milele,
ufalme wake wadumu kizazi hata kizazi.
35Wakazi wote wa dunia si kitu;
hufanya atakavyo na viumbe vya mbinguni,
na wakazi wa duniani;
hakuna awezaye kumpinga,
au kusema ‘Unafanya nini?’
36“Wakati huo huo akili zangu zikanirudia; nilirudishiwa pia heshima yangu, fahari yangu na utukufu wa ufalme wangu. Washauri na maofisa wangu walikuja kunitafuta, nikarudishwa katika ufalme wangu na kupata heshima kama pale awali.
37“Na sasa, mimi Nebukadneza ninamsifu na kumtukuza na kumheshimu mfalme wa mbinguni. Maana matendo yake yote ni ya haki, naye huwashusha wenye kiburi.”

Danieli4;1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: